Asubuhi ya siku iliyofuata, anga lilikuwa la bluu tupu. Hakukuwa na dalili ya mvua. Hakukuwa na upepo. Na ndani ya Kampasi Kuu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mlima wa miamba uliogeuzwa taaluma, Prof Zara Mwinyi alitembea kwenye njia za mawe zenye kivuli cha miti ya miarobaini, akielekea darasani kana kwamba dunia yake haikubadilika jana.
Wanafunzi wachache walikuwa wamekaa kwenye Vimbweta, wengine wakiwa wanaandika vitu kwenye daftari au kuangalia simu zao. Lakini kila mmoja, alipomuona Profesa Zara, alinyamaza.
“Unadhani ataendelea kufundisha kama kawaida?” mwanafunzi mmoja wa mwaka wa pili aliuliza kwa sauti ya chini.
“Sijui. Lakini jana usiku niliangalia Al Jazeera. Walirudia jina la Imran mara kumi kumi. Na wakaonyesha mpaka picha ya harusi yao...”
“Na bado yeye yuko kazini leo. That’s crazy,” mwingine alijibu.
Zara hakuwaangalia. Alitembea kwa mwendo ule ule wa kawaida, mkoba wa ngozi bega moja, daftari moja mkononi, na macho yasiyoonyesha mahangaiko yoyote.
Alipofika darasani, wanafunzi walisimama kimya. Walidhani huenda angesema chochote, hata sentensi ya faraja au kukubali pole. Lakini badala yake, alifungua kitabu chake, akaandika kitu kwenye ubao kwa herufi kubwa:
"LINGUISTICS AND MEMORY: HOW LANGUAGE STORES WHAT WE'D RATHER FORGET."
Ikimaanisha : ISIMU NA KUMBUKUMBU: JINSI LUGHA INAVYOHIFADHI KILE TUNGEPENDA KUSAHAU
Kisha akageuka na kusema kwa sauti tulivu:
“Wanafunzi, leo tutaongelea dhana ya ‘Memory and Language Retention’ - kwa nini baadhi ya matukio hujificha ndani ya lugha zetu, na mengine hujifuta kabisa.”
Hakukuwa na hata rejea moja kuhusu mumewe aliyepotea. Hakukuwa na machozi. Hakukuwa na uzembe. Kulikuwa tu na Zara — mwalimu, mtaalamu, na sasa fumbo lililo hai.
********
Ndani ya ofisi ya Mkuu wa Idara
Profesa Mwinjuma alisimama mbele ya dirisha la vioo refu, kahawa ikiwa bado haijaguswa ndani ya kikombe chake (ceramic mug) kilichoandikwa UDSM Linguistics Conference 2014. Alitazama kwa mbali, macho yake yakiwa kwenye mti wa mporojo unaotikiswa na upepo wa asubuhi.
“Huyu mwanamke...” alitamka kwa sauti ya chini, kana kwamba alikuwa akiongea na kivuli chake. “Ananishangaza. Ama ana roho ya chuma, au kuna kitu hatukielewi.”
Msaidizi wake, Bi Halima, alinyanyua macho kutoka kwenye jalada la faili alilokuwa analipanga.
“Wengine tungekuwa tumelazwa kwa pressure sasa hivi,” alisema kwa sauti ya kutoamini. “Lakini yeye? Yeye ni kama... hana moyo vile”
Profesa Mwinjuma aligeuka taratibu, akaweka kikombe mezani bila kukinywa hata tone. Alikaa kitini, akavuta pumzi ndefu.
“Wanafunzi wake wanamuogopa kuliko kawaida. Naamini mmoja aliniambia alijua ni siku mbaya kwa sababu Zara hakuvaa saa yake ya mkononi. Saa ya mkononi, Halima. Imagine.”
Bi Halima alishika faili kwa nguvu bila kukusudia.
Kimya kilikaa ofisini kwa sekunde kadhaa, kabla ya Profesa Mwinjuma kunong’ona kwa sauti ya chini kabisa, karibu na kuogofya:
“Sio kwamba hana moyo, Halima. Ni kwamba amejifunza kuzika vitu... kuna ambavyo amevizika chini sana, mpaka hata yeye mwenyewe hawezi kuvisikia tena.”
Nyumbani: Usiku
Zara alirejea nyumbani saa moja usiku. Alipofungua mlango, harufu ya chai ya mchaichai aliyoiwacha asubuhi bado ilikuwa hewani. Hakwenda kuoga, hakula chakula, wala hakuwasha redio wala TV. Badala yake, alienda moja kwa moja hadi kwenye chumba cha ofisi yake.
Aliketi kwenye meza yake. Akafungua journal.
Akaandika:
“Today, I returned to campus. They looked at me like a ghost, like a shadow in glasses. I taught about memory, but who truly knows that I’m the one carrying all of theirs? Not Imran, not the students. Me. Me alone."
“Leo nimerudi chuoni. Walinitazama kama mzimu, kama kivuli kilichovaa miwani. Nilifundisha kuhusu kumbukumbu, lakini ni nani anayejua kuwa mimi ndiye nimeibeba kumbukumbu yao? Si Imran, si wanafunzi. Mimi. Mimi peke yangu.”
Alitulia kwa dakika chache. Kisha akaandika mstari mwingine:
"They say silence is the second form of grief. They forget - silence is the first form of decision."
“Wanasema ukimya ni aina ya pili ya huzuni. Wanasahau - ukimya ni aina ya kwanza ya uamuzi.”
Aliifunga journal. Akanyanyuka taratibu. Akafungua kabati dogo la vitabu — na kutoka kwenye kona ya nyuma, akatoa flash drive ndogo ya kijani.
Aliitazama kwa sekunde kadhaa. Kisha akaisema taratibu:
“It’s almost time.”
Comments