Reader Settings

FOR YOU 2

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Uhalifu, Mauaji, Visasi, Vita, Mambo yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA KUMI NA NANE

★★★★★★★★★★★★★★★★


Lexi alifika kule "chini" baada ya mwendo wa masaa kadhaa. Alipokelewa vizuri sana na Lakeisha pamoja na Torres, na wengine wakamwambia jinsi walivyomkosa sana. Walishangaa kiasi baada ya kuona ana jeraha dogo usawa wa mdomo na kuuliza alipatwa na nini, naye akasema aliumia tu kidogo lakini alikuwa sawa. Kevin alikuwa hapo pia, akiigiza kana kwamba amefurahi sana kumwona lakini kiukweli alichukia sana uwepo wake hapo. Ni moja kati ya wale watu wanaodharau sana wanawake, na kwa kuwa Lexi alipewa wadhifa fulani wa kuwa kama kiongozi kwao, hicho ni kitu kilichofanya ionekane ni kama yeye na wanaume wengine wanashushwa hadhi.

Baada ya wote kwenda kwenye chumba cha pamoja ili kuzungumza, Lexi akamkuta Kendrick tayari akiwa ameketi kwenye kiti cha mbele zaidi kwenye meza ndefu. Wakatazamana kwa sekunde chache, kisha Lexi akaangaliana na Torres, ambaye alimtikisia tu kichwa kumaanisha akakae, naye akaenda kuketi karibu na Lakeisha. Bado hali haikuwa sawa kati ya wawili hawa, na kiukweli Kendrick alikuwa anatamani sana kuzungumza na Lexi, ila ni kama alikuwa anajizuia tu. Lexi bado alikuwa na hasira naye, lakini hayo yangepaswa kuwekwa pembeni kwanza.

Torres akaanza kuwaambia kuhusu mahojiano yaliyopangwa leo kumwelekea Salim Khan. Wote walifahamu kuhusu milionea huyo kuiachia miradi mingi aliyokuwa ameishikilia kwenye serikali, na hiyo ilimaanisha huenda kulikuwa na ugomvi kwenye kundi lao la Raisi Paul Mdeme.

"Kwa hiyo inawezekana kwenye hayo mahojiano Salim akaropoka kila kitu, si ndiyo?" akauliza Victor.

"Sidhani sana. Hiyo inamaanisha kwamba kazi zake zote illegal zitawekwa wazi pia. Ni kwamba tu anataka kupata public opinion itakayokuwa upande wake, lakini ni wazi hili suala halijawafurahisha wenzake. Yeye kuondoa mkono wake kwenye mambo mengi kutamuumiza sana Mdeme, na kama mnavyojua, sifikirii Mdeme ataruhusu hilo litokee, ingawa haiko wazi kama atachukua hatua fulani," Torres akawaambia.

"Lakini Salim ana nguvu sana. Mdeme ataweza kumgusa?" akauliza Kevin.

"Mdeme hapana. Lakini vipi kuhusu Jacob na Weisiko?" akauliza Torres.

"Yeah... hao jamaa wanaweza wakafanya jambo fulani," akasema Mensah.

"Lakini hiyo inatuhusu sisi vipi? Kama ni kuuana, wauane tu," LaKeisha akasema.

"Yes, ndiyo maana tuko hapa. Tunahitaji kujadiliana kujua watafanya nini. Ikiwa watamwacha, baadaye tukijaribu kuwafichua itakuwa pointless kwa upande wa Salim, na ikiwa watachukua hatua fulani, basi... maybe... probably... hiyo itakuwa na faida kwetu. Lakini haimaanishi kwamba tunapaswa tukae tu tusubiri lolote maana hii kwa njia fulani inaweza ikatu-impact sisi pia," akasema Torres.

"Kwa hiyo tufanye nini sasa?" akauliza Victor.

"Kwa nini tu tusimtumie Mensah ampasue huyo mwanaume bichwa lake? Na hata hao wengine. Problem solved," akasema Kevin.

"Yeah, halafu mipango yetu yote iwe ya kazi bure," akasema Mensah.

"Mipango ipi? Sijaona jambo lolote likifanyika tokea Oscar alipo...."

"Kevin!" LaKeisha akamkatisha.

Kevin akatulia tu na kukunjia mikono yake kifuani.

Kendrick akamtazama Lexi kwa makini. Lexi alikuwa ametazama mezani akionekana kutafakari jambo fulani.

"Lexi..." Kendrick akaita.

Wote wakamwangalia Lexi. Yeye akageuza kichwa taratibu na kumtazama Kendrick pia.

"Unawaza nini?" Kendrick akamuuliza.

Lexi akatulia kidogo, kisha akasema, "Tutapaswa kwenda."

Wengine wakaanza kuangaliana.

"Kwa nini?" akauliza LaKeisha.

"Kwa sababu Torres yuko sahihi. Jacob na Weisiko hawataruhusu Salim afanye jambo hilo. Ni lazima watafanya kitu fulani leo kwa sababu Salim atakuwa sehemu vulnerable zaidi," Lexi akasema.

"Sehemu ambayo itakuwa na waandishi wa habari ni vulnerable?" akauliza Victor.

"Anamaanisha eneo zima," akasema Torres.

"Sasa kwa nini sisi tunatakiwa kwenda?" akauliza Victor.

"Kwa sababu ile ile ya Oscar. Ikiwa Mdeme alikuwa anataka tu kumkamata mmoja wetu lakini mtu mwingine akatokea na kumuua, hiyo inamaanisha ni Jacob au Weisiko ndiyo walikwenda kinyume naye," Lexi akasema.

Torres akaangalia pembeni na kusema, "Of course... sasa ninaelewa."

"Unaelewa nini?" akauliza Kevin.

"Ni Weisiko na Jacob ndiyo waliomtuma yule assassin kuwafata Oscar na Mensah. Hawataki tukamatwe tukiwa hai kwa sababu... wanaogopa tutaweka kila kitu wazi kuwahusu. Kwa hiyo inaonekana... aisee... Lexi una kichwa dada! Kila mara ambayo Luteni Michael atatukaribia basi huyo assassin anatakiwa kuwepo ili kuzuia tusishikwe, lakini tuuawe. Ndiyo maana hakumuua Luteni ila wenzake tu. Nilikuwa wapi kuona hilo?" Torres akaongea kwa utambuzi.

"Ulikuwa unakula LaKeisha tu," Mensah akasema.

LaKeisha akacheka kidogo.

"Kama Lexi yuko sahihi, basi huyo assassin atakuwepo leo kwa ajili ya Salim," akasema Torres.

"Oookay... kwa hiyo tunatakiwa tuwepo ili kumkamata huyo mpumbavu," akasema Victor.

"Yeah," akajibu Torres.

"Tuna uhakika gani kwamba hilo litatokea? Kwa sababu tu Lexi kasema?" Kevin akaongea.

"No. Ni kwa sababu ubongo wako uliojaa viazi haungeweza kamwe kufikiria mambo namna hiyo," LaKeisha akamwambia.

Kevini akamwangalia kwa hisia kali.

"Fanyeni Lexi anavyosema. Ni lazima huyo mtu tumkamate," Kendrick akaongea.

"Boss, tukienda tunaweza kuhatarisha usalama wetu wote," Kevin akamwambia Kendrick.

"Kwani nani amesema wewe unaenda?" LaKeisha akamuuliza.

Kevin akashangaa na kumwangalia Lexi.

"Kwa hiyo... nyie wote mtaenda, lakini mimi ndiyo natakiwa kubaki? Na mtatumia njia gani ya haraka wakati muda umeshaisha?" Kevin akauliza.

"Lexi atatupanga. Boss, file ulilotaka nimeshaliweka kwa flash, liko mezani kwako," Torres akasema huku akiondoka haraka.

Wengine pia wakaanza kunyanyuka. Kendrick alikuwa amefurahi sana kwamba Lexi alitokeza jambo jipya hapo, lakini akatulia tu na kuendelea kumwangalia. Lexi aliposimama na kutaka kuuelekea mlango, Kevin akafika mbele yake kama kumzuia.

"Unajua kukaa huku nahisi ni kama adhabu, siyo kulindwa. Niruhusu na mimi nije na nyie leo. Tafadhali," Kevin akasema kwa sauti ya chini.

"Wewe tuliza tako lako huku bana," Mensah akamwambia na kumpita.

Lexi akataka kupita pembeni, lakini Kevin akamzibia njia tena.

"Kevin... we' ni mjinga?" LaKeisha akamuuliza.

"Boss, Lexi, sikieni. Mimi kiukweli nime...."

"Kevin... mpishe," Kendrick akamkatisha namna hiyo.

"Boss!" Kevin akasema kinyonge.

Akamwangalia tena Lexi machoni, ambaye alikuwa anamtazama kiumakini sana, naye akampisha na kumwacha atoke.

"Asshole!" LaKeisha akamwambia hivyo na kutoka pia.

"Ahahahah... usicheze na huyo demu, atakuja akuzibe siku moja," Victor akamwambia pia huku akicheka, kisha naye akaondoka.

Kevin alibaki kumtazama Kendrick kwa njia ya kutaka aonewe huruma, lakini Kendrick akanyanyuka tu na kumpita bila kumsemesha lolote. Tokea mpango wake aliomshawishi Kendrick afanye ulipovurugwa na Lexi, boss wao huyo hakuwa amemsemesha lolote lile, ikionekana ni kama alimkasirikia kwa njia fulani kwa sababu ya kumsababishia utofauti na "binti yake" kipenzi. Jamaa akakunja ngumi kwa hasira sana, akiweka chuki kuu moyoni mwake, naye akajiahidi kwamba ni lazima angefanya kitu fulani kuhusiana na haya yote.


★★★


Mkutano wa mahojiano maalum ambayo yangefanywa kuhusiana na milionea Salim Khan kuacha kuunga mkono mingi ya miradi ya serikali ulikuwa umewadia. Maandalizi mengi yalifanywa na waandishi wa habari walifika mapema kwenye ukumbi ambao yangefanyikia. Ilikuwa ni kwenye mida ya jioni sasa, huku giza likivizia kwa mbali kadiri ambavyo watu waliendelea kuongezeka. Kwa kawaida mambo kama haya yangefanywa pakiwa bado mchana, lakini kwa sababu zake Salim alitaka iwe jioni.

Viongozi kadhaa wa mkoa walikuwepo pia, naye ACP Nora alifika hapo pamoja na Halima ambao kwa pamoja walikaribishwa na Emiliana Ngoyi pamoja na Secretary Joachim. Nora alimweleza Joachim kwamba walipaswa kuwa macho kuelekea hafla hiyo kwa kuwa kwa njia fulani ilihusiana na utata wa Mess Makers waliokuwa wanaufuatilia, naye Joachim akamhakikishia kuwa mambo yote yangekuwa sawa.

Upande wa nje ndiko watu kadhaa walikuwepo wakipeana salamu na kuwakaribisha wengine waliofika hapo, na hatimaye wakafika wageni ambao hawakutarajiwa kufika. Ilikuwa ni Jenerali Jacob Rweyemamu, akiwa pamoja na Luteni Jenerali Weisiko, nao wakapokewa kwa shauku kama vile ndiyo walikuwa wageni rasmi. Jenerali Jacob hakuwa akionekana mara nyingi hadharani, hivyo kwa wengi kumwona hapa walijua bila shaka aliliona suala hili kuwa muhimu mno mpaka kuamua kuja. Baada ya baadhi ya watu kusalimiana nao, wawili hawa wakaelekea ndani pamoja kusubiri Salim afike hapo.

Kwa mara ya kwanza kabisa katika kipindi kirefu, Jenerali Jacob alikutana ana kwa ana na binti yake, yaani ACP Nora, nao waliangaliana kiufupi kutokea pande tofauti zenye viti kwa ajili ya wadau ambao wangekuwepo hiyo siku. Nora alimpuuzia upesi na kuketi tu pamoja na Halima, naye Weisiko akamsihi Jenerali Jacob akae pia kwa sababu huu haukuwa wakati mzuri sana kuingiza hisia hapo. Secretary Joachim hata akamtumia Nora ujumbe kwa simu kuuliza kama alijua Jenerali angekuja, lakini akakanusha na kusema hakutaarifiwa hilo. Uwepo wa baba yake hapo ulimkera sana, lakini kama kawaida yake akampuuzia tu na kuendelea kusubiri kilichompeleka.

Katika kundi la waandishi wa habari walioingia ndani ya ukumbi huo, LaKeisha pamoja na Victor walikuwepo pia. Walijichomeka ndani hapo na kujifanya kama walikuwa waandishi wa habari kutoka kituo fulani, na hii ilisaidiwa na vitambulisho bandia ambavyo Victor alitengeneza kwa ajili yao. Walikuwa na vifaa vidogo masikioni ambavyo vingesafirisha mawimbi ya sauti kwa wenzao kuwaambia yaliyoendelea ndani endapo kama kuna jambo lingetokea.

Upande wa nje wa jengo hilo la ghorofa, Lexi pamoja na Mensah walikuwa ndani ya gari ndogo aina ya Polo wakisubiri kutokea umbali mfupi. Ni wawili hawa tu ndiyo waliokuwa ndani ya mavazi yao ya mapambano, tayari kabisa kuonyesha vitendo wakati ambao shida zingeanza.


★★


Haukupita muda mrefu sana, na hatimaye Salim Khan akawa amefika eneo hilo. Alilindwa na watu wenye silaha nzito na waliokuwa na mwonekano wa kikomando, nao wakamsindikiza alipoingia kule ndani ya ukumbi. Lexi aliwakumbusha LaKeisha na Victor kwamba walipaswa kuangalia sehemu za pembeni za eneo hilo la ndani kuona ikiwa wangepata kitu ambacho hakijakaa sawa, na Torres, ambaye alikuwa amebaki kule "chini" awe macho kwenye mitambo yake ili kumpa habari yoyote yenye kuvuta uangalifu.

Basi, baada ya Salim Khan kufika ndani kule na kupokelewa na wengi, akawatazama Jenerali Jacob na Weisiko, ambao wao walikuwa wamekaa tu wakimwangalia kwa kutopendezwa, naye Salim akachekea pembeni na kupanda sehemu iliyokuwa kama jukwaa dogo lenye meza ndefu. Akaketi kiti cha kati na kuanza kutoa salamu tena kwa wote, kisha akaanza kuongelea kuhusu mafanikio ambayo yeye na kampuni zake zimeiletea nchi hii kwa miaka mingi.

Waandishi wa habari walipokuja kupewa fursa za kuanza kuuliza maswali, wengi waliuliza maswali ambayo yalikuwa yanalenga ni kwa nini sasa Salim aliamua kuiachia miradi mingi ambayo bila shaka ingeporomoka kwa kuwa kipindi hiki kilikuwa kigumu hasa kwa sababu ya Mess Makers. Salim akaeleza kwamba kwa miaka mingi amejitahidi sana kuwekeza chochote alichoweza kwenye serikali na kusaidia katika maendeleo, lakini kama tu ambavyo hali imekuwa ngumu kwa serikali wakati huu, imekuwa ngumu kwake pia. Akasema kwa kujitutumua kuwa ni kama tokea wakati ambao Mess Makers wameizingua serikali yeye ndiyo aliyebaki kuibeba, na sasa kuna watu ambao wanachukulia hiyo kwa faida mbaya sana na kumbebesha mizigo mizito mno.

Maswali mengi yalizuka. Wengi waliuliza ina maana Raisi alikuwa ameshindwa kurekebisha hali? Kwa nini amtegemee Salim wakati yeye ana nguvu kubwa akiwa kiongozi wa nchi? Na ni kwa nini hakuwa hata ameomba msaada kutoka nje kuhusu kuwatafuta na kuwadhibiti Mess Makers? Aliogopa nini? Jenerali Jacob na Luteni Jenerali Weisiko waliona kwamba Salim Khan alifanya haya yote kama kuwakomoa wao na kundi lao ambalo jamaa ndiyo alikuwa anatengeneza njia ya kulivuruga.

Waandishi wa habari walipokuwa wakiendelea na maswali huko ndani, Lexi pamoja na Mensah wakasikia sauti ya helicopter ikipita eneo hilo. Giza lilikuwa limeshaingia, lakini wakaiangalia kwa umakini kuona ingeelekea wapi. Ilipita karibu kabisa na jengo hilo walilofanyia mkutano ule, kwa juu, nayo ikaelekea upande mwingine tofauti. Lexi akamjulisha Torres kuwa kuna helicopter imetoka kupita hapo muda siyo mrefu, atafute ni ya wapi na rubani angekuwa nani kabla haijaharibiwa.

Torres akauliza ni kwa nini Lexi alifikiri helicopter hiyo ingeharibiwa, naye akamwambia inaonekana ilimshusha mtu kule juu, labda mtu wao yule waliyekuwa wanamtaka, hivyo bila shaka watu hao wangejitahidi kuharibu jambo lolote ambalo lingeweza kutumiwa kama ushahidi, lakini yeye Lexi alichotaka hasa kujua ni ilikokuwa imetokea. Lexi pamoja na Mensah wakawataarifu LaKeisha na Victor kuhusu jambo hilo na kuwaambia wawe macho sana, kisha wawili hawa wakafunika sura zao, Mensah akibeba bastola yake, nao wakaanza kuelekea karibu zaidi na jengo lile.

Ilikuwa ni wakati huu ndipo Salim Khan alisema kiutani kwamba alihitaji "dinner" kwanza, hivyo angeenda kupata chakula halafu angerudi wakati mwingine kujibu maswali mengi zaidi, naye akanyanyuka na kuanza kuondoka. Waandishi wengi bado walikuwa na maswali kama yote, wakiendelea kuuliza na kumfuata, huku Salim akiondoka pamoja na walinzi wake. Alielekea mpaka kwenye lifti na kuingia na walinzi wake, kisha wakaanza kupanda ghorofa za juu. LaKeisha akamwambia Lexi yaliyokuwa yanaendelea, naye Lexi akatambua kwamba mtu yule bila shaka angekuwa ameingia kwenye sehemu ya lifti. Akawaambia LaKeisha na Victor waondoke huko haraka ili wajiunge na Mensah kwenye gari kubadili mavazi, wakati yeye akitangulia kumfata.

Lexi alikuwa sahihi kabisa. Kwa sababu ni "silaha" yule wa Weisiko ndiyo alikuwa amefika huko, naye aliingia upande wa juu wa lifti kwenye nyaya nene zilizoiendesha. Wakati lifti ilipokuwa bado ikisonga kuelekea juu, akachukua mtungi mdogo sana wa gesi fulani na kufungua mlango wa juu wa lifti hiyo, kisha akaifungua sehemu ya gesi hiyo na kuitupia kwa ndani. Salim na walinzi wake walishtuka sana. Waliangalia juu na kutoona chochote kwa kuwa gesi hiyo ilijaza moshi mzito na kuwamaliza nguvu kabla hata hawajafikiria kufanya lolote. Wote wakaanguka na kupoteza fahamu zao ndani ya lifti hiyo iliyokuwa imebakiza hatua chache tu kufika ghorofa ya mwisho.

"Silaha" huyo akafungua mlango huo mdogo wa juu, yeye akiwa amevaa kizuizi cha kuingiza gesi puani na mdomoni, kisha akaingia ndani hapo haraka akiwa ameshika kamba nene iliyofungwa kama kitanzi mwishoni na kuipitisha shingoni mwa Salim. Alipoangalia zimebaki ghorofa ngapi, akaona imebaki moja na mlango wa lifti ungefunguka, hivyo akawahi kupanda juu kule upesi na kuuacha mlango ule mdogo wa juu wazi, naye akapanda juu zaidi, kisha akatoa kifaa fulani kidogo cha kukata chuma kutoka kwenye mkanda wake kiunoni na kuanza kuzikata nyaya zile zilizoishikilia lifti.

Wakati lifti ilipokuwa imefika tu mwisho na kufungua milango yake, kulikuwa na watu watatu hapo nje wakisubiri kuingia, nao wakashangaa sana baada ya kuona mambo yote ya ndani hapo. Walitambua watu waliokuwa wamelala humo walikuwa ni walinzi, na aliyewekewa kitanzi shingoni alikuwa ni Salim Khan. Mmoja akasema kwa wengine wawahi kuita msaada, lakini ikawa kuchelewa. "Silaha" yule alikuwa ndiyo amemaliza tu kukata nyaya nene ya mwisho, hivyo lifti hiyo ikaachia na kuanza kurudi chini kwa kasi sana!

Kamba ile aliyomfungia Salim shingoni ilikuwa imefungwa huko huko juu, hivyo lifti ile ilipoachia, kamba hiyo ikamning'iniza Salim kwa njia ya kunyonga. Hii ilifanya sehemu ya mkono wake wa kushoto ivunjike (yaani kukatika kabisa) kwa sababu mwili wake ulikuwa mnene kiasi na hivyo lifti iliposhuka na yeye kuvutwa, alipitishwa kwenye mlango ule mdogo wa juu na kubaki amening'inia.

LaKeisha pamoja na Victor walikuwa tu ndiyo wamefika nje, pale waliposikia sauti ya kishindo kikubwa sana kutokea kule ndani. Kiliwashtua wengi sana, na baadhi ya waandishi waliokuwa nje tayari wakaanza kurudi ndani tena. Victor akamtaarifu Lexi kuhusu hilo, naye Lexi akasema abaki ili kujua ni nini, lakini LaKeisha amfate Mensah kisha wamsubiri Victor mpaka atakapotoka kule ndani. 

Lexi tayari alikuwa amezungukia upande mwingine wa jengo peke yake, akiwa mwangalifu sana ili asitambulike. Alitazama kule juu kwa umakini kutokea alipokuwa, naye akamwona mtu yule akiruka kutoka juu ya ghorofa hilo mpaka kwenye ghorofa lililokuwa jirani. Lexi akasema amemwona na angeanza kumfata, hivyo Torres awaongoze Mensah na Lakeisha kuhusu kule ambako angekwenda baada ya Victor kujiunga nao. Alikimbia kwa kasi sana na kuvuka njia nyingi ambazo kufikia wakati huu hazikuwa na watu wengi sana kwa sababu ya wengi kwenda kujua kishindo kile kilitokana na nini.

Wakati Lexi akiwa bado anakimbilia upande wa adui, Victor aliwataarifu wenzake wote sasa kuwa Salim Khan aliuliwa kwa kunyongwa ndani ya lifti, na lifti hiyo ilikatwa na kuangushwa mpaka chini ikiwa na wanaume sita wa ulinzi ndani yake, nao pia wakiwa wamekufa baada ya kuvunjwavunjwa kwa viungo vyao. Taarifa hiyo haikuwa nzuri au mbaya kwa Mess Makers, kwa sababu lengo lao hapa lilikuwa ni huyu mtu asiyejulikana ambaye alimuua Oscar, hivyo Torres akamwambia Victor ajiunge na wenzake ili wakamsaidie Lexi.

Lexi alifanikiwa kumwona mtu yule akishuka kutoka kwenye ghorofa lingine na kuanza kukimbilia upande ambao Lexi alijua kulikuwa na uwanja mpana wa mazoezi, naye akaongeza kasi na kumzungukia kwa mbele. Kule "chini," aliyekuwa amebaki pamoja na Torres ni Kendrick na Kevin, nao walikuwa wakifuatilia kila jambo kwa umakini pia. Kendrick akamuasa Lexi awe makini sana kwa sababu iliwezekana huu kuwa mtego, naye Lexi akasema angekuwa makini.

"Silaha" yule alifika sehemu ya pembezoni ya uwanja huo na kusimama huku akiwa anapumua kwa nguvu sana. Usiku huu alivalia nguo zile nyeusi kama kawaida yake, lakini wakati huu kiziba uso chake kilikuwa kwenye uso mzima na kuacha sehemu ndogo tu kwa ajili ya macho. Wakati akiwa ametulia hapo akisubiri jambo fulani, akahisi mtu akija nyuma yake, naye akachomoa kisu kutoka kwenye mkanda kiunoni kwake haraka na kukirusha upande huo wa nyuma. Lakini ilikuwa ni Lexi, naye akakikwepa na kumrukia mtu huyu na wote kuanguka chini, kisha wakasimama na kuangaliana wakiwa wamejiweka tayari kupambana.

Hii ilikuwa ni mara ya tatu wanakutana, na Lexi alikuwa anataka kuifanya iwe mara ya mwisho. Alikuwa na lengo moja tu hapa, kumlipizia kisasi Oscar kwa kile ambacho mtu huyu alimfanyia, na kisha kukikata kichwa chake na kukituma kwa Jenerali Jacob kama ujumbe kuwa akicheza vibaya na Mess Maker mmoja, amecheza vibaya na wote. Bila kusubiria refa aitwe, Lexi akamfata mtu huyo na kuanza pambano naye. Walikuwa wanapigana kwa njia zenye ustadi sana, na kila mara ilionekana ni kama hawangeweza kuumizana kwa sababu kila mmoja wao alijua kuyazunguka mapigo ya mwenzie.

Lexi alitambua kuwa mtu huyu alipigana kwa mtindo fulani wa "Tai chi," hivyo yeye akaanza kutumia mitindo mingi yenye kuchanganya kwa wakati mmoja. Mtu huyu alikuwa akitafuta njia nyingi sana za kumpiga Lexi kwa mtindo ule unaowamaliza nguvu maadui zake, lakini akagonga mwamba. Ijapokuwa mtu huyu alifanikiwa kumpiga Lexi hapa na pale, Lexi alimpiga chenga nyingi haswa na kufanikiwa kumtandika sehemu fulani za mwili zenye udhaifu, na mtu huyu akaanza kuonekana kuishiwa ujanja. 

Akatoa kisu na kutaka kukitumia kumkata tumboni, lakini Lexi akazungusha mikono yake na kumpiga kwa teke mgongoni, kisha akamfata na kumkaba shingoni akiwa nyuma yake. Alikuwa na hasira sana, na baada ya kuona nguvu zinamwishia mtu huyu, akamrusha pembeni na kubaki akimwangalia huku anapumua kiuchovu.

Wakati Lexi alipokuwa amemrusha mtu huyo namna hiyo, ilifanya kificha uso cha mtu huyo kidondokee pembeni, naye akawa anajivuta chini taratibu kama anatambaa kwa tumbo kuelekea mbele, kwa hiyo bado Lexi hakuwa ameiona sura yake. Lakini alipoanza kumfata taratibu, akatambua kuwa nywele za mtu huyo zilikuwa ndefu na laini, zilizobanwa nyuma ya kichwa chake kwa njia iliyomfanya Lexi atambue kuwa huyu alikuwa mwanamke. 

Akaokota kiziba uso chake kile, kisha akamsogelea karibu zaidi na kumponda nacho kisogoni. Mtu huyo hakugeuka, naye Lexi akatambua kuwa hakutaka aione sura yake, hivyo akamkalia mgongoni na kuvuta nywele zake kwa nguvu sana. Mwanamke huyu akatoa sauti ya maumivu kidogo na kujaribu kufurukuta, lakini Lexi akamdhibiti.

"I'm going to kill you the same way you killed my friend (nitakuua kwa njia ile ile uliyotumia kumuua rafiki yangu)."

Lexi akanong'oneza maneno hayo kwenye sikio la mwanamke huyo, naye akakishika kichwa chake na kutaka kukinyonga kwa nguvu, lakini mwanamke huyo akatumia wepesi wake kuugeuzia mwili upande ambao Lexi aliipeleka shingo yake, hivyo sasa akawa amelalia mgongo wake. Lexi alikuwa ameweweseshwa kidogo kutokana na hilo, lakini akamwahi tena na kuikaba shingo yake kwa kiganja kimoja, huku akitaka kumtandika ngumi usoni kwa kingine, pale mkono wake ulipoganda hewani tu baada ya kutokuamini kile alichokiona. 

Yaani, hakuamini kabisa macho yake. Alimwangalia mwanamke huyu kwa mshangao wa hali ya juu, asiamini na asiamini kwamba kweli alichokiona kilikuwa halisi. Mkono aliokuwa ametumia kumkaba shingoni ukalegea, na ngumi yake ikashuka. Alihisi kuishiwa nguvu ghafla kwa sababu hakutegemea jambo hili hata kidogo.

"Azra?!"

Lexi akaita hivyo kwa sauti ya chini, yenye kuonyesha hisia sana. Mwanamke huyo akakunja uso wake kimaswali, naye akakusanya nguvu na kumsukuma Lexi ambaye alidondokea pembeni yake. Lexi akajivuta chini hapo na kuendelea kumwangalia kimshangao, huku mwanamke huyo akijishika shingoni akiwa anamwangalia adui yake kwa hasira.

"Azra... A... Azra..."

Lexi akaendelea kuita jina hilo, kwa sababu mwanamke huyu alikuwa na sura kama ya mdogo wake wa kike, ambaye alijua miaka mingi iliyopita alipoteza uhai pamoja na watu wengine wa familia yake. Alishindwa kuelewa nini kilikuwa kinaendelea, na mwanamke huyo akasimama na kubaki anamwangalia Lexi kimaswali. Lexi alielewa kwamba hangeweza kumtambua yeye ni nani kutokana na kiziba uso chake usoni, hivyo naye akasimama na kuanza kukitoa. Mwanamke huyo alikuwa anamshangaa sana kwa nini anafanya yote hayo, na baada ya Lexi kuivua mask yake, akamkazia macho kwa uangalifu.

Lexi alikuwa anamwangalia kwa matumaini mengi, akifikiria huenda huyu alikuwa ni mdogo wake, na labda kumwonyesha sura yake kungebadili mambo, lakini haikuwa hivyo. Mwanamke huyo akakunja uso na kuanza kumfata tena, kisha akaendelea kumshambulia.

"No... Azra... subi.... wait...."

Lexi akawa anajitahidi kukwepa mapigo yake na kumwambia aache ili waongee, lakini ilionekana ni kama wehu ulikuwa umempanda mwanamke huyo kwa sababu hakutaka kusikiliza. Lexi hakuelewa kwa nini mdogo wake hakumtambua, na hii ilimfanya ahisi simanzi nzito moyoni mwake. 

Mwanamke huyu akafanikiwa kumpiga Lexi sehemu za viwiko na mabegani kwa mtindo wake ule uliomfanya apoteze nguvu mikononi, naye Lexi akapiga magoti chini. Mwanamke huyo akaokota kisu na kutaka kumchoma nacho, lakini Lexi alipomwangalia usoni kwa huzuni, mwanamke huyo akasita kidogo. Alibaki kumtazama Lexi kimaswali sana, huku Lexi akidondosha machozi kwa hisia.

"Lexi!"

Wawili hawa wakashtushwa na sauti hiyo kutokea upande ule walikotokea mpaka kufikia uwanjani hapo. Ilikuwa ni LaKeisha ndiye aliyeita hivyo, na baada ya Lexi kugeuka akamwona Mensah akiwa ameelekeza bastola yake kwa mwanamke huyu aliyekuwa na sura ya mdogo wake, hivyo akajitahidi kusimama upesi na kumziba. Risasi mbili alizofyatua Mensah zilimpata Lexi kifuani, lakini hakuumia kutokana na nguo yake kuzizuia, naye akadondoka chini tena.

Mwanamke huyo akashangaa sana baada ya kuona jambo alilofanya Lexi, lakini akageuka hapo hapo na kuanza kukimbilia upande mwingine, na Mensah alipotaka kumpiga risasi zingine, Lexi akamwambia kwa sauti ya juu kuwa amwache. LaKeisha na Victor wakafika hapo chini na kujitahidi kumnyanyua Lexi, huku wakimwangalia mwanamke yule anatokomea gizani. Mensah alipofika karibu akamuuliza Lexi ni nini maana yake kumzuia asimpige adui yao huyo na kumwacha atoroke, naye Lexi akabaki tu kupumua kiuchovu huku akiwa amechoka sana kiakili.

Alijiuliza sana swali hili: Iliwezekanaje Azra kuwa hai?

                          END OF SEASON 2 

Previoua Next