Reader Settings

Ilikuwa ni  Jumapili  tulivu  , kwa wale wakristo waliokuwa wakienda kanisani  walikuwa wakienda na kwa wale ambao walikuwa ni  wa dini nyingine  walikuwa na pilipilika za mambo mengine za Maisha yao.

Roma kama kawaida yake aliamka asubuhi asubuhi na kwenda kufanya mazoezi  ya hapa na pale ili kuweka mwili wake katika hali nzuri , kwa upande wa Bi wema alikuwa bize na kuandaa kifungua kinywa  kwa siku hio na kwa upande wa Edna alikuwa bize na kusoma kama ilivyokuwa kawaida yake , aliamini matatizo yake yote yanaweza kutatuliwa na kusoma na ndio maana aliamini katika kusoma sana.

Alijitahidi kusoma kwa muda , lakini akili yake haikuwa ni yenye kutulia  , alionekana kuna jambo lilikuwa likimuumiza kichwa kwani alikosa utulivu , baada ya kuona  haelewi kile alichokuwa anakisoma alisogelea tarakishi yake ya mapakato  na kuingia kwenye mtandao wa  Google na kuanza kutafuta taarifa zinazohusiana na  macho ya mtu kubadilika Rangi , lakini kila majibu yaliokuwa yamekuja yalionekana kutokumridhisha kabisa na kukosa jibu alilokuwa analitaka.

“Au nimuulize mimi mwenywe kwanini macho yake yanabadilika Rangi?” Aliwaza  mrembo huyu huku akiwa amevalia kigauni chake  kilichoufanya mwili wake mnene kiasi kupendeza.

“Ila  naamini siku  moja ataniambia mwenyewe kwanini yuko vile , sitakiwi kumuuliza”Alijiibu mwanamke huyu huku akiona hayupo kwenye nafasi ya kumuuliza mume wake Roma kwanini macho yake yanabadilika rangi anapokuwa na hasira kali.

Saa mbili kamili za asubuhi  Edna alishuka chini kwa ajili ya kupata kifungua kinywa baada ya kuitwa na Bi Wema , Roma alikuwa tayari yupo mezani , na alikuwa anamsubiria mke wake waanze , baada ya Edna kuketi wanafamilia hawa watatu ndani ya jumba hili kubwa la kifahari walianza kupata kifungua kinywa chao ambacho kwa familia za Maisha ya chini wangedhania moja kwa moja aina hio ya chukula ni kwa ajili ya sherehe.

“Miss unaonaje ukienda na Mr Roma leo  kituoni?”Aliongea Bi Wema na kupendekeza .

“Bi Wema kituo gani?”Aliuliza Roma

“Kuna kituo cha kulelea yatima kipo Mkoa wa pwani  Bagamoyo Kiwangwa, Ni kituo ambacho  kampuni  inakifadhili na imekuwa utamaduni kila jumapili Miss Edna kwenda huko kuwatembelea Watoto hao na kuwapelekea baadhi ya mahitaji muhimu”Roma alishangaa.

Edna alimwangalia Roma  , hakuwa akipinga swala hilo la kwenda nae  , kwanza kabisa mrembo huyu alipanga kujiweka kidogo karibu na Roma ili kuweza kujua ni kwanini  macho yake yanabadilika Rangi , aliamini kama watakuwa  marafiki   Roma anaweza kumfungukia.

“Bi Wema kama mke wangu anapenda kuongozana na mimi nipo tayari , isitoshe leo  sina pakwenda na sijazoea kukaa ndani”Aliongea Roma.

“Roma itakuwa vizuri kama tutaenda wote  , unisaidie  kwenye kubeba  mizigo ya kwenda nayo”Aliongea Edna  na Roma aliitikia kwa kichwa.

Baada ya nusu saa Roma alikuwa ashajiandaa kwa ajili ya  kuianza safari ya kuelekea  Bagamoyo , alikuwa sebuleni akimsubiria Edna ambaye kama ilivyokuwa tabia ya wanawake kujiandaa muda mrefu Edna alichukua  lisaa mpaka kuonekana akiwa anashuka.

Roma siku zote alikuwa akijivunia hata kuitwa mume wa Edna , kwani mwanamke huyu hata avae nini , alikuwa akipendeza  sana na kuvutia,Edna alikuwa amevaa  leo Suruali ya jeans rangi ya Bluu  iliomfanya umbo lake kuonekana vyema, na kishati flani kitambaa mtelezo mikono mirefu , na akakikunJa hadi kwenye kiwiko cha mikono , chini  akiwa amevalia viatu vyeupe kama Raba  Rangi ya pink.

Edna alimpa Roma ufunguo na  Roma alitangulia mpaka sehemu ya kuegeshea magari na kubonyeza Rimoti na Pickup  aina ya Cadillac Escalade EX ili Tweak na kuwasha taa  ,Roma alitabasamu na ufahari wa hii gari  , aliitoa na kuleta mpaka katikati  na Edna aliingia.

Bi Wema aliekuwa  juu ya Gorofa alikuwa akitabasamu kwa furaha  baada ya kuona  Edna na Roma wakitoka , alijiambia ni mwenye akili  sana  kushauri waende pamoja.

“Kuanzia sasa misheni yangu ni kuhakikisha  wanafanya mambo kwa pamoja , hii itawaongezea kuwa karibu” Aliwaza Bi Wema  huku akijiona   jasusi mbobezi likija swala la mapenzi.

Safari ya wanandoa hawa iliishia  Mliman City , Watu waliokuwa  ndani ya eneo hili waliwaangalia kwa macho  ya tofauti kabisa huku kila mtu akiwa na mawazo yake ,Edna alikuwa amevalia miwani ambayo ilimfanya apendeze  lakini yeye hakuvaa kwa ajili ya kupendeza , alikuwa  amevaa kwa ajili ya kufanya watu wasimtambue.

Roma alievalia jeans  lake Rangi nyeusi na koti la Ugolo  alijongea upande upande na mke wake , huku akijisikia fahari namna ambavyo  wanaume wa eneo hili walivyokuwa wanamwangalia   kwa macho ya wivu.

Walinunua mahitaji mengi ndani maduka ya vyakula  , baadhi ya nguo , taulo za kike na makolo koloo mengi sana ambayo yalikwa ni sehemu ya  mahitaji ya Watoto , walichukua na baadhi ya zawadi  kwa Watoto hao ikiwemo biskuti pipi na vitu vingine.

Baada ya kumaliza kufanya manunuzi , Roma  kusaidiana na baadhi wafanya kazi  walipakia  huku Edna akiwa bize kulipia.

Wakati Roma akiwa bize kupandisha vitu , mara alisikia sauti iliokuwa ikimuita nyuma  yake , sauti ya kike ambayo alikuwa akifahamu vyema, alikuwa ni mrembo Doris ambaye  alikuwa akiegesha gari yake , akiwa yupo peke yake aliependeza kama kawaida.

“Doris !”Aliongea Roma kwa kushangaa  baada ya kumuona mrembo huyu mbele yake.. wakati Doris  anamwangalia  Roma kwa mshangao  mara alikuja  Edna na kwenda kusimama  karibu na  Roma.

“Edna!”Macho yalimtoka Doris , hakuelewa ni kwanini wawili hao wako  pamoja .

“Vipi Doris umekuja kufanya Shopping?”Aliuliza Edna wa kwanza baada ya kuona Dorisi yupo kwenye mshangao  pasipo kuongea neno.

“Ndio Edna , lakini kwanini upo na Roma?”

“Nisamehe Dorisi  rafiki yangu  , nadhani unakumbuka nilikuambia nina mume?”

“Usiniambie Edna huyu ndio mumeo na siku zote huniambii?”.

“Ndio Dorisi huyu ni mke wangu,Tunaelekea  Bagamoyo na muda unaenda   tutaongea Zaidi”Aliongea Roma  akikata mazungumzo hayo , hakutaka  waendeleee kusimama ndani ya eneo hilo la maegeisho ya magari

“Nitakupigia simu Doris , tutaongea”Aliongea Edna  na Roma alimshika bega Edna na kumsukumizia ndani na kufunga mlango na kisha akazunguka  upande wa dereva na kuingia ndani na kuliwasha huku  wakimwangalia Doris aliekuwa amesimama  akiangalia gari yao ikitokomea.

“F**ck you Roma , siku zote unanichora  tu  kumbe  mkeo ni Edna  , halafu kwanini Edna hajaniambia”Alijiongelesha mwenyewe na kusahau kuwa baadhi ya watu walikuwa wakimshangaa , alifuta machozi kwa mkono ambayo yalikuwa yashaanza kujitengeneza ndani ya mboni za macho yake na kufungua mlango wa gari  na kuingia na kisha akatoa gari ndani ya eneo hilo , alionekana  kughairi , alichokuwa amefata hapo.

“Doris atakuwa amekasirika”Alianzisha maongezi  Edna wakati wakipita Lugalo.

“Kwanini  unasema hivyo?”

“Doris ni Rafiki yangu wa muda mrefu na niseme ni Zaidi ya Rafiki yangu , tumekuwa pamoja kwa muda mrefu kidogo ,  nilimwambia nimeolewa  na kumuhaidi nitakutambulisha kwake lakini sikufanya hivyo na leo ametuona pamoja , kama marafiki atakasirika na kujisikia vibaya”.

“Mke wangu  usiwe  ni mwenye wasiwasi , Doris ni Rafiki yako na wewe ulikuwa pia na sababu za kutonitambulisha kwake  mapema , hivyo atakuelewa , isitoshe hatuna muda mrefu tokea tumesajili ndoa yetu”.Edna aliitikia kwa kichwa.

“Kila jumapili unakujaga huku kutembelea   kituo?”Aliuliza Roma  kwa makusudi a ya kubadilisha stori.

“Ndio , imekuwa utamaduni  , kila jumapili lazima nitembelee , napenda Watoto  na najisikia faraja ninapokuwa nao karibu”.

“Mke wangu nilijua  wewe ni kauzu  kila sekta , kumbe una upande wako mwingine  ambao sikuwa nikiufahamu”.

“Mimi sio kauzu ila napenda kuwa siriasi kwenye maeneo yanayonitaka kuwa hivyo , sipo kama wewe kila  eneo haupo siriasi”.

“Kwa hio mke wangu wewe unataka niwe vipi?”Edna hakujibu aliendelea kukaza macho  barabarani na Roma hakutaka kuongea Zaidi.

Ni masaa machache tu walikuwa washafika  ndani ya kituo hiki , kilikuwa ni kituo kikubwa sana, kilikuwa na majengo makubwa kama chuo , jambo ambalo  lilimshangaza Roma.

“Mke wangu hiki kituo ni kikubwa ni shirika gani limejenga hiki kituo?”

“Sio shirika ni  mke wa raisi wa Kenya  ndio amejenga hapa Tanzania”Roma alishangaa ,yaani  mke wa raisi atoke  Kenya kwao ambako kuna  Watoto wengi waliozagaa mtaani aje ajenge  Tanzania , alishangazwa na jambo hilo.

“Kwanini ajenge Tanzania sio  Kwao Kenya?”

“Hata Kenya kajenga vituo vingi tu  na sio Kenya wala Tanzania ,Uganda , Rwanda  na Kongo kajenga  vituo vinavyofanana hivi hivi, ni mwanamke ambaye ana moyo mzuri sana na anasifika sana  ndani ya Afrika kwa kuisadia jamii.

Roma alitingisha kichwa baada ya kupewa jibu hilo na mke wake  , aliona huyo mwanamama anapaswa kupewa tuzo kwa msaada mkubwa ambao anaufanya kwa  jamii zenye uhitaji.

Kitendo cha kumaliza kuegesha Gari Tu ni kama Watoto waliokuwa ndani ya hili eneo walikuwa wakimsubiria Edna kwani  kundi lote lilimkimbilia na kumzingira huku wakionyesha furaha yake na Edna na yeye hakuwa nyuma , alionekana kufurahi kweli  uwepo wa Watoto  na kwa mara ya kwanza Roma anamshuhudia Edna  akiwa na furaha  sana.

“Sikujua mke wangu kumbe mzuri hivi akicheka , halafu anaonekana kuwa na moyo mzuri sana , kanaigiza tu kuwa siriasi”Aliwaza Roma   huku Watoto hao wakiwa hawana habari nae.

“Edna karibu” Aliongea mwanamama mmoja hivi mnene mwili wa kibonge  mwenye umri si chini ya hamsini hivi alikuwa wa maji ya kunde.

“Asante Mama  Issa ”Alijibu  Edna aliekuwa  akiwaangalia Watoto hawa , lakini kwa upande wa yule mama alimwangalia Roma na hapa ndipo Edna aliekuwa amemshau Roma akainuka.

“Mama Issa  Watoto wamenifanya nisahau kukutambulisha , huyu ni mume wangu anaitwa  Roma Ramoni” Mama huyu macho yalimtoka  kwa mshangao huku Roma akiwa ni mwenye kutabasamu , alijiuliza   huyu mwanaume ana nini mpaka kupata nafasi katika maisha ya Edna.

“Sikujua.. kumbe umepata mume Edna .. jamanii.. karibu baba  mimi naitwa Tabea  Singano  ni mkuu  wa hiki kituo”Aliongea mama huyu huku akionyesha furaha yake waziwazi , alionekana pia ni mtu ambaye alitamani siku moja Edna kumtambulisha mume wake kwake.

“Nashukuru sana kukufahamu Mama”.

“Karibu sana , unabahati sana kumpata Edna katika Maisha yako , umchunge sana”Aliongea  mwanamama huyu huku Edna hata hakuwa akiwasikia , kwani alikuwa bize na Watoto    aliokuwa akiwabeba mmoja mmoja juu.

Walishusha mizigo kwa kusaidiana na wafanya kazi  wa hapa ndani , na Roma pia alisaidia katika kazi hio na baada ya zoezi hilo dogo kuisha Edna na Roma walichukua zawaidi walizokuwa wamekuja nazo na kuanza kuzigawa kwa Watoto hao .

Roma alimkubali sana  aliejenga hiki kituo kutokana na wingi wa Watoto hao  , kilikuwa mpaka na shule kubwa ya msingi mpaka sekondari  , ni kituo ambacho kilionesha kujitosheleza sana kwa kila kitu.

Mama Issa  alimchukua Roma na kuanza kumtembeza ndani ya kituo hichi , kwa kumuonesha baadhi ya huduma ambazo wanatoa  kwa Watoto hawa ya  kimalezi , mama huyu alionekana kuwa mkarimu sana.

“Edna ni   msichana wa kipekee sana ,nimemuona akikua kwanzia alivyokuwa mdogo”Roma alishanga

“Mlikuwa maishi majirani?”.aliuliza Roma na mwanamama huyu alitabasamu.

“Hapana , wakati wa utoto wake alikuwa akija na bibi yake hapa mara kwa mara kucheza na Watoto na naweza kusema Muda wake wa utoto  mwingi alicheza na Watoto ambao walikuwa kwenye hiki kituo”Aliongea mama huyu na kumfanya Roma ashangae , na wakati huu walikuwa wakiingia ndani ya mejengo ya ofisi  hizi za  kituo hiki kilichokuwa kinafahamika kwa jina la Son and Daughter Orphanage(SDO)..

Roma  baada ya kuingia ndani ya  hii ofisi kubwa ya  mama Issa  alijikuta akishangaa picha iliokuwa juu ya ukuta ,ilikuwa ni picha ya mwanamama  mmoja  maji ya kunde aliekuwa kwenye pozi la kutabasamu, kichwa chake kilianza   kuuma na  kupiga kama Radi na picha picha za matukio zikianza kupita .. macho yake yalianza kubadilika palepale na kuwa ya kijani.

Previoua Next