SONGA NAYO................
Alisimama na kujibanza kwenye mti baada ya kuona jambo la kutisha mbele kidogo kutoka pale ambapo alikuwepo. Mwanaume ambaye kwenye mwili wake alivalia koti refu la rangi ya ugoro, suruali ya jeans ambayo ilifanania na koti lake pamoja na buti kubwa ambalo ni maarufu kama American boot huku uso wake ukiwa umefunikwa kwa kitambaa chenye rangi ya ugoro na kichwani akiwa na kofia aina ya NY ndiye ambaye alikuwa anayafanya matukio hayo ndani ya huo msitu. Kusita kwake ni kwa sababu alimuona mtu huyo akiwa anaufanya ukatili kwa wenzake.
Bwana yule alikuwa anatembea kama mashine, miguu yake ilikuwa myepesi isivyokuwa kawaida lakini spidi yake ndiyo ambayo ilikuwa inatishia usalama wao. Alijigeuza kwenye mti ambapo alipishana na risasi ambayo ilitua hapo, alijitokeza kwa kujiviringisha chini lakini wakati anajitokeza ni shilingi ambayo ilikuwa inaongea lugha moja na mkono wake, shilingi hiyo ilitua kwenye jicho la mwanajeshi mmoja ambaye alianza kupiga makelele bila utaratibu huku silaha yake ikiwa inarusha risasi hovyo kila mahali. Mwanaume huyo alijinyanyua pale chini kama mzimu na kutua pembeni kidogo mwa yule mwanaeshi aliyekuwa na shilingi kwenye jicho lake.
Alizikutanisha ngumi zake mbili kwenye shingo ya mwanajeshi yule, alitulia na kushuka chini taratibu lakini alitumiwa kama ngao kwani mwanaume huyo alimrusha kwa viganja vyake vya mkono kwa nguvu na kwenda kumzoa mwenzake mmoja wakadondokea mbali. Yeye hakuwa na muda wa kupoteza, alitembea kama mzimu kiasi kwamba hata wapiga risasi hawakuelewa wapige wapi kwani alikuwa anawachanganya kiasi kwamba kama wangekurupuka basi wangejikuta wanaanza kuuana wao wenyewe kwa wenyewe. Mwanaume huyo aliruka sarakasi za haraka haraka na kudunda kwenye mti mmoja, alitua chini kwa kutumia goti lake moja ambapo wakati anatua alikuwa ameichomoa bastola kwenye buti lake, risasi zilipigwa kwa muda mfupi mno ambazo zilitua kwenye kichwa cha mwanajeshi mmoja. Alikufa pale pale na wakati wanaangalia risasi zilipo tokea ili waweze kumshambulia, hakuwepo lile eneo, alikuwa ametoweka. Yule mwanajeshi ambaye alikuwa ni mwanamke alikuwa akiyashuhudia yote hayo akiwa haamini huku akiwa amejibanza kwenye mti.
Licha ya kuangalia kwa umakini ila hakuelewa mwanaume huyo alipotelea wapi, ni muda mfupi tu alishuhudia mwenzake akipigwa risasi nyingi za kichwa. Jambo ambalo alilifanya ni kuhamisha uso wake kumwangalia mwenzake ambaye mpaka wakati huo alikuwa amekufa, wakati anayarudisha macho yake mahali ambapo yule mwanaume alikuwepo, hapakuwa na mtu, ni miti tu na nyasi zilikuwa zikimwangalia na kumzomea. Lilikuwa jambo la ajabu kwake kiasi kwamba alijikuta ana muda mchache wa kuweza kuyapata majibu ya maswali mengi na sio maswali tu bali maswali ambayo yalikuwa ni magumu kwake.
Swali la kwanza ni kwamba, alikuwa ana uhakika kuwa ni huyo mtu ndiye ambaye alimpitia na kuiharibu hiyo simu, kama ni hivyo maana yake alikuwa ana nafasi ya kumuua, sasa kwanini alimuacha hai tofauti na wenzake ambao alikuwa anawaua kikatili? Alijikuta anapoteza ile nafasi ya kujiamini kwenye moyo wake, alijihisi yupo mikononi mwa ibilisi na hakuwa na msaada kwani huenda alishamkana Mungu kwenye maisha yake sasa msaada huo angeupatia wapi na ameshaingia kwenye mikono ya baradhuli shetani? Akiwa anazidi kujipa presha kubwa ya kumfanya atokwe na jasho jingi kwenye msitu ambao ulikuwa na baridi ya kutosha ndipo likaibuka swali la pili kwenye kichwa chake.
Huyo mwanaume alikuwa ni nani? Ni swali ambalo hakulipa muda mrefu kwenye akili yake kwani hakuwa na huo uwezo wa kuweza kulijibu hivyo akajikuta anahamia kwenye swali namba tatu ambalo huenda ndilo lilikuwa mhimu zaidi kuliko yote kwa wakati huo. Ni kwanini huyo mwanaume alikuwa anawaua watu hao, na sio kuwaua tu kwanini alikuwa anawaua kikatili namna hiyo mithili ya mtu ambaye alikuwa na uhasama nao mkubwa? Hilo swali hata hakupewa muda wa kutosha wa kuweza kulitafakari kwa sababu alishtushwa na sauti ya mlio wa kitu, hakikuwa kitu bali kichwa cha mtu kikiwa kinapasuka baada ya kubamizwa kwenye mti kisha buti likatua kwenye kichwa hicho. Yule mwanamke hakuvumilia kushuhudia tukio lile, alijikuta anayafumba macho yake huku chozi likimtoka.
Mwanaume yule alikuwa ni miongoni mwa binadamu wachache ambao walikufa kikatili yeye binafsi kuwahi kuwashuhudia. Hakuelewa yule mwanaume alitokea wapi bali alimuona tu wakati anamzoa mwenzake kwa miguu yake miwili ambayo aliipitisha shingoni na kumrushia hewani bila shaka alikuwa anaichanganya akili yake. Wakati mwanajeshi yule anashuka chini akiwa anaomba msaada ndipo alikutana na bwana yule ambaye alimdaka kwa nguvu kwa mikono yake na kumtua kwenye goti lake, uti wa mgongo ulikuwa haufai mpaka muda huo na ndipo hapo alipomrushia kwa nguvu kwenye mti kisha akafuatisha buti lake ambalo lilikipasua kichwa kama vile kondomu ilijazwa maji halafu ikatupwa chini.
Zile kelele ziliwaleta wenzake ambao walikuwa wamebaki wawili tu pekee, aliyekuwa mbele alikuja kwa kasi bila mahesabu wala kumuona mhusika wao. Ile kasi yake ilimfanya aanze kutembea kwa kusita sita, sio kwamba alipenda bali shilingi ilipitishwa kwenye koo lake ikatokea nyuma na kwenda kukita kwenye mti. Ile kusita sita kutembea ni kwa sababu alikuwa ameshikilia koo lake akiwa anahangaika huku hawezi hata kutoa sauti ya kuweza kuhitaji msaada ndani ya eneo hilo. Mwanaume yule alikuwa amemfikia ambapo aliizungusha shingo yake kama ananyonga jogoo la pasaka na ni wakati ambao hata yule kiongozi wao alikuwa amefika hapo.
Alipokelewa kwa mtama mzito ambao almanusura umfanye sura yake idondokee kwenye jiwe kubwa lakini alitanguliza mkono ambapo alijivuta na kujigeuza kwa sarakasi safi lakini silaha ilikuwa imedondokea upande mwingine hivyo alichomoa kisu kwenye kiuno chake na kukielekezea kwa mwanaume yule ambaye hakuonekana kumchukulia kwa uzito. Aliangalia pembeni na kupigwa na butwaa kwa namna miili ya vijana wake ilivyokuwa imezagaa pale chini, hakuweza kukubaliana na jambo hilo hivyo alipata hasira kali ambayo ilimfanya kujiinua kwa ngumu na kujipinda kwa sarakasi ambayo iliutanguliza mguu mmoja, ulimkosa mwanaume yule na mguu wa pili ukawa unakuja shingoni lakini nao alifanikiwa kuukwepa hivyo mkono ukawa unafanya kazi kubwa baada ya kujipinda na kurusha kisu chake.
Mkono wenye kisu ulikutana na bega la mwanaume yule kiasi kwamba akarudi nyuma kidogo, aliyainua macho yake ila awamu hii ni yeye ambaye alichelewa hivyo alikutana na ngumi ya kwenye taya ambayo ilimfanya kudondosha meno mawili chini aliyo yatema kwa ghadhabu. Alirusha mkono wenye kisu lakini alitumia hasira zaidi ya akili, mkono ulidakwa na kugeuzwa kwa nguvu kiasi kwamba ulivunjwa bila huruma, kisu kilimponyoka kikawa kimetua kwenye mikono ya mwanaume huyo ambacho alikitumia kumkita mwanajeshi huyo kwenye moyo wake kwa nguvu mpaka pale alipohakikisha amekichana chana kifua chake ndipo alikizamisha kisu hicho kwenye koo la mwanajeshi huyo na kumtupa akiwa ni maiti tayari. Wakati analitekeleza tukio hilo alikuwa anaaangalia pale ambapo mwanajeshi yule wa kike alikuwa amejibanza, bila shaka alijua kabisa kwamba mtu huyo alikuwa anajua kwamba yeye amejificha pale.
Hali ya kuangaliwa na muuaji yule ilizidi kumharibu akili yake, alikuwa hawezi kufanya jambo lolote kwa ambayo alioyaona pale hata silaha yake hakuwa nayo muda huo. Ni hofu ndiyo ambayo ilikuwa imeiteka sehemu kubwa ya moyo wake na asingeweza kufanya jambo lolote lile. Mwanaume yule alivua kile kitambaa chake usoni ili kumuonyesha sura yake halisi mwanamke yule. Asalaleee! Alikuwa ni yule mwanaume ambaye muda mchache uliokuwa umepita alitoka kumshuhudia akichomwa moto na kuuawa kwa petroli ndani ya ile nyumba, sasa kivipi tena awe hai? Alichanganyikiwa.
Alijikuta anatetemeka mpaka akadondoka chini akiwa ameishiwa nguvu kabisa, kivipi mtu ambaye alitoka kuuawa muda mfupi uliopita aonekane tena akiwa mwenye afya njema kabisa? Ulikuwa ni mzimu wake au walikuwa mapacha? Hilo jambo alilipinga kwa sababu mtu huyo hakuwa na ndugu hata mmoja hapa duniani na aliyekuwa hai ni yeye tu, sasa huyo alikuwa ni nani? Kupiga kwake magoti kulikuwa na sababu kubwa mbili, sababu ya kwanza ni kuchanganyikiwa kuhusu mtu yule lakini sababu ya pili alikuwa anajua sheria za wauaji, hata kama alikuwa na mpango wa kukuacha hai ila ukifanya kosa la kuiona sura yake tu basi ni lazima akuue. Alikuwa na uhakika kwamba mtu yule asingeweza kumuacha hai na kwa yale ambayo alimshuhudia akiyafanya! Hakutaka hata kuhangaika kuweza kupambana naye alijua ni lazima afe.
Mwanaume yule alimsogelea mwanamke yule mpaka pale jirani ambapo alikuwa amepiga magoti akiwa analia, alimwangalia kwa umakini sura yake na kuhakiki kama alikuwa amemuona vizuri usoni.
"Binti kama wewe hautakiwi kuwepo maeneo kama haya, sio salama kwa maisha yako. Ni jambo la hatari kubwa nchi hii ikianza kuwapoteza warembo wa aina yako kwa uzembe wa watu wachache. Naenda kuua wenzako wote ambao wamebaki kwenye ile nyumba ila wewe nitakuacha hai, nakuacha hai kwa sababu moja tu, wewe hautakiwi kufa kwa sasa ila zingatia hiki ambacho naenda kukwambia hapa "Watu ambao wamekutuma wewe na wenzako bila shaka wametumiwa video na picha na kuambiwa kwamba nimekufa hivyo mimi ni mfu kwako pia, hatakiwi kujua binadamu yeyote hata kwenye maisha ya huko baadae kwamba mimi bado nipo hai, kama ikitokea hivyo basi nitakuja kukutafuta kwenye maisha yako na kuua kizazi chako na familia yako yote kiasi kwamba jina la familia yako litafutika kana kwamba halikuwahi kutokea hapa duniani" Mwanajeshi yule akiwa anahitaji kuuliza angalau swali moja tu pekee kujua ni sababu zipi ambazo zilifanya yeye asiweze kuuliwa kwa wakati huo, alipokea kofi kali ambalo lilimtoa damu puani na kufanya shavu lake kuwa jekundu ghafla. Akiwa hajakaa sawa alikutana na mguu ambao ulikomaa kwenye tumbo lake, alinyanyuliwa na kupigwa na kiganja kwenye kifua chake kiasi kwamba alitapika damu nyingi kwenye mdomo wake. Alianza kuelemewa na ndipo mwanaume huyo alipopipitisha vidole vyake viwili kwenye shingo ya huyo mwanamke aliyepoteza fahamu hapo hapo.
Alimtupia chini na kumwangalia kwa umakini kwenye pua yake, bado alikuwa anahema kwa mbali hivyo alikuwa hai. Kufanya hivyo ilikuwa ni kumsaidia mwanajeshi huyo kwani kama ingetokea akakutwa akiwa hai na wenzake wote wameuawa kikatili basi lazima ingemletea shida kwa kutengeneza maswali kwa wapelelezi kwamba ni kwanini wenzake wote walikufa ila ni yeye pekee ndiye alipona? Kama angekutwa akiwa mzima kabisa basi lazima angekuwa mshukiwa wa kwanza ila kupigwa namna hiyo hata kama angezinduka bado asingekuwa kwenye hali nzuri hivyo hata kama angeomba msaada basi naye angechukuliwa kama mhanga ambaye huenda muuaji kwa bahati mbaya alisahau kuweza kumuua hivyo hakuna mtu ambaye angekuja kuwa na mashaka naye. Baada ya kuhakikisha amelimaliza jambo hilo, mwanaume huyo alitoweka taratibu akipotelea kwenye ile nyumba ambako kulikuwa na wanajeshi kadhaa ambao walikuwa majeruhi na wasingeweza kutembea kwa kuumizwa vibaya.
Sehemu ya pili inafika mwisho hapa, panapo majaaliwa tukutane ndani ya sehemu ya tatu kuweza kujua safari ya huyu muuaji mpya msituni.
FEBIANI BABUYA.
Comments