FOR YOU 2
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Uhalifu, Mauaji, Visasi, Vita, Mambo yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA NANE
★★★★★★★★★★★★
Siku zilizofuata, Lexi angekaa pamoja na Lakeisha hapo kwenye nyumba na kumzoeza vitu vingi na kumfundisha mambo mengi, kutia ndani Kiswahili. Mwanamke huyu alikuwa mwepesi kujifunza mambo na hatua kwa hatua Lexi akaona jinsi alivyokuwa na bidii, na mcheshi pia.
LaKeisha alisimulia maisha yake na kusema yeye ndiye aliyekuwa mtoto pekee wa kike na wa mwisho kwenye familia yao yenye watoto sita. Walikuwa na maisha magumu, na kaka zake wote walijiingiza kwenye mambo haramu ili kuitegemeza familia yao tokea walipokuwa wadogo. Lakini baadaye wote waliuawa kwa kuchomwa visu na watu waliokuwa wanawadai, hivyo hiyo ikamwacha yeye na mama yake tu, kwa kuwa na baba yake alikuwa amekufa mapema. LaKeisha alianza kufanya kazi za kucheza ngoma kwenye kundi fulani, baadaye kama mhudumu wa mgahawa mdogo, mtumbuizaji wa dansi kwenye kumbi za starehe, na hizo zote zilimweka katika hali mbaya kihisia lakini hakuwa na jinsi. Alipenda masomo, lakini kwa sababu ya kutopata pesa ya kutosha hakuweza kuendelea.
Baadaye ndiyo alianza kuwafanyia kazi watu wakubwa ambao walitumiana bidhaa za madawa ya kulevya, yeye akiwa mhamishaji kama vijana wengine. Kipindi fulani mama yake aliumwa sana ugonjwa wa pumu na alihitaji matibabu yenye gharama, hivyo LaKeisha akamwomba boss wake kiasi kikubwa cha pesa kama mkopo ili amlipie mama yake matibabu. Boss wake alimpa, lakini pia akampa tarehe hususa ya kuzirudisha, naye LaKeisha akaenda na kumlipia mama yake matibabu.
Akaanza kufanya kazi za pembeni tofauti na hiyo ili akusanye pesa kwa ajili ya kumlipa boss wake, lakini kwa tukio baya mama yake akawa amepoteza maisha. Hiyo ikamwacha akiwa peke yake tu. Muda ulifika wa kurudisha deni lakini hakuwa amekusanya pesa ya kutosha, na boss wake alimwambia kama asingerudisha basi angemuua. Kwa hiyo akajiingiza kwa boss mwingine wa masuala hayo hayo na kutafuta njia ya kuzirudisha pesa za yule wa mwanzoni, ndiyo mpaka kufikia kisa kile kilichomkuta kabla ya Lexi kumwokoa.
Hadithi ya maisha yake ilihuzunisha, lakini bado alikuwa mtu asiyekata tamaa na kuendelea kubaki imara. Wengine pia walimzoea haraka kwa sababu ya utundu wake na madoido aliyokuja nayo hapo, hadi mwisho wa siku Kendrick akaanza kumfurahia kwa sababu alionyesha kuwa mwaminifu kwake.
Ilipofika siku ambayo vijana wa Kendrick walitakiwa kwenda kuiba dhahabu kwa mara ya mwisho, LaKeisha aliomba kwenda pamoja nao. Wote walikataa, lakini akasisitiza kwa kusema alihitaji kuwasaidia ili na yeye apate chochote cha kuweza kuwalipa wanaume wale ambao mpaka kufikia muda huo wangekuwa wanamtafuta. Wengine wakamuuliza Lexi anaonaje kuhusu hilo, na baada ya kutafakari, Lexi akakubali na kumpanga sehemu mpya muhimu kwenye kazi hiyo. Walikuja kuondoka na dhahabu kilo 300 siku hiyo ilipofika, na msaada wa LaKeisha ulikuwa mzuri sana. Kendrick alianza kumfurahia hata zaidi, naye akasema sasa angekuwa mmoja wa kundi lao rasmi.
Baada ya hapo, Lexi pamoja na Mensah walikuja kumsindikiza LaKeisha alipokwenda kuwalipa wanaume wale pesa zao. Tena kwa kiburi kakawarushia usoni kwa sababu kaliwalipa mara mbili zaidi ya kile walichokadai. Alikuwa mwenye kujiamini sana wakati huu kwa sababu ya kuwa miongoni mwa kundi lenye ubora zaidi, na lililomtendea kama familia.
★★★
Baada ya mambo yote hayo, sasa ulikuwa umefika wakati wa Kendrick na Lexi kuanza kupiga hatua za mipango yao kuelekea nchi waliyotoka. Kwa muda mrefu walikuwa wameshafatilia mambo mengi sana yaliyoendelea huko, kwa hiyo wakati huu wangeanza kujipanga ili kutimiza lengo lao. Victor, Mensah, na Oscar wangekwenda Tanzania kwanza. Mpango ulikuwa ni kwenda kujenga nyumba kubwa huko, ambayo ndiyo ingekuwa sehemu ya kufikia wengine. Walikwenda na pesa kama zote, kwa hiyo wangeajiri wajenzi wenye uzoefu ili kuanza kazi ya ujenzi wa nyumba hiyo kwa mpangilio aliowapatia Torres.
Sehemu waliyopaswa kujengea nyumba hiyo ilikuwa ni ile ambayo Kendrick na Casmir walitengeneza handaki chini ya ardhi. Kendrick alikuwa ameshakinunua kiwanja chote kuzunguka eneo hilo miaka miwili iliyopita kutokea huku huku Ghana, na hakuna yeyote nchini kule aliyejua ni yeye kwa sababu alitumia utambulisho tofauti aliokuwa akiutumia wakati huu.
Kwa hiyo wakina Victor walitakiwa kusimamia ujenzi huo, lakini uliotakiwa kufanywa kwa umakini sana. Zilitakiwa kujengwa kwanza kuta za kuzunguka eneo hilo, halafu ndiyo ujenzi wa ndani ungeanza. Victor na wenzake wangetakiwa kuwa macho ili wajenzi wasitambue sehemu ile ya mwingilio wa kule chini. Yaani, wangepaswa kujenga tu nyumba na kuipangilia, lakini kufikia sehemu hiyo hawakupaswa kupagusa.
Lakini, mmoja kati ya wajenzi ambaye alikuwa makini sana aliitambua sehemu hiyo. Huyu alikuwa ni Kevin Dass. Kwa utambuzi wa haraka, alihisi ni kama watu hawa walikuwa wakifanya hivyo makusudi, naye akaona afatilie kimya kimya ili kujua nia yao ilikuwa ni nini. Alikuja kugundua kwamba wakati ambao mafundi wangeondoka, Victor, Mensah, na Oscar wangeingia kule chini ili kupatengeneza pawe pa kisasa zaidi. Alikuja kuwafuata siku moja chini huko, nao wakamkamata na kumfunga.
Kevin aliwaeleza alichofikiria, akisema inaonekana walikuwa wakificha jambo fulani muhimu, na yeye hangewasema kwa yeyote, lakini angewasaidia ili wasitambulike. Akawaambia kuendelea kuwaficha mafundi na wasimamizi wengine kuhusu jambo hili isingekuwa kazi rahisi, kama ilivyokuwa kwake tu mpaka akajua, lakini kama wangemwingiza kwenye mipango yao basi angewasaidia kuficha siri yao na hata kuwasaidia kupajenga chini huko vizuri zaidi. Alipenda pesa, na ikawa wazi kwa wengine kwamba hilo ndiyo lilikuwa lengo lake; afanye nao kazi hii ya siri ili apate pesa zaidi.
Ikabidi Victor aongee na Kendrick, ambaye bado alikuwa nje ya nchi. Alimwambia kuhusu hali halisi, naye akauliza wafanye nini. Baada ya kutafakari mambo kwa kina, Kendrick akaomba kuongea na Kevin. Alimwambia kuhusu kile kilichokuwa kikiendelea na kumuuliza kama angeweza kuwa pamoja nao mpaka mwisho, na kijana huyo akakubali. Kwa hiyo Kendrick akawaamuru wengine wafanye kazi pamoja naye, ingawa uamuzi huu haukumfurahisha kabisa Mensah. Hata akaongea na Kendrick kumwambia huu haukuwa uamuzi mzuri, lakini Kendrick akamwambia asiwaze sana, na awe anamchunga mtu huyo ili kuona kama ataleta nuksi. Kama angeleta nuksi, basi Mensah angekuwa na kibali cha kumshughulikia.
Vijana hawa ambao walikuwa Tanzania waliongozwa na Victor, naye alikuwa akimwelekeza Kevin kuhusu mipango yao. Mara kwa mara wote wangemjaribu Kevin ili kuona ikiwa alikuwa mwaminifu na msiri au ni kigeugeu, lakini akawathibitishia kuwa alikuwa mwaminifu. Lexi, Torres, na Lakeisha walikuja kuambiwa kwamba kuna mtu mwingine ameongezwa kwenye kundi lao, ambaye angesaidia ujenzi wa nyumba yao kule Tanzania, nao wakaridhia pia.
★★★
Ni Lexi, Torres na Lakeisha ndiyo pekee waliobaki na Kendrick huko Ghana. Lakini kwa muda ambao wenzao walikuwa wamekwenda Tanzania, wenyewe walikuwa wakifanya kazi ya kununua au kutengeneza vitu vingi kwa ajili ya kutumia wakati ambao wangefika nchini kule. Walikwenda sehemu kama Jamaica alikokuwa akiishi Torres, Manhattan kule Marekani, Prague huko Ufaransa, na Johannesburg Afrika Kusini. LaKeisha alifurahia zaidi safari hizi kwa sababu hakuwahi kutoka nje ya nchi aliyokulia toka azaliwe, na kuzifanya ziwe kama nafasi ya kutalii, na hata kutoka na wazungu kwenye "date."
Walipokuja kurudi Ghana, walianza kupangilia mambo na vitu kwa ajili ya kutuma kule Tanzania. Torres alitangulia huko na yeye miezi michache baadaye akijiweka kama mfanyabiashara wa kawaida tu, huku vitu vingi ambavyo angeviingiza vingepitia bandarini. Walikuwa na njia nyingi sana za kuingiza mambo yao bila kutambulika, na wakati huo mambo ya ujenzi kwenye sehemu ile yalikuwa yakielekea kukamilika. Alipata nafasi ya kukutana ana kwa ana na Kevin Dass, nao wakaanza kutumia wakati pamoja ili kumzoeza vizuri hata zaidi njia zao za kufanya mambo.
Hiyo ikawaacha Kendrick, Lexi na Lakeisha huko Ghana. Kufikia kipindi hiki, Kendrick na Margaret bado waliendelea kuonana lakini hakukuwa na "mahaba" yaliyofanyika baina yao. Margaret alikuwa amejifungua mtoto wa kiume pamoja na mume wake miaka miwili nyuma, hivyo hawakutumia muda mwingi pamoja ingawa bado walijiona kuwa wapenzi.
Ingawa Kendrick alihisi ni kama walikuwa wanalazimisha mambo, kuendelea kwake kuwa mtu wa pembeni wa Margaret ilitokana hasa na shukrani yake kubwa kumwelekea mwanamke huyo kwa sababu ya kuokoa maisha yake mpaka hapo alipofikia. Margaret mpaka kufikia muda huo hakujua lolote kuhusu mishe za kisiri alizofanya Kendrick na vijana wake, naye Kendrick aliona mambo yalitakiwa kubaki namna hiyo.
★★★
Wakati fulani, Lexi pamoja na Lakeisha walikuwa wakifanya matembezi kwenye mitaa ya Kumasi mjini, naye LaKeisha akamwambia Lexi kwamba mapolisi waliwakamata wale wote waliofanya kazi na boss wake siku iliyopita kwa kuuza madawa. Akasema alikuwa anafurahi sana kwamba hakuwa huko tena, kwa sababu aliwahi kuwekwa jela na hakutaka kurudi huko, hivyo kama angekuwa nao kufikia kipindi hiki basi na yeye angepelekwa nao. Akiwa na furaha nyingi, akaona sehemu fulani waliyokuwa wakitengeneza nyama za kuchomwa na vyakula mbalimbali, naye akamwambia Lexi angekwenda kufata nyama ili warudi nazo nyumbani kukamua.
Lexi akamwambia aende tu naye angemsubiri, naye LaKeisha akaondoka kuelekea huko. Akiwa amesimama pembezoni mwa barabara, aliona watoto fulani ambao walikuwa wamezunguka mtaro pembeni ya barabara hiyo upande wake wa kushoto, wakiwa wanaponda kitu fulani kwa mawe madogo madogo ndani ya mtaro huo. Kwa kukisia, akadhani walichokuwa wakiponda ni nyoka labda, naye akaona asogee hapo ili aangalie alikuwa ni nyoka wa aina gani, huku akimsubiria LaKeisha.
Alipofika hapo, akakuta haikuwa ni nyoka waliyekuwa wakimponda, bali mnyama mdogo mwenye kufanana na paka. Alikuwa kama mtoto wa paka, naye alikuwa akijaribu kukimbia lakini mawe aliyopondwa yalimfanya asiweze kufanya hivyo kutokana na kuumia mguu mmoja zaidi. Lexi angeweza kuona majeraha yake yenye kutoka damu, naye akamwonea huruma sana. Akawaambia watoto hao waache kumponda, kisha akawafukuza hapo ingawa walikuwa wabishi.
Lexi akaingia mtaroni hapo na kuchuchumaa na kumwangalia, na mnyama huyu mdogo bado alikuwa akijaribu kujivuta lakini kwa maumivu. Ngozi yake ilikuwa ya rangi inayokaribiana kabisa na nyeupe, kama kijivu, na ilikuwa na madoadoa madogo madogo kuzungukia mwili wake wote. Kulikuwa na mistari ya mbali kutokea chini ya macho yake mpaka sehemu ya midomo, naye Lexi akatambua huyu hakuwa paka.
LaKeisha akafika hapo pia akiwa na mishkaki minene ya nyama ya mbuzi ndani ya mfuko, naye akauliza kwa nini Lexi alikuwa ameingia kwenye mtaro mchafu. Lexi akamwonyesha kitoto hicho, naye LaKeisha akamwambia aachane nacho tu ili waondoke wakapate chakula kule kwao. Lexi alikitazama tena, na kwa sababu asiyoijua akaanza kumfikiria Sandra. Alikumbukia jinsi mara ya mwisho kumwona alivyokuwa akiomba Weisiko asimuumize, naye kwa kumwangalia mnyama huyu, akadondosha chozi.
LaKeisha mpaka akamshangaa na kumuuliza alikuwa na tatizo gani, lakini Lexi hakujibu lolote na kumbeba tu mnyama huyo, kisha akamwambia Lakeisha waondoke. LaKeisha akashangaa sana kiasi kwamba hadi akaanza kumcheka. Akamwambia wakati mwingine alikuwa anamchanganya sana ila ndiyo hivyo, alikuwa ameshamzoea.
Baada ya kumpeleka kule walikoishi, Lexi alianza kumpa huduma muhimu mnyama huyo mdogo. Alimtunza vizuri na kumpa mahitaji yake kama tu alivyofanya kwa mifugo yake ya sungura. Siku zilipozidi kusonga, afya yake ikawa nzuri zaidi. LaKeisha alikuwa anapendezwa sana na jinsi Lexi alivyowajibikia hata vitu ambavyo yeye hakuona ni muhimu kivile. Lakini pia, alianza kuona utofauti kwenye utu wake na yule aliyeonekana kwa nje. Lexi alikuwa mwanamke kwa nje ndiyo, lakini kila kitu alichofanya kilikuwa kwa mtindo wa mwanaume, na hili liliitia udadisi akili ya LaKeisha kumwelekea.
Usiku mmoja wakiwa chumbani kwa Lexi huku akicheza na mnyama wake mpya, LaKeisha alikuwa anamwangalia tu Lexi kwa umakini. Alikuwa aina ya mwanamke ambaye akitaka kujua kitu fulani, angekijua tu haijalishi nini kingehitajika. Lexi akatambua alikuwa anatazamwa sana, naye akamuuliza ana shida gani.
"Nothing," LaKeisha akasema.
"Kwa Kiswahili," Lexi akamwambia.
"Ahahah... aam... hamuna kitu," LaKeisha akasema kiutani.
"Acha masihara, najua unaweza kuongea Kiswahili vizuri sa'hivi, ila unajifanya tu," Lexi akamwambia.
"Siyo vizuri sana lakini. Ila ninajitahidi kwa sababu nina mwalimu mzuri," LaKeisha akasema.
Lexi akawa akirusha mpira mdogo upande mwingine wa chumba, na mnyama wake akawa anaukimbilia na kumletea kwa mdomo.
"Ahahahah... good girl!" Lexi akamsifia huku akichezea manyoya yake laini.
"You know, you haven't named her yet (unajua, bado haujampa jina huyu)," LaKeisha akamwambia.
"Yeah. I'm struggling to find her a good name. Something rare (ndiyo.. ninasumbuka sana kutafuta jina zuri.. jina adimu)," Lexi akasema.
"Don't... usimpe jina gumu itakuwa hard for her to get used to. And... mpe mapema ili alizoee haraka," LaKeisha akamshauri.
"Unanipa ushauri now wakati wewe ndiyo uliniambia nimwache mtaroni!" Lexi akamwambia.
LaKeisha akacheka kidogo na kuendelea kumwangalia kwa hisia. Lexi sasa akawa kama amechoshwa na jinsi LaKeisha alivyokuwa anamtazama.
"What's wrong with you? (una matatizo gani?)" Lexi akamuuliza huku anatabasamu.
LaKeisha akatabasamu, kisha akasema, "Nothing's wrong with me. I'm just weird... you know that (hakuna tatizo kwangu.. nakuwaga wa ajabu tu.. unajua hilo)."
"Yeah, no shit," Lexi akasema.
LaKeisha akatabasamu tena.
"If you want to say something, just tell me. We tell each other everything right? (kama kuna kitu unataka kusema, niambie tu.. huwa tunaambiana kila kitu, si ndiyo?)" Lexi akamwambia.
LaKeisha akavuta pumzi ya juu, kisha akaishusha na kusema, "Ina son ku."
Lexi alimtazama kiumakini. Alielewa maneno hayo ya kikabila cha Hausa yalimaanisha "I like you," njia fulani ya kumwambia mtu unapendezwa naye lakini kwa njia ya kimapenzi.
"Are you drunk? (umelewa?)" Lexi akamuuliza.
"No, I'm just serious... (hapana.. niko makini/mkweli tu)" LaKeisha akasema.
Lexi akamtazama mnyama wake tu.
"You... you're different. Its like... I don't know. Like there's something you're hiding about yourself that just... makes me like you. You never even have sex. Who does that? (wewe.. uko tofauti.. ni kama.. sijui tu.. ni kama kuna kitu kuhusu wewe unakificha ambacho.. kinafanya navutiwa nawe.. huwa hata haufanyi mapenzi.. nani huwa yuko hivyo?)" LaKeisha akasema.
Lexi akacheka kidogo. Akamtazama machoni tena na kuona kweli LaKeisha alikuwa anamaanisha alichosema, hivyo akamwambia asubiri akamwekee kwanza mnyama wake chakula ili waje kuzungumza.
Alirudi na kuanza kumweleza ukweli wote wa maisha yake. Kwa vijana wote wa kundi hili la Kendrick, walijua sababu ya wawili hawa ya kutaka kulipiza kisasi kule Tanzania ilikuwa ni ishu ile ya Demba Group miaka kadhaa nyuma iliyowaharibia maisha yao. Lakini kuhusu Xander kubadilishana miili na pacha wake, hawakujua. Sasa LaKeisha ndiyo akawa mtu mwingine tofauti na Kendrick aliyejua kuhusu hili. Ilikuwa ngumu kwake kuamini mwanzoni, lakini hakukuwa na sababu ya kukataa jambo hilo. Lexi alimwelezea vitu kwa hisia mpaka machozi yakawa yakimlenga.
LaKeisha, akiwa amepatwa na ukaribu wa kihisia zaidi kwa Lexi, akamkaribia na kumshika usoni, kisha akambusu mdomoni kwa upendo. Lexi hakuwa na itikio lolote lile zaidi ya kumwacha tu, naye LaKeisha akaendelea kulazimisha busu hiyo mpaka ikaanza kuwa denda kati yao. Pole kwa pole LaKeisha alianza kujiweka karibu zaidi ya Lexi, na wawili hawa wakaanza kupeana mahaba.
Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Lexi kufanya mapenzi na mtu tokea alipoingia kwenye mwili huu wa pacha wake. Lakini Lexi hakutaka bado kufanya mapenzi kwa njia ya wawili, yaani, yeye alimwonyesha tu LaKeisha mahaba kama jinsi ambavyo angemfanyia mwanamke wakati alipokuwa ndani ya mwili wake wa kiume, lakini hakuruhusu LaKeisha amfanyie hivyo kwa sababu kihalisi hakutaka kujua mwanamke huhisije. Kwa hiyo ilikuwa kama kumridhisha tu LaKeisha, na ilikuwa ajabu kwake kidogo kuona kwamba aliweza kumfikisha LaKeisha mahala pazuri ingawa hakukuwa na mashine iliyotumika!
Basi, baada ya mahaba yao ya KUS na KUS kama sumaku, Lakeisha alimwambia Lexi jinsi alivyofurahia burudisho hili jipya kwake. Lakini Lexi akamweka wazi kwamba hakuwa na muda wa kuwa na mahusiano, kwa sababu hali yake ya kimwili bado ilikuwa tata. LaKeisha akaonyesha kumwelewa kwa kusema jambo hilo halikuwa na tatizo, ila kama angehitaji show nyingine basi asimnyime. Kwa hiyo wangeendelea kuwa aina ya marafiki wa faida.
LaKeisha akaanza kumchora Lexi tattoo nyingi mwilini mwake kuanzia hapo na kuendelea, akiupamba mwili wa "kipenzi" chake kipya kwa umaridadi wa hali ya juu.
★★★
Mwaka mmoja baada ya hayo, Kendrick alikutana na Margaret na kumwambia kwamba ulikuwa umefika wakati sasa wa yeye kurudi nchini kwao. Margaret aliuliza ikiwa hilo lingekuwa jambo la busara, naye Kendrick akatania kwa kusema kwa kuwa sasa alikuwa na miaka 56, hakuna mtu yeyote angeweza kumtambua huko kutokana na kuzeeka. Margaret alimkumbatia kwa hisia sana siku hiyo, naye akamwambia ijapokuwa safari yao ilikuwa na vikomo, bado Kendrick angeendelea kuwa moyoni mwake.
Baada ya Lexi pia kuonana na Margaret na kusema kwa heri zao, sasa Kendrick, LaKeisha na Lexi wakaelekea Tanzania hatimaye. Walikuta nyumba yao ile iliyojengwa kwa umaridadi wa hali ya juu ikiwa imekamilika, nao walipokelewa vyema na wenzao huko ambao walikuwa wamekwishaizoea nchi hiyo. Handaki lile chini ya ardhi lilikuwa sehemu za katikati ndani ya nyumba hii, na vijana wale walikuwa wameipanua na kuifanya iwe kubwa na yenye ubora huko huko chini, hasa kwa msaada wa Torres. Walikuwa wametia jitihada kubwa sana kuunda kila kitu kiwe jinsi walivyotazamia, na sasa kazi iliyokuwa mbele yao wangeanza kuipangilia vizuri hata zaidi baada ya boss wao na Lexi kufika.
Yote hayo ndiyo yaliyokuwa yamepelekea wizi wa kiasi cha shilingi trillioni 20 kutoka majengo ya benki kuu, na bado kundi hili lingeendelea kuisumbua kiaina serikali hii iliyokuwa chini ya utawala mbovu wa Raisi Paul Mdeme.......
★★★★
WAKATI ULIOPO
Ikiwa ni siku iliyofuata baada ya Kendrick Jabari kuongea na Lexi kwenye simu usiku, Raisi Paul Mdeme alikuwa akisubiri kwa hamu mzigo wake wa dhahabu ufike. Alikuwa ametumia njia fulani ya siri kuuingiza nchini, akiwa amefanya makubaliano na watu fulani kutokea nchini Afrika Kusini ili wafanye kama "kumkopesha" madini hayo, naye angewapatia vitu fulani vya thamani kutoka nchini kwa njia haramu. Yangepitishwa DRC Congo, kisha kwa njia ya kificho yangeingizwa nchini.
Njia yenyewe ya kificho ilikuwa ni treni. Yaani tena treni zile zinazobeba kokoto nyingi tu kwenye mabehewa yaliyowazi, kutokea Kigoma mpaka Dar es Salaam. Dhahabu hizo zilifichwa chini ya behewa moja la katikati ambalo lilijazwa kokoto mpaka juu kama mabehewa mengine tu, hivyo haingekuwa rahisi kwa yeyote kutambua kuna vito vya thamani hapo. Pia, treni hii ililindwa na watu wachache wa Raisi waliojua kuhusu ishu hii, nao wangekaa mbele kule kama waongozaji wa kawaida tu mpaka wakati ambao treni ingefika ilipotakiwa na kushusha mzigo huo.
Kwa upande wa timu ya Luteni Michael, walijigawanya mara mbili siku hii ili kwenda kwenye kampuni zile binafsi zilizohusiana na masuala ya madini kutoka makampuni ya nje ya nchi. Ikiwa unakumbuka vyema, hii ilikuwa ni sehemu ya utafiti mpya uliopendekezwa na ACP Nora baada ya kufanya uchunguzi kuhusiana na nguo zile walizovaa Mess Makers ambazo zilikuwa na uwezo wa kuzuia risasi. Walitaka kwenda kuona kama kampuni hizi zingekuwa na uhusiano fulani wa kisiri pamoja na watu hawa ili waweze kuwakamata haraka.
Luteni Michael alikwenda kwenye kampuni iliyokuwa mkoani Geita, akiwa pamoja na Mario, Hussein, na Omari, naye ACP Nora akaenda kwenye ile iliyokuwa upande mwingine wa jiji la Dar es Salaam akisindikizwa na Vedastus, Mishashi, pamoja na Alex. Walimwacha Bobby kwenye jengo lao lile la uchunguzi, nao wangekuwa wakiwasiliana pamoja naye.
Upande wa treni yenye dhahabu za Raisi Paul Mdeme, ilikuwa ikitembea kwa kasi sana. Yaani siku hii hakuna treni nyingine yoyote ya abiria na mizigo iliyotakiwa kufanya safari, ni hii tu ndiyo iliyopaswa kutembea. Wasafiri kutokea Kigoma waliotaka kuchukua treni kwa reli hii ya kati kwa leo wangepaswa kusubiri mpaka kesho, au wachukue usafiri mbadala lakini siyo treni. Wengi hawakuelewa sababu, na kuchukulia ni jambo la kawaida tu; huenda kulikuwa na rekebisho likifanywa, waliwaza.
Kufikia mida ya jioni, tayari ilikuwa imeshavuka mikoa kadhaa na sasa ikawa maeneo fulani ya Morogoro yenye milima iliyo pembezoni mwa reli hiyo. Raisi Paul Mdeme aliwasiliana na watu wake walioiongoza ambao walimjulisha kwamba mzigo haukuwa mbali kufika, naye Raisi akaridhika sana.
Lakini, kutoka juu ya mlima fulani usio mrefu sana (lakini ni mrefu), kulikuwa na watu wachache wakiwa wamesimama hapo. Hawakuwa wengine ila Mess Makers. Hatari! Wahuni tayari walikuwa wameshanusa dhahabu zilipo, nao wakawa hapo wakiisubiri treni ipite usawa huo ili waanze kujichukulia madini yao. Acha kabisa! Mdeme alikuwa anawashusha thamani sana hawa jamaa, ila sasa ndiyo wangemwonyesha jina lao linamaanisha nini.
Walikuwepo watano hapo kutoka kwenye kundi lao; Lexi, Victor, Mensah, LaKeisha na Oscar. Walikuwa wamesimama huku wanaiangalia kwa umakini treni ikitembea, naye Oscar alikuwa tu ameachia tabasamu lake la masihara. Ilipoanza kukaribia usawa wao, wote wakachuchumaa, kisha wakazivaa "mask" zao usoni. Lexi akanyanyua kiganja chake juu na kuweka vidole vitatu hewani. Treni ilipoanza kuwapita, akaanza kushusha kidole kimoja-kimoja kwa kuhesabu 3, 2, 1, kisha akakunja ngumi, nao wote wakaruka kuelekea chini. Nyuma ya nguo zao maalumu kwa ajili ya mapambano walizovaa, walijifunga kamba ndefu na ngumu sana zilizoshikizwa vyema juu ya mlima huo, nao wakawa wanateremka kwa kudunda na kudunda kuelekea chini.
Kamba hizo zenye ubora ndiyo vitu waliyokuwa wamevifata kule Mwanza mpaka Kevin akakamatwa ile juzi. Walizichukulia sehemu tofauti-tofauti kwa ajili ya mishe hii, na hapa alitakiwa kuwepo Kevin pia lakini kwa sababu sasa alijulikana ilibidi wamwache kule "chini" kwenye sehemu yao ya kujificha. Hii ndiyo iliyokuwa mission ambayo Lexi na Kendrick waliizungumzia. Torres katika ufatiliaji wake wa mambo alipata kujua dili la Mdeme na watu kutoka Afrika Kusini, hivyo akafanya mipango na Lexi ili wawazingue tena kwa mara nyingine. Yaani walikuwa wanataka kuwafundisha viongozi wale waovu somo fulani muhimu kupitia haya yote waliyokuwa wanafanya, na huu ulikuwa ni mwanzo tu.
Watano hawa wakafanikiwa kufikia mabehewa na kuzifungua kamba zile, huku treni ikiendelea kusonga tu bila ya wale walioiongoza kutambua kwamba kitumbua chao kiliingia mchanga! Watano hawa wakakaribiana na kusimama juu ya behewa moja, kisha Lexi akatumia kifaa chake maalumu kumuuliza Torres dhahabu zingekuwa kwenye behewa la ngapi. Torres akamwambia lilikuwa behewa la 6 kutoka mwisho, na watano hao wakalielekea upesi. Walitaka kuwahi kwa sababu treni ilikuwa ikitembea haraka na haingechukua muda mrefu kutoka kwenye maeneo hayo yenye milima kufikia maeneo yenye watu.
Walipolifikia behewa hilo, Victor, Oscar, pamoja na Mensah wakasaidiana kuifungua sehemu ambayo ilikuwa imeliunganisha na mabehewa ya mbele. Kwa kuwa ilikuwa ngumu, LaKeisha akawapatia kifaa fulani cha kukata chuma, nacho kikasaidia kuondoa ugumu na hatimaye behewa likaachia. Oscar alikuwa kidogo aangukie kwenye reli lakini wenzake wakamwahi na kumshikilia, naye akawa anacheka huku wakiyaangalia mabehewa ya mbele yanawaacha nyuma. Mensah na Victor wakamvuta Oscar kwa nguvu na kulala juu ya kokoto za behewa hilo huku wakicheka, naye Lexi pamoja na Lakeisha wakawa wanacheka pia.
Mabehewa sita yaliyobaki sasa yakawa yakipunguza mwendo kwenye reli mpaka yakasimama hatimaye kwenye eneo lililo na uoto mwingi wa asili na miti mingi ya pori. Lexi akawaambia sasa hapo kazi ndiyo ingeanza. Wakashuka na kuanza kulifungua behewa hilo sehemu ya mbele kwa kutumia vifaa vile vya kukata chuma, na baada ya dakika nyingi likaachia. Hiyo ingefanya kokoto zote zimwagike, hivyo wakawa makini kukwepa ili zisiwaponde. Baada ya zote kumwagika, wakaanza kuzichambua sasa, nao wakaweza kuyaona mabamba madogo-madogo ya dhahabu zenyewe. Wakawa wakizitoa na kuzirusha pembeni ili kuzitenganisha na kokoto.
Oscar alikuwa anachekelea tu, huku akisifia sana jinsi kundi lao lilivyo la aina yake. Angalau walifurahishana kwa mazungumzo huku wakiendelea na kazi. Wakafanikiwa kuhamisha dhahabu nyingi mpaka giza kuanza kuingia kwa mbali.
Lexi akaangalia muda na kumuuliza Torres kupitia kifaa chake, "Yuko wapi?"
"Anakuja. Amekaribia kufika," Torres akajibu kupitia kifaa kile.
Wakaendelea tu kuzihamisha na kuzipanga, na ndipo wakasikia gari likija eneo la hapo. Lilikuwa ni lori dogo aina ya Canter, naye Oscar akaanza kushangilia kwa shauku. Wote walijua ni nani aliyekuwa amefika hapo, naye hakuwa mwingine ila Kendrick Jabari. Ilitakiwa kuwa Kevin au yeyote ambaye wangemweka pembeni ili wakishazitoa dhahabu ndiyo aje na gari hilo, lakini kwa hali iliyomkuta Kevin, ilimbidi tu Kendrick ndiyo aje.
Gari likaegeshwa usawa wa dhahabu zile, naye Kendrick akashuka na kupokelewa vyema na vijana wake. Akawapongeza na kuwaambia kiutani kwamba sasa walikuwa wameongeza utajiri mwingi hata zaidi. Kisha vijana wote wakaanza kusaidizana ili kuziingiza dhahabu ndani ya lori. Wanaume walitoa chuma bapa ya shaba kutoka kwenye lori hilo na kuiweka chini, kisha wakawa wanaziweka dhahabu hapo na kuzipandisha sehemu ya wazi nyuma ya lori, ambako Lexi na Lakeisha wangezipokea na kuzihifadhi kwenye vitu kama mabeseni yaliyopangiliwa vyema.
Baada ya kazi hiyo yenye ugumu kiasi, walifanikiwa kuziweka dhahabu zote ndani ya lori. Ilikuwa imeshafika usiku sasa, na safari ya kuondoka ikaanza. Kendrick alirudi kukaa mbele pamoja na Victor ambaye aliendesha zamu hii, huku Lexi, Mensah, LaKeisha na Oscar wakikaa nyuma ya lori sehemu yenye dhahabu hizo wakifurahia story.
Mess Makers wakawa wamechafua hali ya hewa kwa mara nyingine tena.
★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★
Comments