Mwisho wa Dunia Kimya Kimya – Episode ya Kumi na Tano
Mhusika Mkuu: Najim Kifu
---
Kabla hajajibu chochote kwa Ayubu, Najim alihisi ardhi ikizidi kuwa baridi — si kwa hali ya hewa, bali kwa hofu ya moyoni. Macho ya Ayubu hayakuwa ya kawaida, yalikuwa yanang'aa kwa kivuli, kama vile yanatazama mema na kuyapinga kimyakimya.
Khadija akamsogelea Najim kwa tahadhari, “Huyu… si mtu. Ni chembe yako ya kivuli. Ayubu ni wewe usiyekubali kuumia tena. Ukimpinga, utajeruhi moyo wako mwenyewe.”
Najim alimtazama Ayubu kwa makini. “Wewe si kaka yangu. Wewe ni chaguo niliokataa.”
Ayubu akacheka kimya kimya. “Lakini mimi ndiye aliyekuokoa Mogadishu. Mimi ndiye aliyekufanya umsahau Layna kwa miaka mitano. Mimi ndiye uliyemruhusu akupende Khadija — wakati moyo wako ulikuwa bado umefungwa.”
Kimya.
Najim akanyosha mkono wake. “Sitaki mapenzi yaliyopitia njia zako. Sitaki uhai unaokimbia hisia. Niko tayari kuumia — kwa sababu ndicho kinachonifanya kuwa binadamu.”
Ayubu akamtazama, akauliza: “Na kama Layna akiamka na akupende tena — kisha usimtambue?”
Najim akasogea karibu, hadi pua zao zikatishana pumzi. “Nitampenda tena, hata nisipomkumbuka. Kwa mara ya pili. Na ya tatu. Na hata ya mia.”
Ghafa Ayubu akasogea nyuma. Macho yake yakabadilika. Uso wake ukaanza kupasuka kwa mwanga.
Akasema kwa sauti ya mchanganyiko wa huzuni na matumaini:
> “Basi nitapotea, lakini nitaacha alama. Ukinisahau kabisa, hutajua umefika.”
Kisha Ayubu akatoweka. Kulia kwake, kulibaki kipande kingine cha Layna — sauti. Ilikuwa imefungwa kwenye kisanduku cha mawe ya anga, ambacho kilikuwa kinazunguka kimya hewani.
Najim alikipokea. Kisanduku kilipoguswa, sauti ya Layna ikatoka:
> “Najimu... ulikuwa sababu ya mimi kuamini tena. Lakini nilikuchukia pia. Uliniacha. Uliondoka.”
Najim akashika kisanduku kwa mikono yote miwili, kama kinara wa taa. Akasema kwa sauti ya taratibu:
> “Niliogopa… lakini sasa, nakurudia nikijua hofu haiwezi tena kuniongoza.”
Ghafla, mwanga mkali ukatoka chini yao — mlango wa sehemu ya tatu ya roho ya Layna ulifunguka.
Wakaporomoka kwenye giza refu, kisha wakatua mahali pa ajabu.
Ilionekana kama Zanzibar, lakini ya kale — visiwa vilivyowekwa juu ya maji ya taa. Jua lilikuwa la buluu. Anga lilijaa ndege waliotengenezwa kwa barua zisizowahi kufikishwa.
Khadija akatabasamu. “Hii ni ndoto ya Layna kuhusu ndoa yenu, Najim.”
Najim akamgeukia. “Na wewe?”
Khadija akajibu kwa huzuni. “Mimi nilikuwepo kwenye ndoto yake kama mtu wa kukusindikiza tu.”
Katika kivuli cha mnara wa taa, msichana mmoja akawa amekaa — akiwa na sura ya Layna, lakini mdogo zaidi. Alikuwa na macho ya majonzi ya miaka mingi, lakini bado na nuru ya msamaha.
Najim akasogea.
Msichana yule akasema:
> “Najim… kama unataka kuniunganisha, lazima univunje kwanza. Huwezi kuokoa moyo uliovunjika bila kuuvunja vizuri tena.”
Najim akasimama kimya.
Khadija akauliza, “Na ukishamvunja, je? Atakubali kukusamehe?”
Msichana akasema:
> “Atanisamehe… kama kweli alikuja kwa mapenzi. Kama alikuja kwa hatia, hatanisamehe kamwe.”
Najim akapiga magoti. “Nimekuja kwa sababu siwezi kuendelea bila wewe. Sitaki kukumbuka tu, nataka kufufua.”
Kisha, kwa mikono miwili, akaweka kisanduku cha sauti juu ya kiganja cha msichana.
Mwanga ulianza kulipuka taratibu. Sauti ya Layna ikaanza kurudi taratibu taratibu… kisha msichana yule akaanguka kama majivu, na ndani yake kulibaki lulu ya bluu — ishara ya sehemu ya tatu ya Layna: Imani.
Waliipokea.
Khadija akasema kwa sauti ya wazi, “Sasa zimebaki nne. Tuko nusu.”
Mara ghafla, waliposimama, kulisikika sauti ya kike yenye ukakamavu:
> “Najim Kifu! Safari yako imevuruga mizani ya wakati. Kwa jina la Kitengo cha Kwanza cha Ulinzi wa Muda, unakamatwa!”
Walimgeukia.
Akasimama mbele yao mwanamke mrefu, mwenye sare ya chuma nyeusi. Aliitwa Nurath — kamanda wa Jeshi la Saa ya Mwisho.
---
Comments