Sehemu ya 9: Mtego wa Kimya
Gari lilitembea kwa mwendo wa haraka kupitia njia za vichochoro vya Tabata. Njia zilikuwa nyembamba, zenye giza zito, na taa chache za mitaani zilizokufa zikiwa mashahidi wa kimya wa jiji linaloishi kwa sura mbili: mchana na usiku.
Ayubu alikaa kwenye kiti cha abiria, mikono yake ikiwa imeshikilia mkanda wa usalama, macho yakizunguka huku na kule kwa hofu na mshangao. Mwanamke yule, ambaye bado hakuwa ametajwa jina, aliendelea kuendesha kwa ustadi mkubwa. Hakuwa tu dereva, alikuwa mtu aliyekuwa amefunzwa na maisha yenye hatari.
“Samahani, lakini hadi sasa sijajua jina lako,” Ayubu alizungumza kwa mara ya kwanza baada ya dakika kumi nzito za ukimya.
Mwanamke alitabasamu kwa upole huku akichezesha gia.
“Hilo jina halina umuhimu sana kwa sasa. Unahitaji kufahamu nani wewe kwanza. Halafu tutaweza kuzungumza kuhusu mimi.”
Ayubu alipumua kwa nguvu. Alijua anachotafuta si jina, bali ukweli.
“Basi niambie kitu kimoja tu—ni nani ananifuata? Na kwa nini?”
Mwanamke alitazama kioo cha nyuma kwa sekunde chache kabla ya kusema kwa sauti ya chini:
“Wanaitwa ‘Kivuli’... kundi lisilo rasmi, lisilosikika, lisilo na uso. Watu waliopotea katika historia, lakini wanaendesha mambo makubwa ulimwenguni. Wanataka kitu kilichofichwa ndani yako, Ayubu.”
Ayubu alishika kichwa chake kwa mkono mmoja, kana kwamba akili yake ilikuwa ikijaribu kuzuia mafuriko ya maswali yasiyo na majibu.
“Kitu gani kiko ndani yangu? Mbona sifahamu chochote? Hata wazazi wangu siwajui! Nimekulia mitaani. Hakuna aliyeweza kuniambia asili yangu.”
Mwanamke akapunguza mwendo, gari likapita barabara ya changarawe kuelekea kwenye nyumba moja ya ghorofa mbili iliyozungukwa na ukuta wa zege. Aliweka gari pembeni, kisha akageuka kumtazama Ayubu usoni.
“Na hapo ndipo jibu lilipo. Hujui asili yako kwa sababu ilifutwa kwa makusudi. Wewe ni mmoja wa watoto wachache waliotolewa kwenye programu ya siri iliyoitwa ‘Chanzo.’”
Ayubu alishtuka. Alikumbuka.
Neno hilo “Chanzo”—alilikuwa analisikia sana kutoka kwa watu waliomvamia, kutoka kwenye karatasi ya ajabu aliyopata, kutoka kwenye ndoto zake za utotoni ambazo hakuweza kuzifafanua.
“Programu? Kama vile jaribio?”
Mwanamke alishuka kwenye gari. “Njoo ndani. Tutazungumza kwa kina. Lakini jua hili Ayubu: maisha yako ya sasa si bahati mbaya. Ulikusudiwa kuwa mtu mwingine kabisa.”
Walitembea hadi ndani ya jumba hilo ambalo lilionekana kama limejengwa kwa matumizi ya zamani—milango mikubwa ya mbao, vioo vilivyopasuka nusu, na vumbi lililojaa kila kona. Lakini ndani kulikuwa na vifaa vya hali ya juu: kompyuta kubwa, skrini zinazoonyesha mitandao ya kamera, ramani za Dar es Salaam, picha za watu walioko kwenye hatari, na jina moja lililoandikwa kwenye ubao mweupe—AYUBU.
“Subiri,” Ayubu alisema kwa mshangao, “Hii ni nini sasa?”
“Hii ndiyo kituo chetu cha upelelezi. Mmoja wa waasisi wake alikua baba yako wa kupanga. Alikutunza kwa muda, kabla hajauawa.”
Ayubu alitikisa kichwa, machozi yakianza kujikusanya machoni.
“Kwa hiyo… nilikua nimeachwa kwenye kituo cha watoto si kwa sababu wazazi wangu waliniacha… bali walikuwa wameuawa?”
Mwanamke alimtazama kwa huruma. “Ni zaidi ya hivyo. Walikufa wakikukimbiza, wakikuokoa. Na sasa, ni wakati wako kurudi kwenye mizizi hiyo—kupambana kwa ajili ya ukweli, na kwa ajili ya wale waliokufa kwa ajili yako.”
Kimya kilitawala kwa dakika chache. Hatimaye Ayubu akasema kwa sauti tulivu lakini thabiti:
“Niko tayari kujua kila kitu. Lakini kabla ya yote—ni lazima nijue jina lako.”
Mwanamke akasogea mbele, akamuangalia usoni kwa muda mrefu, halafu kwa mara ya kwanza akasema:
“Naitwa Nasra. Nasra Ibrahim. Nilikuwa rafiki wa karibu wa mama yako.”
Ayubu akahisi dunia ikigeuka polepole.
Kabla hajafunguka zaidi, ghafla taa zote ndani ya jumba hilo zikazima.
Skrini zikaanza kuonyesha maandishi ya kisiri yaliyokuwa hayana maana moja kwa moja:
>> TUMEWAFUATA. USIKIMBIE. CHANZO NI YEYE.
Comments