Reader Settings

“Ukurasa umefunguka. Lakini kila neno lina gharama yake.”

Usiku huo, mvua iliendelea kunyesha polepole, ikilainisha udongo wa njia ya kuelekea kanisani. Padre Ian na JackXavier walitembea kimya kimya, miguu yao ikitumbukia kwenye tope baridi la Lushoto. Ilikuwa ni safari fupi kwa umbali, lakini ndefu kwa hisia.

Walipofika katika nyumba ya wageni ya parokia, Padre Ian alifungua mlango wa chumba kidogo kilicho na godoro dogo, meza ndogo ya mbao, na mshumaa mmoja uliokuwa uking’aa kwa mwanga wa dhahabu hafifu. Ukutani kulining’inia msalaba wa chuma, umechokwa na wakati lakini bado ukiwa na uthabiti wa imani.

“Pumzika, kesho tutaanza mchakato wa maandalizi,” Padre Ian alisema kwa sauti ya upole, akimkabidhi Jack shuka na kikombe cha chai ya tangawizi.

Jack hakuongea. Aliketi tu pembeni mwa godoro, akishika kikombe kama mtu anayeshika roho yake.

Lakini usiku haukuwa mtulivu kwake. Baada ya kunywa chai yake Jack aliingia kulala kwani alikuwa amechoka mnoo.

Kwa mara ya kwanza katika maisha yake, Jack aliota.

Alijikuta amesimama katika bustani ya ajabu, yenye mwanga laini wa dhahabu unaotiririka kutoka juu kama mvua ya nyota. Bustani hiyo haikuwa ya kawaida, ilikuwa na safu kubwa za sanamu 1,999, kila moja ikiwa imechongwa kwa sura tofauti, mavazi tofauti, na ishara za kipekee.
Zilikuwa kama mashahidi wa muda. Kimya. Lakini hai.

Ghafla, moja ya sanamu ilianza kutembea.

Ilikuwa ni ndefu, imevalia ngozi ya simba, mkanda wa mikuki mgongoni, na macho mekundu yaliyojaa moto wa maarifa. Alimkaribia Jack na kusema kwa sauti nzito:

"I am the Sharp Spear. Guardian of the Memories. You have unlocked the first gate."

“Mimi ni Mkuki Mkali. Mlinzi wa Kumbukumbu. Umefungua mlango wa kwanza.”

Sharp Spear alinyoosha mkono wake, na mbele yao kikatokea Kitabu cha Majira – Juzuu ya Kwanza, kikielea angani hadi mikononi mwa Jack. Kila ukurasa ulitoa sauti ya upepo wenye historia.
Jack aliponyoosha mkono kuugusa ukurasa wa kwanza, upepo wa giza ukatanda. Anga likabadilika. Sanamu nyingine zikaanza kugeuka na kupiga kelele za onyo.
Sauti moja ikatokea kutoka mbali sana, nzito kama sauti ya dunia yenyewe:

“Bado hujatakaswa…”

Ndoto ikavunjika. Jack akaamka kwa ghafla, jasho likimtoka, na moyo ukimpiga kwa kasi kifua.

Asubuhi ilipofika, Padre Ian alikuja chumbani na kumpa Jack chakula cha moto na daftari la kuandika. Waliketi pamoja kimya, huku Padre akimchochea Jack azungumze tena.
Badala ya maneno, Jack alichukua kalamu na kuanza kuchora:
Alichora saa yenye umbo la hourglass pamoja na umbo la spiral, yenye nukta 1,999 ndani yake.

Padre Ian alitazama mchoro huo kwa mshangao. Alishindwa kuvumilia na kuuliza kwa hamasa:

“Umeiona wapi hii Jack?” aliuliza, sauti yake ikiwa ya hofu na tumaini kwa wakati mmoja.

Jack hakujibu. Alimtazama tu. Lakini macho yake yalikuwa na maana kubwa kuliko maelezo yoyote.

📩 Barua Kutoka Vatican

Mchana huo, kupitia kasisi mkuu wa parokia, barua ilifika: Vatican ilikuwa imeidhinisha rasmi scholarship ya kimataifa kwa Jack.
Masharti yalisema: kabla ya kusafiri, Jack lazima afanyiwe vipimo vya afya ya mwili na akili katika kituo maalum jijini Dar es Salaam.

Safari ikapangwa kwa siku mbili zijazo.

Wakiwa njiani kuelekea Dar es Salaam ndani ya gari la parokia, mvua ilikuwa imetulia. Anga lilikuwa limefunikwa na wingu jeusi lenye mpasuko wa nuru ya jua upande wa mashariki. Padre Ian alikuwa akiendesha kimya kimya, huku redio ya gari ikicheza nyimbo za Injili kwa sauti ya chini.
Jack aliegemea dirishani, macho yake yakifuatilia mandhari ya milima inayopita kwa kasi ya taratibu. Lakini ndani yake kulikuwa na msongamano wa hisia — sauti yake ya kwanza, safari ya ghafla, ndoto ya ajabu.

Kisha, ulimwengu ukatetemeka kidogo, si kwa macho ya Padre, bali kwa ya Jack pekee.

Mara moja, dirisha la mbele la gari lilianza kutikisika kama maji, na barabara ilififia kama picha inayooshwa na mvua.
Miti ikapinda kana kwamba ilikuwa inahema. Anga likabadilika na kuwa rangi ya zambarau ya iliyokolea sana, kama anga lililovunjika usiku wa kale.

Jack hakuona gari, wala Padre Ian. Alikuwa peke yake — ameingia ndani ya Wingu la Kumbukumbu.

Kila upande alipoangalia, mandhari yalijibadilisha mbele ya macho yake kama kurasa za kitabu kilicho hai:

  • Vita vya mapanga vikilipuka katikati ya kijiji kilichojaa moshi — sauti za nderemo, vilio na vishindo vya silaha.
  • Majiji ya anga yenye magari yanayoruka juu ya barabara za nuru, miinuko ya vioo vinavyoteleza angani.
  • Watoto wakicheza na maji, lakini si kawaida — walikuwa wakiyainua kwa mikono yao, wakichezesha mizunguko ya maji angani kama wachoraji wa mvua.
  • Nyumba za udongo, lakini kuta zake zilikuwa dhahabu — zikiangaza kwa alama za kale zinazong’aa kama miiba ya mwanga.

Na pale, katikati ya yote hayo, macho elfu moja mia tisa tisini na tisa yalimtazama — kila njozi ikiwa tofauti: ya vita, ya huruma, ya uchovu, ya tumaini.

Halafu… sauti zikaja.

Zote kwa wakati mmoja. Sauti zilizovunjika. Zilizoteseka. Zilizoimba. Zilizolia.
Zikimwita.

“Mwangalizi wa Mwisho…”

Naye Jack anazungumza kimoyomoyo, kama mtu anayeanguka ndani ya kitu kikubwa kuliko yeye)

“Sijawahi kulala nikiwa salama.
Sijawahi kuamka nikijua nipo salama.
Lakini kwa mara ya kwanza, dunia inanivuta, si kwa mateso — bali kwa jambo ambalo sijui.
Ni kama kuna mlango niliuzoea kufunga kwa nguvu kila siku, sasa umeamua kufunguka wenyewe.
Na nyuma yake…
Si hofu. Si huzuni.
Ni sauti. Ni macho. Ni kumbukumbu ambazo si zangu, lakini… zinajua jina langu.
Mimi ni nani?
Mbona najua mahali ambako sijawahi kuwa?
Mbona najua vita ambavyo sijawahi kupigana?
Mbona nawakumbuka watu ambao sijawahi kuwaona?
Mbona macho yao yananikumbuka?”

“Wanasema mimi ni mwangalizi.
Wanasema mimi ni wa mwisho.
Lakini hakuna aliyeniambia mimi ni nani kwa mara ya kwanza.
Na sasa… sauti hizi zinataka niwasikie.
Sina uwezo wa kuzikimbia tena.
Kwa hiyo — nisikilize.
Niambie.
Niandike.
Nione.”

Jack alijikuta anakumbatia kichwa chake kwa mikono miwili. Sauti hizo hazikuwa tu zikizungumza tu — zilikuwa zikimiminika ndani yake, zikimwandika upya.
Ndoto. Maumivu. Historia. Kumbukumbu. Vizazi.
Vitu ambavyo hakuwahi kuishi, lakini vilimjua.

Halafu ghafla — kimya.

Mandhari yakafifia. Anga zambarau ikarudi kuwa buluu ya kawaida. Miti ikasimama. Dirisha la gari likarudi kuwa kioo tu.

“Jack!” Padre Ian aligeuka kwa hofu. “Uko sawa?”

Jack hakumwangalia. Kwa muda alibaki kimya, akitafuta pumzi kati ya ukweli na maono. Kisha, kwa sauti ya pole lakini thabiti, alisema:

“Tupo wapi?”

Lakini swali hilo halikuwa tu kuhusu mahali.
Lilikuwa kuhusu wakati.
Na kuhusu nafasi aliyopo sasa katika dunia ambayo haifuatili tena mistari ya kawaida ya muda.

🌃 Ndoto ya Pili: Kugeuza Ukurasa

“Ukurasa umefunguka. Lakini kila neno lina gharama yake.”

Usiku huo baada ya kufika Dar es Salaam, Jack hakuwa peke yake.

Alipowasili na Padre Ian katika Makao Makuu ya Kanisa Katoliki, waliingia katika jengo kubwa lenye ukuta wa mawe meupe uliopambwa na vitasa vya zamani vya shaba. Milango ya mbao ilifunguliwa kwa mapokezi ya kipekee masista wawili waliovaa vitambaa vyeupe walikimbia kuwakaribisha, wakatabasamu kwa furaha ya kweli.

“Karibu sana, Padre Ian... na huyu ndiye yule mtoto?”

Habari za JackXavier tayari zilikuwa zimeenea kwenye dayosisi nyingi, mvulana bubu, aliyesema neno moja tu, na hilo neno likabadilisha hatima yake. Kila mtu pale alimtazama kama vile alikuwa sehemu ya unabii ambao hawakuelewa kikamilifu, lakini waliuhisi.

Walipokelewa kwa upendo: walipata maji safi ya kunywa, na baadaye walikaribishwa kwenye meza ya chakula ya jioni — meza iliyopambwa kwa taa za mshumaa, mkate wa tambi, mchuzi wa mboga uliopikwa kwa ustadi, na chai ya mdalasini.

Jack alikula kimya kama kawaida, lakini alihisi joto la mazingira mapya. Kwa mara ya kwanza, hakulazimishwa kula. Hakukemewa kwa kuchelewa. Alijisikia kama... binadamu.

Baada ya chakula, Padre Ian alimshika mkono kwa upole na kumwongoza kuelekea ukumbi mdogo wa ibada. Pale, kwenye taa hafifu na sauti ya kwaya ya masista waliokuwa wakifanya ibada ya jioni, Jack alikaa nyuma kabisa. Alisikiliza. Hakuelewa maneno yote, lakini alihisi kitu cha kina ndani ya mwili wake kikiyumba — kama mto wa faraja unaojitokeza kutoka kwenye kifua chake cha ukimya.

Masista waliimba kwa sauti nyororo:

“Ee Mungu tuonyeshe njia, kwa wale waliopotea...”

Jack alifumba macho, na kwa mara ya kwanza tangu Lushoto, alihisi roho yake ikijibu wito wa sauti nyingine.

Ibada ilipomalizika, walipelekwa katika vyumba vya wageni. Kila chumba kilikuwa na godoro safi, sabuni ya harufu nzuri ya ndimu, na dirisha lililoangalia kwenye bustani ya maua ya kijani.

Na ndipo Jack alilala — kwenye kitanda halisi, si sakafuni kama alivyowahi zoea.

Dirisha lilikuwa wazi, na upepo wa bahari ulipuliza pazia lake taratibu, kana kwamba linaimba wimbo wa siri wa usiku.
Alijifunika shuka nusu, mwili wake ukiwa umechoka kwa safari ndefu, lakini moyo wake ukiwa umechoka zaidi kwa safari ya ndani — ya sauti, ndoto, na vitu visivyo na jina.

Na kabla ya alfajiri kugonga, mlango wa ndoto ulimuita kwa mara nyingine.

.

Na kabla hata hajazama usingizini, mwanga wa ajabu ulimvuta — kama handaki la dhahabu lililofunguliwa ndani ya nafsi yake.

Alijikuta tena kwenye ile bustani ya kale, lakini leo ilikuwa tofauti.
Hewa ilikuwa nzito kama mvuke wa tambiko.
Anga lilikuwa la dhahabu iliyoyeyuka.
Na hewa ilikuwa imejaa sauti zisizoimbwa — sauti zilizowekwa kimya kwa makusudi.

Kati ya safu ya sanamu zilizonyamaza, Sharp Spear (Mkuki Mkali) alisimama mbele yake. Lakini leo, hakusema kwa sauti ya amri. Alizungumza kwa sauti ya mtu anayeheshimu hatima ya mwingine:

“Ulikaribia jana. Lakini leo... utaanza.”

Mkono wa Sharp Spear ulionyooshwa haukuwa wa ushujaa tena, bali wa mlezi.
Katikati ya viganja vyake, Kitabu cha Majira kilionekana tena — kikielea kama kimefungwa na pumzi ya waliokufa.
Kifuniko chake kilikuwa kimeandikwa kwa mwanga, si wino. Na pembeni, vidole vya Jack vilianza kutetemeka… si kwa hofu, bali kwa heshima.

Alipoikumbatia mikono yake juu ya kurasa za kitabu hicho, mlio wa kina ulisikika — si wa kupasua hewa, bali wa kupasua wakati.
Na ukurasa wa kwanza ukajifungua… polepole… kana kwamba uliogopa kuonekana na yeyote asiyestahili.

Wakati huo huo, sanamu zote 1,999 zilinyamaza kabisa. Viongozi wa kale, wahenga waliovikwa silaha, walimu wa siri, na watoto wa zamani — wote walimuangalia Jack kwa jicho la maamuzi.

Kisha ikaja sauti moja — si sauti ya mwanamume, wala mwanamke, wala roho tu.
Ilikuwa sauti ya vizazi vilivyokufa na bado vinaishi.
Sauti ya ulimwengu ulioandika kila tendo, kila maumivu, kila tendo la upendo katika nyuzi za wakati.

“Sasa umefungua ukurasa. Lakini kila neno… lina gharama yake.”

Jack alifikiria kuuliza maana ya maneno hayo, lakini hakuweza.
Kwa sababu moyoni mwake, tayari aliielewa.
Kila kumbukumbu atakayogusa, italeta baraka au mzigo.
Kila roho atakayoamsha, itakuwa rafiki… au adui.

Ndipo akaamka.

Lakini hakuwa JackXavier wa jana.
Sauti ya ulimwengu ilikuwa imemgusa.
Moyo wake haukupiga kwa hofu tena, bali kwa utulivu wa mtu ambaye ameona zaidi ya macho ya kawaida.

Aliinuka kitandani kwa taratibu, akatizama dirisha lililokuwa wazi.
Na akajua bila shaka yoyote…

"Leo nimekanyaga mpaka wa dunia mbili. Na hakuna kurudi nyuma."

Previoua Next