Reader Settings

FOR YOU 3

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Uhalifu, Mauaji, Visasi, Vita, Mambo yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA PILI

★★★★★★★★★★★


Upande wa jengo lile ambalo mauaji ya milionea Salim Khan yalifanyika, maafisa wa usalama walikusanyika hapo muda mfupi tu baada ya tukio. Tayari baadhi ya waandishi wa habari waliokuwepo walichukua picha na video za lifti ile iliyoanguka kutoka juu ya ghorofa, na mambo mengi yaliulizwa kuhusu ni nini kilichotokea. ACP Nora alikwenda kule juu pamoja na Emiliana Ngoyi, Secretary Joachim, na maaskari wengine ili kuchunguza mkasa huo, na baada ya muda wakawa wamefanikiwa kuutoa mwili wa Salim kwa uangalifu sana; uliokuwa umejeruhiwa vibaya sehemu ya mkono.

Nora alighafilishwa sana na mambo aliyoona. Jambo hili lilimkumbusha kuhusu usiku ule ambao mmoja wa wale Mess Makers alimsaidia kwa kuwaua wanaume waliotaka kumtendea vibaya kimwili, naye akawa anajiuliza ikiwa ni huyo ndiye aliyefanya na ukatili huu pia. Lakini kwa nini? Mess Makers wangepata faida gani kwa kumuua Salim Khan, mwanaume ambaye alikuwa hagusiki? 

Alijadiliana na Emiliana pamoja na Joachim na kuona hata wao walihisi kuna mchezo mkubwa uliofanyika nyuma ya pazia. Kila shuku ilimwelekea mtu mmoja tu; Raisi Paul Mdeme, kwa kuwa ilikuwa wazi kwa mtu yeyote kwamba jambo alilofanya Salim la kuiachia miradi ya serikali halikumfurahisha Raisi, hivyo tukio la namna hii moja kwa moja lingefanya aelekezewe vidole. Lakini muda si mrefu lawama ikapata mfadhili.

Maaskari waliochunguza chuma la lifti iliyoharibiwa walipata kibandiko (sticker) cha aina ile ile walichotumia Mess Makers kila walipofanya tukio fulani, yaani sura ya simba mweupe anayenguruma. Kilikuwa kimebandikwa kwenye sehemu ya chuma iliyokunjika, na mkataa wa haraka uliofikiwa ukawa kwamba Mess Makers ndiyo waliohusika na mauaji ya Salim Khan pamoja na walinzi wake. Jenerali Jacob na Luteni Jenerali Weisiko wakaongea mambo machache kuhusiana na "ushahidi" huo, wakisema kwamba kwa sababu ya kitendo hicho, Mess Makers walihitajika wakiwa hai au wamekufa. Jenerali Jacob akaahidi kwamba angewakamata wote na kuhakikisha wanalipia kwa kifo cha Salim, na baada ya hapo yeye na Weisiko wakaondoka tu.

Kibandiko hicho chenye picha ya simba kilikuwa ni uthibitisho kwa wengi hapo kwamba Mess Makers ndiyo waliohusika na mauaji, lakini kwa Nora haikuwa hivyo. Alielewa kwamba kuna mambo ambayo yaliingiliana baina ya serikali, milionea huyo, na hao Mess Makers, lakini bado uthibitisho huo haukumshawishi kabisa kwamba ni Mess Makers ndiyo waliofanya haya. Akili yake ikamwambia kwamba kuna mtu alitaka ionekane hivyo ili kuficha utambulisho wake, na hakuna yeyote ambaye angefikia kiwango cha juu cha kushuku isipokuwa Raisi Paul Mdeme. Lakini akaona akae kimya kuhusiana na wazo hilo.

Baada ya muda, wengi waliokuwa eneo hilo wakatawanyika, naye Nora akarejea kule hotelini kwake kupumzika. Gumzo lililokuwa limeanzishwa kwa sababu ya tukio hilo lingeendelea kwa muda mrefu sana, Nora alijua hilo. Kwa hiyo kuanzia sasa alitambua angepaswa kuzama zaidi kwenye utafiti wake wa matukio haya, hasa kwa sababu mambo mengi yalikuwa yanaingiliana kwa njia zenye kuchosha sana akili. Jambo lingine muhimu zaidi kwake ilikuwa ni kujua Lexi ni nani hasa, kwa sababu baada ya kugundua kuwa naye alitokea Ghana kama tu Oscar Amari, kichwa chake kilimsumbua mno kwa maswali.

Uwezekano wa mwanamke yule kuingia kwenye maisha yake ili kumzunguka ulionekana kupatana na akili, lakini bado alitumaini yale yote ambayo alihisi kumwelekea hayakuwa ya kweli. Akaamua kuingia kulala tu, ili kesho aanze kutafuta ukweli kwa nguvu zote.


★★★


"CHINI"


Mess Makers wanne waliokuwa kwenye tukio lililompata Salim Khan walikuwa wamefanikiwa kuondoka Dar es Salaam na kufika kule kwenye nyumba yao ya maficho, a.k.a "chini." Ilikuwa imewachukua masaa kadhaa kama kawaida, na sasa Lexi alikuwa amerejesha nguvu mwilini mwake. Safari nzima ya kuelekea huko, wengine walikuwa wakiongelea kuhusu jambo lililompata Salim Khan, huku mara kwa mara Lexi akisemeshwa, lakini hakutoa jibu lolote. Alikuwa kimya mwanzo mwisho mpaka wanafika huko.

Kendrick, Torres, na Kevin waliwapokea wenzao, ikiwa inakaribia alfajiri kabisa sasa, naye Victor akaanza kuwasimulia jinsi mambo yalivyokuwa huko kwa mara nyingine tena. Akaeleza jinsi Lexi alivyofanikiwa kumkamata muuaji yule, na kwamba alikuwa ni mwanamke, lakini kwa sababu fulani isiyojulikana Lexi akamwachia akimbie, huku tayari akiwa ameiona sura yake. Kendrick alishangaa na kumuuliza Lexi, ambaye alikuwa ameegamia ukuta kwa njia legevu, aeleze ni sababu gani iliyomfanya afanye uzembe wa hali ya juu namna ile.

Mensah hata akaongeza kwa kusema kwamba alikuwa anamfyatulia risasi mtu yule lakini Lexi akamkinga ili zisimpate. Kendrick alijua Lexi asingefanya hayo bila kuwa na sababu kuu, hivyo akasisitiza Lexi ajieleze. Lexi alikuwa anatafuta namna ya kusema kile alichoona, lakini hisia zikamlemea na kusababisha aanze tu kulia. Alikuwa akijaribu kutoa maneno lakini yanazibwa kwa kilio cha chini kilichoonyesha uchungu mwingi, na hali hiyo iliwatatiza sana wengine. LaKeisha akasogea karibu yake na kuanza kumpangusa machozi kwa kujali, akimuuliza pia tatizo lilikuwa ni nini, naye Lexi akamwangalia Kendrick kwa huzuni na hatimaye kumwambia ukweli.

"Huyo mwanamke... uncle Kendrick... huyo mwanamke ni Azra!" Lexi akamwambia huku akilia.

Kendrick akabaki kushangaa. "Nini?!" akamuuliza.

"Azra? Nani Azra?" LaKeisha akauliza pia.

"Lexi unamaanisha nini?" Kendrick akamuuliza tena.

"I don't know... sielewi yaani... oh God!" Lexi akaongea na kuinamisha uso wake kwa huzuni.

"Boss... what is she talking about? (anaongelea nini?)" Mensah akamuuliza Kendrick.

Kendrick akashindwa ajibu nini. Hiki ni kitu ambacho hata yeye kilimchanganya sana. Akamsogelea Lexi karibu zaidi na kumshika mabegani.

"Lexi... unamaanisha kwamba... mtu aliyemuua Oscar... ni Azra?" Kendrick akauliza.

Lexi akatikisa kichwa kukubali.

Kendrick akachoka. "How is that possible? (hiyo inawezekanaje?)" akauliza.

"Jamani, si mgetuambia nini kinaendelea... hii show yote ya nini?" Kevin akauliza.

"Kevin, nakuomba uondoke hapa sasa hivi kabla sijageuka!" Kendrick akasema kwa hasira.

Kevin akashangaa. Alipomwangalia Torres, akamwonyesha kwa ishara ya kichwa kuwa aondoke, naye Kevin akatii na kuanza kuondoka. Lakini alijifanya tu kuondoka, kwa kuwa alipofika usawa wa kuta nyingine alijibanza na kutulia hapo ili ajue kilichoendelea.

"Lexi... una uhakika? Una... una uhakika kabisa na ulichokiona?" Kendrick akamuuliza.

"Ndiyo. Nimemwona usoni uncle. Ni yeye kabisa!" Lexi akamwambia.

"Boss, Azra ndiyo nani?" LaKeisha akauliza.

"Azra ni mdogo wake Lexi," Torres akasema.

LaKeisha akamwangalia kimaswali. Hata Victor na Mensah wakashangaa pia.

"Mdo...? That bitch is your sister?! (yule malaya ni dada kwako?)" LaKeisha akauliza akiwa haamini.

"LaKeisha!" Kendrick akamzuia kuongea vibaya.

"Kivipi? Si ulisema... familia yako na hata ya boss ziliuliwa na Weisiko na Jacob? Huyo Azra ni wa wapi?" akauliza Victor.

Lexi akakaa chini akihisi uchovu wa hali ya juu; siyo wa akili, siyo wa mwili. Kendrick akachuchumaa na kumtazama usoni.

"Lexi... tuliwaona. Mimi na wewe tuliwaona wote wakiwa... hii inawezekanaje?" Kendrick akauliza tena.

"Boss... hapa kuna mchezo umefanyika. Inawezekana hata huyo assassin amevaa tu sura inayofanana na mdogo wake Lexi. Tusiwe emotional sana, labda ndiyo kitu maadui zetu wanachotaka," akasema Victor.

"I agree (nakubali)," LaKeisha akasema.

"Hapana. Hapana, ilikuwa ni yeye. I know her. Najua ilikuwa ni yeye," akasema Lexi.

Kutokea pale Kevin alipokuwa amejibanza, alikuwa amesikia mambo yote yaliyosemwa, naye akatikisa kichwa chake kwa kukerwa sana, kisha akaondoka tu na kuelekea chumbani. Torres akasogea mpaka Lexi alipokaa na kumshika begani.

"Lexi... najua kuna vitu vingi sana unawaza. Lakini kwanza, unahitaji kurudisha uimara wako mwilini na akilini. Kuna jambo ninataka tuzungumze, wote kwa pamoja, na nitahitaji focus yako nzuri, kwa hiyo nakuomba ujitahidi kuiweka akili yako sawa kwa sababu kuna mambo mengi tunahitaji kufanya. Please..." Torres akasema kwa ustaarabu.

"Unahitaji tuongelee kuhusiana na Salim Khan?" akauliza Lakeisha.

"Ndiyo. Kutia ndani na Azra pia," Torres akasema na kumwangalia Lexi.

Lexi akamtazama kwa umakini, kisha akaanza kujinyanyua taratibu.

"Umepata nini kuhusu Azra?" Lexi akauliza.

"Unahitaji kupumzika kwanza Lexi. La sivyo sitakwambia lolote," Torres akasema.

"Ndiyo Lexi. Hapo najua una maumivu. Unahitaji kupumzika. Twende," LaKeisha akamwambia huku akimvuta taratibu.

Lexi akawa anaangaliana sana na Kendrick, ambaye alibaki kumwangalia tu kwa hisia mpaka LaKeisha alipofanikiwa kuondoka naye na kuelekea upande wa juu wa nyumba hiyo. Torres akamtazama tu Kendrick kwa ufupi, naye akamshika begani kama kumpa kitia moyo, kisha yeye pamoja na Victor na Mensah wakamwacha peke yake akiwa amesimama hapo mwenyewe. Akaanza kumkumbuka sana rafiki yake kipenzi, ambaye alipoteza maisha kikatili na kumwachia malezi ya mwanae huyu ambaye alikuwa akipitia mambo mengi magumu kihisia.

Kendrick akashusha pumzi kwa kufadhaika sana na kuuliza hivi, "Kwa nini mambo yanakuwa magumu namna hii kwa huyu mtoto, Casmir?"


★★★


Siku hii mpya ilipoendelea kupitisha muda, tayari baadhi ya mashirika ya serikali yalikuwa yamesafisha "uchafu" uliokuwa umebaki baada ya tukio lililompata Salim Khan. Kwa sababu ilionekana kwamba ni Mess Makers ndiyo walimuua mwanaume huyo, Raisi kupitia wawakilishi wake alitoa tamko kwamba kuanzia wakati huu, wangefanya msako wa hali ya juu kupita maelezo kwenye nchi yote ili kuwakamata hao watu. Yaani wananchi waliambiwa mapema kuwa wasishangae endapo maaskari au wanajeshi wangeingia kwenye nyumba zao kama migambo, kwa sababu msako huu sasa ungekuwa mkubwa kuliko mwanzoni. Lakini hii yote ilikuwa ni njia ya serikali ya kujikosha tu ili kuwapa watu matumaini bandia.

Raisi Paul Mdeme alikutana na wenzake waliobaki kwenye kundi lao siku hii huko Ikulu. Gavana wa Benki Kuu Laurent Gimbi alikuwa na mashaka kuhusu jambo lililompata Salim, naye aliuliza ikiwa Raisi alihusika katika kifo chake. Mdeme kama kawaida alikataa, akiwashawishi wengine wakubali kwamba ilikuwa ni Mess Makers, huku Jenerali Jacob na Luteni Jenerali Weisiko wakiwa wanaujua mkanda mzima.

Kwa hiyo sasa swali likabaki kuwa baada ya kifo cha Salim ni nini kingefuata, naye Mdeme akawaambia kwamba angetumia uchochezi wake ili kujiingiza katika sehemu ya mali ambayo Salim aliacha. Yaani, angeongea na baadhi ya watu au wanasheria wa Salim Khan waliosimamia miradi yake ndani na nje ya nchi, kwa njia ya kuwalaghai ili sehemu kubwa ya mali za Salim zitumike kumuunga mkono yeye na serikali yake tena.

Hii ilikuwa ni kwa sababu Mdeme alijua kuhusu mambo mengi haramu aliyofanya Salim na kumfichia kwa kipindi kirefu, kwa hiyo angeyatumia hayo kuwalaghai watu waliobaki kusimamia mali na miradi ya Salim. Hangeweza kufanya hivyo wakati Salim alipokuwa hai kwa kuwa jamaa pia alijua mambo mengi kumhusu Mdeme na alikuwa na nguvu sana, lakini kifo chake kilifanya nguvu hiyo ipungue kwa sababu wengine hawakujua kuhusu muungano wao.

Ingawa Makamu Eliya, Waziri Yustus na Gavana Laurent waliona hilo kuwa hatari, Jenerali Jacob na Weisiko wakamuunga mkono Raisi Mdeme na kuwashawishi wengine kufanya hivyo. Kihalisi, hiyo yote ilikuwa ni sehemu ya mpango wa Jenerali Jacob, ambao alimpatia Mdeme na kumfanya aridhike nao. Kwa hiyo baada ya wengine kumuunga mkono Raisi pia, sasa ambacho kingefuata ingekuwa ni utekelezaji tu.


★★


Kwa upande wa timu ya Luteni Michael, mambo hayakuwa mazuri sana kwake ijapokuwa kiujumla hayakuwa mabaya. Baada ya tukio la Salim Khan, alitafutwa na Kanali Oswald Deule kwa njia ya simu na kuambiwa aende kukutana naye kwenye jengo maalum la kijeshi, ambako ndiko ofisi za viongozi kama yeye zilikuwa. Luteni Michael alikwenda huko siku hii, na baada ya kukutana na Kanali Oswald, akaambiwa kwamba kuanzia sasa msako huu wa Mess Makers angeushughulikia yeye moja kwa moja. Yaani, uhuru aliokuwa amempatia tokea ACP Nora alipojiunga na msako huo sasa ungeondolewa, kwa hiyo kila jambo lingefanywa kwa mwelekezo wake moja kwa moja na si vinginevyo.

Hii ilimshangaza kiasi Luteni Michael, kwa sababu ilikuwa ni kama anaondolewa kwenye uongozi wa msako huu kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Kanali Oswald akamwambia hiyo ilikuwa ni kwa sababu kwa muda sasa Luteni Michael amekuwa hafanyi kazi aliyopewa na badala yake kuendekeza hisia za kijinga, yaani kumwelekea ACP Nora. Luteni Michael alishangazwa na ni jinsi gani Kanali Oswald angejua kuhusu hisia zake kwa Nora, lakini akamwambia kwamba hilo lilikuwa nje ya masuala ya kazi, na hajaliingiza popote kwenye msako wao muhimu.

Ndipo Kanali Oswald akamwambia anajua Luteni Michael alikuwa anapoteza tu muda wake kumfata ACP Nora na kupiga mwanamke mwingine ambaye ni rafiki tu, kwa sababu alikuwa anasumbuliwa na wivu wa kipuuzi. Akamwambia kama Jenerali Jacob angepata kujua kuhusu mambo aliyokuwa anafanya basi anafahamu ni jinsi gani hiyo ingemwathiri vibaya. Luteni Michael akaomba tu samahani kwa heshima, naye Kanali Oswald akamwambia hahitaji samahani yake bali utekelezaji wa kazi. Akamwonya kwa kusema ikiwa angepata tena taarifa kuhusu mambo hayo aliyoyaona kuwa ya kitoto, basi angemjulisha Jenerali Jacob ili amshughulikie yeye mwenyewe. Alimwambia ajitahidi kukaa mbali na ACP Nora, kwa sababu baba yake hakuwa mtu wa kucheza naye kabisa.

Luteni Michael hakuwa aina ya mwanaume wa kuogopa vitisho vya "nitakusema kwa baba" hata kidogo, lakini kwa sababu ya nidhamu yake ya kijeshi, akakubali ushauri wa Kanali na kumwambia makosa ya namna hiyo hayangejitokeza tena. Kwa hiyo baada ya hapo Kanali Oswald akamruhusu aondoke ili akawajulishe na wengine kuhusu "mabadiliko" hayo.

Luteni Michael alirejea kwa timu yake akiwa amekwazika kiasi. Siyo kwa sababu ya Kanali Oswald kumwambia angepaswa kujiweka chini kwenye msako huu, ila ni jinsi ambavyo watu walihukumu hisia zake. Kuanzia kwa Nora, baadhi ya vitu wanajeshi wa timu yake walivyomwambia, na hata maneno ya siku ile ya Lexi, yalimfanya ajiulize ikiwa labda kweli hakujua alipotakiwa kuwa. Lakini akajikaza tu kiume na kwenda kuwafikishia wengine taarifa mpya. Bobby, Alex, Mario na Hussein walishangaa kiasi, wakiuliza ikiwa hiyo ilimaanisha kwamba hangewaongoza tena, lakini akasema ni kwenye msako huu tu na si vinginevyo.

Akawaita Mario na Hussein pembeni baada ya hapo na kuwauliza ikiwa walimwambia yeyote kuhusiana na yaliyotokea kwenye chumba cha Nora siku ile, lakini wote wakakanusha. Akawauliza kwa mkazo iliwezekana vipi Kanali Oswald akajua kuhusu hilo, kwa sababu Nora hakuwa aina ya mwanamke ambaye angemwambia mwanaume yule. Mario alisema wazi kwamba hakuna yeyote aliyemwambia, naye Hussein akakataa pia. Lakini Hussein akawa ametambua kwamba huenda alifanya makosa makubwa, kwa sababu ni yeye ndiyo aliyesema kuhusu kilichotokea siku ile kwa Aliyah; mpenzi wake mpya. Akajiuliza ikiwa Aliyah alimwambia mtu mwingine, na kama alifanya hivyo basi mapenzi yote aliyomwonyesha usiku ule yalikuwa ni kwa ajili ya kumpeleleza.

Baada ya Luteni kuwaacha, Hussein alikwenda faragahani kuongea na Aliyah na kumwambia anajua ni yeye ndiye aliyefanya uchongezi. Alimwambia kwa njia ya moja kwa moja kama vile anajua kila kitu tayari, naye Aliyah akafunguka kwa kusema ni kweli; alimtaarifu Tariq kwa kuwa Kanali Oswald aliwaweka wampe taarifa zilizofichwa kwake. Kufikia wakati huu Aliyah alikuwa amempenda sana Hussein, hivyo akamwomba samahani na kuahidi hangemchongea tena. Hussein alikasirika na kumwambia asingeweza kuendelea naye tena kwa sababu uhusiano wao ulijengwa kwa uwongo, kwa hiyo kuanzia siku hii wangekuwa wamemalizana kimapenzi, na kubaki kuwa na uhusiano wa kikazi pekee.


★★


Kwa upande wake Nora, alikuwa ameamkia ofisini kwake kuendelea na uchunguzi wa hapa na pale kuhusiana na Lexi, Kevin Dass, pamoja na Oscar Amari. Alikuwa akijaribu kuunganisha mambo ambayo yangepatana kuhusiana na watatu hawa ili kubaini ikiwa Lexi alikuwa ni mmoja wao. Tokea walipoachana jana asubuhi na Lexi kusema alikwenda nje ya mkoa, Nora hakuwa amempata tena kila alipojaribu kumpigia.

Baada ya tukio lililotokea usiku wa jana kiukweli mashaka kumwelekea yaliongezeka, lakini bado Nora hakuwa amepata jambo lolote lenye kuongezea mashaka yake kumhusu "mwanamke" huyo. Kama tu jinsi ambavyo taarifa nyingi kuhusu maisha ya zamani ya Kevin Dass na Oscar Amari zilivyokuwa zimefichika, ilikuwa namna hiyo hiyo kumwelekea Lexi ingawa mengi ya maisha yake ya kawaida akiwa huku kwa wakati huu yalikuwa wazi.

Wakati akiendelea na tafiti za Mess Makers na Salim Khan pia, akapigiwa simu na Kanali Oswald Deule, ambaye alimtaarifu kwamba sasa taarifa zozote za kazi alizofanya angempatia yeye na siyo Luteni Michael. Nora akauliza sababu ya badiliko hilo, naye Kanali akamwambia ni ili wafanikiwe zaidi wakati huu kwa sababu ilionekana kama kazi imemlemea sana Luteni Michael. Jeshi la Nchi mpaka sasa halikuwa limepata matokeo mazuri, na Jeshi la Polisi nalo ndiyo kabisaa, kwa hiyo akasema kwamba yeye kuingia tena moja kwa moja kungebadili mambo.

Nora hakuwa na kipingamizi, naye akamwambia kufikia sasa bado hakuwa amepata jambo lolote jipya. Kanali Oswald akamwamuru afanye kazi kwa uharaka kwa sababu walikuwa wameshawadekeza hao Mess Makers vya kutosha, na sasa eti chini ya utawala wake hilo lingekwisha. Nora alimwona kuwa aina ya wale viongozi wanaojali sana sifa, kwa hiyo akampuuzia tu na kukata simu.

Wazo la kumuuliza Luteni Michael ni kwa nini mambo yalikuwa yamebadilika ghafla lilimwingia, lakini hakuona umuhimu wa kumtafuta mwanaume huyo hasa ukitegemea na jinsi hali ilivyokuwa mbaya baina yao. Alijua Michael alisema alitazamia wangeongea tena vizuri, lakini yeye Nora bado hakuwa tayari. Akaendelea tu kutulia ofisini kwake akiitazama moja kati ya picha za Lexi, akimtafakari sana mwanamke huyu aliyekuwa "ameuteka moyo wake."

Baadaye, alitoka na kuelekea kule Sea House. Wakati huu angekuwa peke yake, lakini ni kama kila kitu kuhusu sehemu hiyo kilimkumbusha mara zote alizokutana na Lexi. Akapata vinywaji, kisha akaenda mpaka ile sehemu ya fukwe ambayo Lexi alimwonyesha. Alikumbukia maongezi yao, alikumbukia kuhusu jinsi Lexi alivyoficha tattoo zake, na jinsi alivyombusu kwa mara ya kwanza kabisa wakiwa sehemu hiyo. Kuwaza kwamba huenda kila kitu kuhusu jinsi mahusiano yao ya kirafiki yalikuwa yamejengwa kwa uwongo kulimtatiza sana, naye akajikuta anakaa tu hapo kwa muda mrefu mno akitafakari vitu vingi.


★★


Upande wa Mess Makers. Siku hii ilikuwa imeanza kwa kikao kidogo cha kundi hili kilichoongozwa na Torres. Alikuwa anataka kuwaeleza mambo fulani kuhusiana na yaliyotokea siku ya jana, na angalau kwa wakati huu Lexi alikuwa ametulia zaidi kihisia baada ya kutumia muda fulani kupumzika.

Torres kama kawaida alianza kuyaorodhesha mambo kwa jinsi yalivyotokea mpaka Salim Khan kuuawa, naye akafikia mkataa kuwa huo ulikuwa ni mpango wa Jenerali Jacob bila shaka. Aliwaeleza kwamba kwa kumuua Salim, hii ingempa Raisi Mdeme nafasi ya kujiingiza kwenye mfumo wa mali alizoacha milionea huyo na hivyo kuiinua miradi ya serikali, lakini kwa sababu lawama ya kifo cha Salim ilielekezwa kwao, hii sasa ilimaanisha hata watu wa nje waliokuwa na ukaribu na mwanaume huyo wangeingizwa ili kuwasaka Mess Makers kwa njia tata zaidi, na hiyo ingeongeza hatari kwao zaidi ya ilivyokuwa mwanzo.

Kwa misingi hiyo, Torres akawaambia ingebidi waharakishe zaidi mpango wao wa mwanzo, mpango uliofanya waibe zile trilioni 20, kwa sababu muda usingekuwa rafiki kwao na ingefika tu siku ambayo sehemu yao ya maficho ingejulikana. Walitakiwa kuharakisha mpango wao ili isiwafikie wakiwa hawajaukamilisha.

Baada ya wote kuonyesha wamemwelewa, sasa Torres akaanza kuzungumzia kuhusiana na helicopter ile iliyofika kule juu ya ghorofa usiku wa jana na kutokomea. Aliwajulisha kuwa alifanya uchunguzi na kubaini kwamba Salim Khan hakuwa na nia ya kuondoka kwa gari tena. Alikuwa ameagiza helicopter ifike pale ili akimaliza mahojiano apande kuelekea juu na kuingia, kisha ndiyo aondoke; kimtindo yaani. Lakini helicopter ambayo ilifika haikuwa ile iliyotakiwa kwenda hapo, kwa sababu ilifika dakika 30 kabla ya muda hususa ambao ile halisi ilitakiwa kufika.

Bila shaka helicopter hii ndiyo iliyomshusha mwanamke yule ambaye Lexi alimtambua kuwa Azra, naye Torres akawaambia baada ya kuifatilia na kujua ilikotokea, alitambua ni nani aliyeiendesha, mwanaume aliyeitwa Khalid Juma, ambaye ni mmoja wa wanajeshi maalumu wa vikosi vilivyoongozwa na Luteni Jenerali Weisiko. 

Akasema inaonekana Azra alipotoka kwenye jengo lile na kuelekea kwenye ule uwanja, hiyo helicopter ilitakiwa kuwa hapo ikimsubiria, lakini kwa sababu Torres alikuwa ametumia njia za kiteknolojia kupata taarifa hizo, aliyeiongoza helicopter hiyo alitambua hilo, na hivyo akaona asirudi nyuma kwa kuwa alihofia labda ni vyombo vya usalama ndiyo vilikuwa viki-hack mifumo yake. Kokote Khalid alikoipeleka helicopter baada ya hapo Torres hakuweza kuifatilia tena, na huenda hiyo ilimaanisha waliiharibu mifumo yake au labda helicopter nzima kama tu Lexi alivyokuwa ametabiri.

Kwa hiyo, kilichokuwepo sasa ilikuwa ni kumkamata mwanaume huyo wa kijeshi, Khalid Juma, ili awaambie ni nani aliyempa amri ya kuiongoza helicopter ile kumpeleka Azra mpaka jengoni pale kufanya mauaji, na huenda taarifa ambazo wangezipata zingewasaidia kumkamata Azra. Lexi akakubaliana na hilo upesi na kusema wangepaswa kuanza kulishughulikia haraka, lakini Kevin akawaambia wote kwamba haikujalisha muuaji huyo alikuwa ni nani, walipaswa kumlipizia kisasi Oscar kwa sababu aliuliwa kikatili kupitia mtu huyo. Hawakupaswa kumfata ili kumkamata, bali kumuua. Kevin hakuelewa uzito wa kile alichokuwa anasema, kwa sababu alipenda sana kutanguliza maoni ya kibinafsi, na ingawa ilionekana hoja zake zina usahihi, hicho ni kitu ambacho hata yeye mwenyewe alijua kingepingwa tu.

Lexi akamuuliza Kevin vipi ikiwa angegundua kwamba muuaji wa rafiki yake ni dada yake wa damu, angefanya nini? Kwa kiburi Kevin akajibu kwamba angemuua tu. Lexi akamsikitikia sana, naye akamwambia alikuwa amepanga kumtumia na yeye kwenye mishe hii ya kumkamata Azra, lakini kwa sababu ya jibu lake lisilo la akili, angeendelea kubaki huko huko "chini." Kevin akaudhika sana, lakini hakuwa na njia ya kuweka kipingamizi. Lexi akamwambia Torres ampe maelezo kuhusu huyo Khalid Juma, na baada ya Torres kumweleza mambo machache kumhusu mwanajeshi huyo, Lexi akasema angekwenda leo leo kumfata; yeye pamoja na Victor na Lakeisha pekee.

Torres angetakiwa kubaki huko "chini" ili Lexi akifanikiwa kumpata mwanaume huyo na kumnyonya ukweli basi ampe taarifa (Torres) ili wapange njia nzuri ya kumkamata Azra. Kendrick akakubaliana na mawazo hayo, naye akasema kuna mambo anahitaji kuendelea kupangilia kwenye zile kampuni zake, hivyo angeondoka pamoja na Mensah kuelekea Geita kwanza. Kwa hiyo kwenye maficho yao wangebaki Torres na Kevin mkalia ndoo.

Hivyo bila kuchelewa, Lexi, LaKeisha na Victor wakaondoka hapo na kurudi Dar kumsaka Khalid Juma, ili hatimaye waweze kumpata Azra.


★★★★★★★★★★

 ITAENDELEA

★★★★★★★★★★

Previoua Next