Reader Settings

Chanzo ni Yeye
Sehemu ya 11
Na. Machokulenga TZ
0623238283

Taa za jiji la Dar es Salaam zilimulikiza anga kama nyota zilizokaribiana mno. Katika kona ya barabara ya Lumumba na Jamhuri, Ayubu alisimama kwa muda akijificha nyuma ya lori lililoharibika. Alikuwa amevaa koti refu jeupe la maabara, alilolivaa kutoka duka la Mama Saumu ili kujifanya daktari wa mazingira anayefanya utafiti wa usiku.

Bastola yake ilikuwa karibu, ikining’inia kwenye mkanda wa ndani wa suruali. Kifaa cha mawasiliano kilikuwa kimya tangu alipotamka maneno ya mwisho: "Nakuja."

Lakini moyoni alijua, alikuwa akilenga eneo la hatari. Aliingia kwenye nyumba ya ghorofa moja iliyokuwa imefungwa, akaingia kupitia dirisha la nyuma lililovunjika. Aliweka kifaa cha kuchanganua mawimbi ya kielektroniki na mara moja skrini ilionyesha ishara nyekundu—kuna mfumo wa ufuatiliaji wa sauti na kamera uliokuwa bado hai.

Alitambaa hadi chumba cha mbele na kuanza kuvuruga nyaya. Dakika tano baadaye, aliziona: kamera zilipoteza mwelekeo, taa za usalama zikaisha, na mfumo wa mlango wa siri ukafunguka. Alikuwa amefika kwenye kile kilichoitwa "Kituo B" kwenye faili alichopewa na Mama Saumu.

Chumba kilichojitokeza kilikuwa tofauti. Hiki hakikuwa chumba cha kawaida cha silaha au taarifa. Palikuwa na mapipa makubwa ya kemikali, vitabu vya uhandisi wa kijeni, na picha ya jengo kubwa la serikali. Kulikuwa pia na skrini kubwa ya LED iliyokuwa ikionesha ramani ya jiji—lakini si ya kawaida. Ramani hiyo ilikuwa ikionesha wigo wa "mionzi ya kibinadamu"—alama ya kipekee ambayo ilihusiana na aina fulani ya chembechembe za DNA.

Ayubu alisogea karibu zaidi. Alama nyekundu zilitanda zaidi maeneo ya Temeke na Kinondoni. Palikuwa na alama ya kijani, moja tu—maeneo ya Kunduchi—na ilikuwa ikielea, ikihama kama mtu anayesogea.

Mara mlango wa chuma ulifunguliwa kwa kishindo. Hakupata muda wa kufikiri. Alijirusha chini ya meza ya udhibiti, na kabla risasi haijaanza kulia, aliweza kuona miguu ya watu wanne wakiingia—wamevalia mavazi ya kijeshi, wakitumia bastola za kisasa zenye vibanio vya sauti.

"Target confirmed. Ayubu yuko ndani," mmoja alizungumza kupitia redio.

Akihitaji sekunde chache za kuishi, Ayubu alirusha bomu la moshi kutoka mfukoni mwake. Moshi mzito ulitanda, akakimbilia upande wa kulia, akaweka mtego wa mlipuko wa kelele kwenye mlango wa pili, kisha akarudi chini ya sakafu kwa kupitia kifuniko kidogo kilichokuwa karibu na jukwaa la udhibiti. Ilikuwa ni njia ya dharura ya kutoka.

Aliibukia katikati ya dampo karibu na Kawe, akivuja jasho, akihema kama mtu aliyepiga mbizi kwa dakika tatu mfululizo. Hapo ndipo alipoamua: muda wa kujificha umeisha. Alihitaji washirika. Lakini nani angemwamini kijana ambaye asili yake haieleweki, ambaye historia yake ni faili la kijeshi?

Kwa akili ya haraka, alimkumbuka mtu mmoja—Ally, fundi wa vifaa vya kielektroniki, aliyewahi kumsaidia kuunganisha simu ya kisasa ya ufuatiliaji. Ally alikuwa na duka lake nyuma ya jengo la Fire, karibu na Karume.

"We Ayubu?" Ally alishangaa kumwona akiwa na mavazi yaliyopauka, macho mekundu, uso wa kuchoka lakini mwenye azma kali.

"Nahitaji msaada wa haraka, Ally. Naamini mimi si mtu wa kawaida. Kuna watu wananifuatilia, na kila wanachokisema ni 'Chanzo ni wewe'."

Ally alimkazia macho, kisha akamvuta ndani. "Kabla ya yote... umekuja na mtu yeyote?"

"Hapana."

Ally alifungua droo chini ya meza, akatoa kifaa cha kuchunguza ufuatiliaji. "Simama hapa. Natafuta kama umewekewa chip yoyote au mionzi ya kufuatilia."

Dakika tatu baadaye, Ally alishtuka. "Bro... mwilini mwako kuna laini ya mionzi ya DNA, kama vile una kifaa ndani yako kinachotuma taarifa... na kinatumia chanzo chenye nguvu sana. Hii ni teknolojia ya kijeshi ya daraja la juu."

Ayubu alitetemeka. "Kwa hiyo wamekuwa wakinifuatilia kila mara... bila mimi kujua."

Ally alichukua sindano ndogo yenye sumu ya kuua chuma ndani ya mwili bila maumivu. "Nitakiondoa. Lakini utalazimika kupitia maumivu makubwa. Je, uko tayari?"

Ayubu alijibu kwa sauti ya chini lakini imara: "Nilizaliwa kupitia maumivu. Haya ni madogo."

Baada ya dakika 30, kifaa kiliondolewa, na Ayubu alihisi tofauti. Kichwa chake kilikuwa wazi zaidi, fikra zilitulia. Ally alimpa kifurushi cha vifaa: bastola ya kielektroniki, simu ya mawasiliano isiyoweza kufuatiliwa, na vifaa vya kutambua minong’ono ya redio.

"Haya yote hayatoshi," Ayubu alisema. "Nahitaji kujua ni nani aliyenitengeneza. Na kwanini."

Ally alinyamaza kwa muda kisha akamwambia: "Kuna mtu mmoja pekee anayeweza kukujibu. Anaitwa Nashiri. Alikuwa mkuu wa mradi wa majaribio. Anajificha kwenye mji wa chini ya ardhi ulioachwa miaka 20 iliyopita."

"Nashiri..." Ayubu alijirudia hilo jina. Sasa lilianza kujitokeza kwenye ndoto zake, sauti iliyokuwa ikimuita tangu utoto.

Bila kusubiri, alifunga kifurushi chake, akaingia mtaani, macho yake yakielekea mashariki ya jiji. Usiku huo haukuwa wa kulala. Ilikuwa ni mwanzo wa mapambano mapya. Na safari ya kuelekea kwenye majibu ya kweli ilianza rasmi.

Previoua Next