Majira ya asubuhi tulivu kabisa iliyo pambwa na ukungu na nuru iliyoanza kuangaza taratibu katika kijiji fulani kinacho onesha kuwa ni kijiji cha wafugaji wengi na wakulima kiasi, hii ni kutokana na kuwa baadhi ya mifugo ilikuwa ikirandaranda asubuhi hii. Walionekana baadhi ya mbuzi, kondoo, mbwa na baadhi ya ndama pamoja na kuku walio wengi. Ukiachana na mifugo, pia wanafunzi walionekana wakielekea shuleni, pia baadhi ya wanakijiji wengine walionekana wakielekea kwenye shughuli zao za kila siku hasa wakulima.
Kijiji hiki sio kijiji masikini kabisa, muonekano mzuri wa makazi (nyumba), lunch kubwa, mashamba makubwa ya mpunga na mto wa asili, ni vitu ambavyo vilificha umaskini wa kijiji hicho.
Katika nyumba mojawapo iliyopo pembezoni kidogo mwa barabara ya mtaa, anaonekana mzee mweupe makadirio ya miaka 50-55, alikuwa na ndevu nyingi na nywele nyingi zilizo changanyikana na mvi za kutosha. Alikuwa na sura kama ya kipemba. Alivalia kaptula la rangi ya kijani iliyokolea aina ya Timberland na jacket jeusi, pia alivalia rainboot zilizo katwa kwa juu kupunguza urefu wake. Asubuhi hii anaonekana akigonga gonga kwenye kibanda cha mbao kilichopo pembezoni kidogo mwa nyumba yake. Pia alikuwa na gongo la kutembelea aliloshikilia upande wake wa kushoto, ilionekana dhahiri katika mguu wake wa kushoto haukuwa na utimamu, alionekana kuchechemea.
Suleiman Seif ndio jina lake, lakini watu wa kijijini hapo walimzoea kwa jina la mzee Sele mpole. Haiba yake ni mpole, yaani ule upole wa kuboa! Alikuwa na kauli za utata na za busara, na hakuwa mtu wa kuchanganyika ovyo na watu.
Akiwa anagonga gonga mbao kwenye kibanda chake, mara ni kama amekumbuka kitu na palepale akaangalia saa yake ya mkononi, kisha akatoa simu ndogo ya batani kutoka kwenye kaptula yake, akaangalia kitu kisha akairudisha tena mfukoni, alafu akaangalia upande uliopo mlango mkubwa wa nyumba yake. Akaanza kuita;.
"Nadir......Nadir.. bado umel..". Kabla hajamaliza kuongea akatokea kijana mrefu mweupe mwenye nywele kama za kizungu, makadirio ya umri wa miaka 17. Akiwa amevalia sare za shule, suruali ya bluu (kitambaa), shati jeupe lenye mikono mirefu, mgongoni alibeba begi dogo jeusi, miguuni alivaa viatu vyeusi vya ngozi vinavyo ng'aa kama sio kumeremeta!
"Aaaah nikajua bado umelala, nimeangalia saa nikaona ni saa moja na dakika tatu, nikahisi labda leo ni wikiendi.., lakini nikaangalia kalenda nikagundua leo ni Ijumaa ....,, Mbona umechelewa sana leo?"
"Ndio leo ni Ijumaa, nimechelewa tu kuamka, na hakuna kitu usicho kijua pindi nichelewapo kuamka... Sidhani kama inapaswa uniulize ankoo....! Alijibu akiwa na uso mkavu!
"Nadir! Kwa sasa mimi sio jibu sahihi la mafikirio yako! Mazingira ndio yatahusika kwa kila kitu... Mimi nasimama kwenye njia ambayo napaswa kusimama."
"Hata hivyo nishazoea maneno yako anko,siku zote haujawahi kuwa muwazi kuhusu asili yangu, ingawa unadai wewe ni mjomba lakini unanificha kutoitambua asili yangu..., Ok sitolizungumzia suala hili tena! Na usijali kuhusu mimi". Baada ya kuongea hivo, Nadir aligeuka na kuanza kuondoka taratibu kuelekea shule. Huku nyuma mjomba wake alikuwa akimwangalia kwa sura ya masikitiko kiasi,akimuacha Nadir akikata mitaa kuelekea shule na yeye kushikilia vizuri gongo lake na kuendelea kutengeneza banda lake.
Muda mfupi kidogo, Nadir alifika kwenye barabara kuu, upande wake wa kulia umbali wa kama hatua tano kutoka alipo, kulikuwa na bango lililoandikwa "BR SAMARA KATI" likielekeza barabara ya kuelekea mtaa anakoishi Nadir na anko wake.
'SAMARA' ndio kijiji alichokuwa anaishi Nadir na anko wake, katika mtaa wa 'SAMARA KATI'.
Nadir alifika shule akiwa amechelewa. Baada ya kujieleza kidogo kwa mwalimu wa zamu, aliruhusiwa kwenda kujiunga na wenzake ili kuanza masomo ya siku hiyo. Ilipotimu saa nne muda wa break ndogo, wanafunzi walitawanyika kukiendea kifungua kinywa. Nadir hakutoka darasani, ila baada ya muda kidogo aliletewa taarifa kuwa anahitajika ofisini kwa sir John ambaye ni mwalimu wake wa darasa. Hakuonesha mabadiliko yoyote, ila tu alinyanyuka na kuanza kuelekea ilipo ofisi ya mwalimu huyo. Baada ya kufika hakumkuta sir John pekeake ila pia alikuwepo na mjombaake yaani anko Sele.
"Nadir Sporah! Usahaulifu wako unasababisha kumtesa mzee wa watu mwenye matatizo ya miguu kiasi cha kukuletea kifungua kinywa hadi shuleni kweli?....., mbona unakosa huruma kiasi hicho....?
"Aaaah usimlaumu bure Nadir ni kwamba tu alisahau kubeba, hata hivyo imekuwa ni fursa kwangu kufanya mazoezi kidogo ya kunyoosha viungo" alijibu anko Sele kwa bashasha.
"Hapana mzee ungemuacha tu na wala usingehangaika hadi kumletea chakula shuleni, anazoea huyu maana hii sio mara ya kwanza wala ya pili, mara kadhaa ulimletea chakula kwa visingizio vyake vya kusahau... Anatakiwa akuheshimu sana hajui kama wewe ni mzazi wake. Hapo alipo hamjui babaake mzazi wala mamaake, Shuleni kwenyewe anatumia jina la mamaake na hamjui ni naa........ Aaaghhh!! Kabla hajamaliza kuongea, sir John alihisi kukabwa shingo kwa nguvu na nguvu isiyo onekana. Wakati huo Mzee Sele mpole alikuwa na tabasamu lake tu kawaida huku Nadir akionesha kushangazwa na ukelele wa sir John akitapatapa bila hata kuguswa na mtu. Jicho lilimtoka!
Comments