Reader Settings

 

Zilipita dakika 15 Jamal akiwa amelala chini ya sakafu alikurupuka baada ya kusikia milio ya viatu ya watu walio onekana wazi walikuwa wanakuja ndani ya hicho chumba ambacho yeye aliluwepo. Ni kweli baada ya kusimama tu waliingia wanaume waliokuwa wamevalia suti nyeusi na viatu vyeusi, walikuwa wapo wawili tu.

"Jiandae tuondoke" sauti nzito yenye bezi ya yule mmoja ilimshtua kwenye mshangao aliokuwa nao akiwaangalia hao watu waliokuwa wageni kwake, alikuwa anasita sana ila aliamua kufuata maneno ya baba yake ambaye alimwambia hao watu ni sawa na anavyo muona baba yake awasikilize kwa umakini mkubwa ndio watakao msaidia kwa sasa. Alitaka kutoka humo ndani kwa sababu hakuwa na cha kujiandaa alizuiwa na mkono wa mwanaume mmoja akamrushia suti mpya, Jamal hakuwa mtu wa hizo nguo hata ufungaji wa tai tu kwake ulikuwa mtihani basi alivaa suruari shati na koti lake pamoja na viatu tai akaitupia pembeni. Hakuelewa kilicho endelea alishtuka dakika 10 baadae wakiwa wanaelekea sehemu ambayo hakuijua kwani juzi tu tena usiku ndo alikuwa amekanyaga kwenye ardhi ya Mzizima kwa mara ya kwanza. Muda wa kutoka mle ndani alipigwa na ngumi nzito ya shingo iliyo mzimisha kwa sababu hakutakiwa kujua ni wapi alikuwa ikiwa ni njia za kumlinda mkuu wa majeshi ya nchi ya Tanzania, wakati huo walikuwa wamepita Tazara wakiutafuta uwanja mkubwa nchini wa Mwalimu Nyerere ( JNIA).

 

Walifika salama wakaonyesha vitambulisho walipigiwa saluti muda wote Jamal alikuwa anashangaa mambo yalikuwa yanaenda kwa kasi mno kiasi kwamba yalikuwa yanaizidi akili yake uelewa, baada ya kuangalia juu kabisa ya uwanja huo ndipo alipo yaona maandishi makubwa kabisa JULIUS NYERERE INTERNATIONAL AIRPORT, akakumbuka maelekezo ya mkuu wa majeshi alimwambia inatakiwa asafiri kwenda Cuba basi akili yake ilimwambia safari ilikuwa imeshaanza. Walipita salama na kwenda kwenye ndege moja kwa moja aliingia kama mtu maalumu hivyo hakukaguliwa wala kukaa kusubiri, alienda moja kwa moja mpaka ndani ya ndege alibahatika kupata siti ya dirishani. Tofauti na mawazo yake yalivyokuwa alidhani wale wanaume wawili anaenda nao ila baada ya kuhakikisha amepata siti na amekaa na wakati huo abiria wengine walikuwa wameshaanza kuingia wanaume hao walianza kuondoka ambapo mmoja aligeuka na kumpa maelekezo ya mwisho.

 

"Ukifika mwisho wa safari yako nenda mapokezi kuna mtu utamuona ameshika bango lenye jina lako la Jamal Hauston mfuate huyo ndiye mwenyeji wako, uwe na safari njema" hakuwa na muda wa kuruhusu maswali mengi sana aliondoka bila kuruhusu Jamal kuuliza chochote, kijana mdogo alikuwa anaiacha ardhi ya nchi yake kwa mara ya kwanza kwenda nchi za watu huko mbali na alikuwa ameridhia kuwa tayari kwa chochote kitakacho tokea baada ya kuhisi huenda kutakuwa na sababu ya msingi mpaka hayo yote yanatokea kwake aliamua kumsubiri daktari mzuri ambaye ni muda kama baba yake mzazi alivyokuwa amezoea kumwambia anapokuwa na uharaka wa kutaka kulijua jambo fulani linapokuwa linamtatiza kwenye maisha yake.

 

JOSE MARTI INTERNATIONAL AIRPORT

Hii ndiyo airport kubwa zaidi na bora zaidi ndani ya nchi ya Cuba, ni airport ambayo huwa inahudumia wateja zaidi ya milioni nne kwa mwaka mzima, inapatikana kwenye mji mdogo wa Boyeros ni kilomita 15 tu kusini magharibi mwa Havana ambao ndio mji mkuu wa Cuba. Masaa 23 na dakika zake 30 yalikuwa yamepita ndio muda ambao ndege aliyokuwa amepanda Jamal ilikuwa inatua ndani ya nchi ya Cuba, nchi ambayo inasifika sana kwa ufuaji wa makomando wakubwa duniani na mbinu nyingi sana za kivita japokuwa ni nchi ndogo sana kieneo. Jamal aliweza kushuka na abiria wenzake wote, alikuwa haelewi ila aliwafuata hao watu wote waliokuwa wanatoka hapo hatimae alifika eneo la mapokezi, hakumwangalia Kwanza mwenyeji wake bali alikuwa akishangaa namna kulivyokuwa kumechangamka sana alitabasamu baada ya kukumbuka maisha aliyokuwa anayaishi mbeya Kyela.

 

"Nusu ya furaha ya maisha ya mwanadamu yamekuwa ni pesa sasa, ukiwa na pesa unaweza kwenda popote pale duniani, unaweza ukanunua vitu karibia vyote ukiweka pembeni pumzi ya kuivuta ili uishi, asante MUNGU namimi leo nimetoa mikosi kufika nchi za watu huku" alitabasamu baada ya kuyaongea haya maneno huku akijinyoosha kwa furaha, aliinama chini ili achukue kibegi chake kidogo kwani hakubeba vitu vingi zaidi ya nguo chache tu na passports zake za kusafiria na nguo chache. Kabla ya kuibeba hiyo begi yake ndogo alitokea mwanamke mmoja mrembo sana mbele yake alimpamia Jamal kimakusudi kabisa ila kwa vile Jamal alikuwa ameinama alidhani ni bahati mbaya, alikuwa imara licha ya kupamiwa wala hakutikisika zaidi yule mdada alibaki kumshangaa kijana huyo aliye onekana kuwa kuku wa kienyeji kwenye jiji hilo (mshamba). Jamal wakati anakaanza kumuomba msamaha huyo dada alisonya na kuachia tusi zito kwa kiingereza lakini lilieleweka kichwani mwa Jamal mrembo huyo aliondoka kwa hasira Jamal akiwa anamshangaa tu, baada ya sekunde thelathini aligeuka ili aweze kumuangalia tena huyo mwanamke lakini hakuweza kumuoona ni baada ya kushtuka sehemu waliyo gusana ilikuwa na maumivu kiasi ikionekana wazi huyo alikuwa ni mtu wa mazoezi haswa, alishtuka hakuamini mwanamke mrembo namna hiyo awe amekomaa hivyo hata hivyo alipotezea baada ya kuona mbele hatua kadhaa kuna mtu ameshika bango lenye jina lake akamfuata.

 

"Karibu Havana Mr Jamal" ilikuwa ni sauti ta mwanaume aliyekuja kumpokea ndani ya airport na alionekana kuwa mwongeaji kupitiliza.

"Asante"

 

"Vipi unaenda moja kwa moja au nikuzungushe Kwanza uweze kuijua mitaa yetu kidogo kwenye jiji letu zuri hili la burudani"

"Nipeleke moja kwa moja ninapotakiwa kufika muda huu" hakutaka mambo mengi Jamal alihitaji kufika kwa hao wenyeji wake, moja kwa moja alijua lazima atakuwa anaenda ni kambini tu.

 

Ndani ya sehemu yenye upepo mzuri wa bahari kwa wale wenzetu ambao MUNGU amesha wanyooshea baraka za kuwa na mifuko mirefu ya kujikunia (pesa), Masaki jijini Dar es salaam kwenye ofisi moja kubwa sana na ndipo yalipokuwa makao makuu ya kampuni kubwa ya usindikaji nyama nchini iliyojulikana kama M96 OWNER'Z ndani ya ofisi ya bosi wa hiyo kampuni alikuwa anamalizia hesabu zake kwenye komputa yake mpakato akiwa anaonekana alikuwa yuko bize sana kupiga mahesabu yake kwa usahihi wakati huo milango yote ya chumba chake ilikuwa imefungwa, madirisha yote yalifungwa kilichokuwa kinafanya kazi ni kamera tu pekee ambazo zilimuwezesha kiongozi huyo kuweza kuona kila kitu kilichokuwa kinaendelea ndani ya hiyo kampuni yenye jengo lake likiwa na ghorofa takribani thelathini, baada ya kuona kila kitu chake kipo sawa aliizima hiyo komputa yake akachukua simu na kupiga mahali.

 

"Dakika tano natoka hapa andaa gari halafu kila mtu aondoke hiyo sehemu sitaki kumkuta mtu yeyote naendesha mwenyewe" alionekana kutoa maelekezo sahihi kwa mfanyakazi wake huku akiwa anaiangalia saa yake, alikuwa na haraka kana kwamba kuna sehemu ya mhimu sana alikuwa anawahi na alitoka humo ndani kwa kukimbia mbio kulifuata gari hiyo ilipo. Ilikuwa ni majira ya saa 11 za jioni kuelekea saa 12, alipanda ndani ya hiyo gari yake la kifahari na kuitoa ndani ya uzio mkubwa wa hiyo kampuni yao kwa spidi kali sana na kupotelea kusiko julikana.

 

Ndani ya soko la Buguruni, ni soko dogo ambapo panauziwa bidhaa za majumbani hususani vyakula kama matunda na vingine vingi Kama wabongo (watanzania)tunavyo wajua kwa kuchangamkia fursa maeneo ambayo wanaona kuna biashara zinaendelea. Ndani ya eneo hili kulikuwa na omba omba mmoja aliyekuwa maarufu sana kwa muda mrefu ndani ya soko la Buguruni zaidi ya miaka mitano sasa yupo ndani ya hii sehemu alikuwa amesha zoeleka mno na kila mtu alikuwa akimchukulia kama mtu asiyekuwa na makazi maalumu wala hakubahatika kuwa na ndugu yeyote wa kumpa huduma nzuri ya kueleweka ambayo ingempa uangalau wa maisha kwa sababu muda wote alikuwa mchafu sana akiwa anazurura na vindala vyake vilivyo choka mno. Kwa majina aliyofahamika kwenye hilo eneo lilikuwa ni jina moja tu la Jumbe. Hakuna mtu hata mmoja aliyewahi kujua asili ya huyu omba omba mchafu wala kujua uhalisia wake kabla ya kuwa kichaa kwamba ni nini kilimkuta mpaka akawa kwenye hiyo hali ya maisha magumu sana akitegemea kuomba ili aweze kuweka kitu kinywani pake.

Zaidi zaidi watu wengi hususani wenyeji wa pale walikuwa wanajua kwamba huyu omba omba kila siku tatu za wiki ndani ya siku saba huwa anapandwa na kichaa ambacho huwa kinamfanya kupiga makelele hovyo hovyo kwa nusu saa kila kikimpanda, kwa baadhi ya binadamu walio jaaliwa roho za upekee na hofu ya ukuu wa MUNGU ndani yao hawakuacha kumsaidia kwa chochote omba omba huyu ili kidogo nayeye aweze kuinjoi uwepo wa watu hapa duniani. Siku tatu za wiki ambazo kichaa chake kilikuwa kinampanda lililuwa linaonekana gari moja jeupe la bei ghali sana na huwa inaonekana wanamletea dawa na kuondoka haraka hayo maeneo, kama ujuavyo watanzania wengi hawakuhisi chochote zaidi ya mambo ya kishirikina kwamba huenda mtu mwenye hilo ghari amemfanyia mwenzake hivyo ili achume utajiri kwa njia zisizo za halali, hayo mawazo yalikuwa yanakuja kutokana na watu wengi kuwa na asili ya uvivu wa ufanyaji kazi wakisubiri kuwakosoa walio fanikiwa Kwa kuwahusisha na hayo mambo ya nguvu za giza ili wao wasionekane ni wavivu mbele ya jamii.

 

Huyu omba omba mchafu na kichaa alikuwa na kitu kimoja cha kushangaza sana ndani ya mwili wake, ni miaka mitano sasa imeisha hakuwahi kuosha nywele zake hata mara moja ambazo kila siku zilikuwa zinajisokota rasta na kuwa ndefu zikizidi kuwa chafu mno lakini hakuonekana kuzijali kabisa alichokuwa anawaza yeye ni kupata namna tu ya kuweza kula ndani ya hiyo mitaa.

"Shika hiyo ndugu yangu usije ukafa bure kwa MUNGU tukaonekana hatukuwajali wanadamu wenzetu" alikuwa ni mpiga debe mmoja mzoefu wa hayo maeneo akiwa anamrushia huyo omba omba kipande cha mhindi wakati huo alikuwa amekaa karibu na bara bara ya kwenda Temeke, yule omba omba aliudaka ule mhindi na kumpa alama ya ushindi yule mpiga debe kisa akakiweka kile kipande cha mhindi kwenye mfuko wake, aligeuka akamuangalia tena yule mpiga debe kisha akatabasamu na kuondoka hapo akiwa kayakaza macho yake mbele tu wala hakugeuka kuangalia nyuma, kwa miaka mingi aliyokuwa amekaa hapo aliweza kuwaelewa vyema wanadamu namna wanavyo wadhalilisha wanadamu wenzao wenye kipato cha chini, walikuwa wakisimangwa na kutukanwa japo hakuwa na muda nao ila moyoni alikiri pesa ni sabuni ya roho huwa inamfanya kila mtu anukie na kuwa na mvuto wa pekee sana kwenye macho yake anapokuwa anatazamwa na watu wengi.

 

Safari yake ilienda kuishia kwenye uchochoro mmoja aliangalia huku na huku hakuona mtu alipanda juu ya ukuta kwa sarakasi moja ya juu kama mashine inavyokuwa inaenda haraka aligeuka tena kutazama nyuma aliwaona watu kwa mbali wakiendelea na shughuli zao alitabasamu tena na kurukia upande wa pili ambako kulikuwa na majumba mengi yenye viwanda vidogo vidogo ndani yake ambapo mengine yalikuwa hayatumiki, kwa mbele kulikuwa na bara bara ndogo ya lami mbele kidogo kulikuwa na gari la kifahari mno lilionekana kumsubiri hapo, hakuwa na muda wa kupoteza alijitazama juu mpaka chini akajicheka sana kisha akaingia zake kwenye gari, gari lilitolewa kwa nguvu bila kujali kama kungekuwa na mtu mbele au nyuma ingekuwa ni hatari ila kilicho angaliwa hapo kwanza ni umuhimu wa huyu omba omba kichaa mchafu sana ndani ya Buguruni kuweza kuwa salama pamoja na kuonekana kuna mahali ambako ni mhimu sana alitakiwa kuwahi kufika.

 

Huyu Omba omba ni nani hasa kwenye mji wa watu wapenda pesa huu!?......sehemu ya tano sina la ziada tena MUNGU akipenda tukutane wakati ujao.

 

Bux the story teller

 

 

Previoua Next