Mwisho wa Dunia Kimya Kimya – Episode ya Sita
Wakati jua la Kigoma likianza kuzama juu ya maji ya Ziwa Tanganyika, kila kitu kilionekana kutulia kwa nje — lakini ndani ya akili ya Najim kulikuwa na mapigano makali zaidi ya yote aliyowahi kushiriki. Wayota alikuwa ametoweka katika tukio lisiloelezeka vizuri. Imeli alikuwa kimya, macho yake yakiwa na huzuni ya mtu aliyejifunza maana ya kuwa na roho katika dunia isiyoamini roho zipo.
Katikati ya ukimya huo, sauti ya ndege wa porini ikachoma hewa kwa mlio wa kipekee — kama ishara kutoka enzi za zamani. Najim aligeuka polepole na kumkuta mzee mmoja akiwa ameketi kwenye jiwe karibu na mti wa mkuyu. Alikuwa mzee wa kweli, mwenye ngozi iliyochanika na macho yaliyokwishaona dunia mara mbili.
"Umerudi," alisema bila kumuuliza jina.
Najim alimtazama kwa mshangao. "Unanijua?"
Mzee alitabasamu. “Sijui jina lako. Lakini najua miguu yako imepitia barabara ambazo wengi walikwepa. Hiyo inatosha.”
Kabla hajauliza zaidi, Imeli alisogea na kuketi karibu na Najim. Alimtazama mzee huyo kwa heshima ya ajabu. “Unaitwa nani?”
“Mimi ni Mwandishi,” mzee alijibu. “Si jina, bali nafasi. Niliandikiwa kukaa hapa mpaka nione historia ikigeuka.”
Najim alihisi sauti ya ardhi ikianza kubadilika tena. Si kwa vurugu kama awali, bali kwa namna ya onyo la asili. Akakumbuka maneno ya Layna: ‘Ukifika Sifuri ya Dunia, utakuwa na dakika tano tu.’ Zile dakika tano zilikuwa zimeisha. Lakini walikuwa bado hai. Hilo lilimaanisha kulikuwa na mlango mwingine — au walikuwa kwenye historia ambayo haikutakiwa kuandikwa.
“Wayota yuko wapi?” Najim aliuliza.
Mwandishi akanyoosha mkono wake kuelekea maji ya ziwa. “Yuko kati ya sauti na ukimya. Kati ya waliokufa na waliokataa kufa. Anaandikwa tena.”
Imeli aliinamisha kichwa chake. “Tuna muda mchache. Hatujajua bado ni kwa nini mimi…”
Mwandishi alisimama, akaanza kuchora mduara kwenye ardhi kwa kutumia fimbo yake ya miiba. Kisha akaandika majina matatu: Imeli, Najim, na W.
“Nyinyi si watu watatu. Ni nguvu tatu zilizopishana kwenye mlolongo wa historia. Wakati Wayota alipopewa uhai wa ajabu, Najim alipewa uwezo wa kutambua mipaka ya ukweli. Na Imeli… alipewa nafasi ya kubeba kumbukumbu zote kabla hazijatokea.”
Najim alitikisa kichwa. “Sasa tunafanya nini? Dunia bado ipo kwenye hatari?”
“Hapana,” Mwandishi alijibu. “Sasa dunia iko katika hali ya uamuzi. Hili si tukio tena. Hii ni nadharia ya mwisho. Dunia itabaki kama ilivyo ikiwa mtamwachia Wayota awe upande wa historia. Lakini kama mtamtoa kabisa katika mlolongo huu — kila kitu kitabadilika, hata nyie wenyewe.”
Imeli alimshika Najim mkono. “Upo tayari kwa hilo?”
Najim alimtazama kwa macho tulivu. “Nilipochagua njia hii, nilijua siku moja nitakutana na ukweli ambao hautaniruhusu kurudi nyuma.”
Mwandishi alifumba macho na ghafla upepo mkali ulianza kuvuma. Majina yale matatu yaliyokuwa ardhini yalielea juu angani kama moshi wa tambiko. Ardhi ikavunjika kimya kimya, na anga likageuka kama kurasa zinazobadilika zenyewe.
Walijikuta katikati ya jiji la kisasa, Tokyo, lakini si Tokyo ya sasa — Tokyo ambayo haijawahi kuwapo. Magari yalisafiri hewani, majengo yalizunguka polepole kwa mzunguko wa kipekee. Na katikati ya mtaa mmoja, walimwona Wayota — akiwa kijana mdogo, akicheka na wenzake, akivaa sare ya shule. Hakuwa bado mtu wa kuogopwa. Alikuwa tu mtoto.
Najim alimtazama. “Hii ndiyo historia ya zamani?”
“Hapana,” Mwandishi alisema nyuma yao, sasa akiwa na sura ya kijana. “Hii ni nafasi ya mwisho. Kumpa chaguo.”
Imeli alitembea hadi karibu na kijana Wayota. Alisimama, akanyoosha mkono wake, akimpa kijitabu kidogo. Jalada lake liliandikwa: Kumbukumbu za Watu Waliokataa Kuwa Miungu.
Kijana Wayota alikipokea, akakifungua. Mara macho yake yakabadilika. Kuanzia sura ya furaha ya utoto hadi uso wa mtu mzima aliyeshindwa kutawala ulimwengu.
Ndani ya sekunde chache, kila kitu kilivunjika kama kioo kilichopigwa kwa mawe ya ukweli.
Najim na Imeli walikuwa peke yao tena — si Kigoma, si Tokyo, si kwenye treni. Walikuwa uwanjani, nyumbani kwao. Wakiwa hai. Wakiwa binadamu.
Imeli alimtazama Najim. “Hii ni dunia mpya?”
Najim akatabasamu. “Sidhani kama ni mpya. Nafikiri tumeirudisha tu mahali ilikopaswa kuwa.”
Comments