Reader Settings

Msisimko wa Regina

Hamza alimshika tai yule dokta kwa nguvu  akiwa amemkazia macho.

“Unapaswa kuniitia mtaalamu wa kunipa maelezo ya kutosha na sio kutafuta Credit kwa kuniambia  mke wangu yuko sawa”

“Sawa Mr .. ngoj,,, ngoja niite   daktari  bingwa wa

masuala ya  ubongo, aje na akupatie maelezo”Aliongea kwa kutetemeka  na Hamza alimwachia.

“Wife usiwe na wasiwasi ,  nitajua  njia ya kukusaidia  kurudisha kumbukumbu zako. Unapaswa kushirikiana nao  wakufanyie vipimo kwanza”Aliongea akimwangalia Regina.

“Sitaki kufanyiwa vipimo. Nataka kuondoka hapa” Regina  haraka alishuka chini akiwa hana viatu vyovyote na kutaka kutoka  lakini Hamza aliwahi kumzuia kwa kumshika mabega.

“Mke wangu , naomba unisikilize , nipo tayari  kukuthibitishia  mimi na wewe ni mume na mke , tuna hadi cheti cha ndoa”Aliongea Hamza.

“Tuna hadi cheti , kiko  wapi?”Aliongea Regina akiwa amekunja sura. “Kipo nyumbani”

“Na hapa tupo wapi?”

“Paris”

“Kwanini tuwe Paris?”

Hamza hakujua namna ya kuelezea  , lakini  muda ule alimkumbuka Shangazi.

Hivyo Hamza haraka haraka alitoa simu yake na kuitafuta namba ya Shangazi na kupiga.

Haikuchukua muda mrefu , Shangazi alipokea simu ile , masaa hayakupishana sana kati ya Tanzania na Paris hivyo , ilikuwa ni rahisi shangazi kupokea simu yake.

“Hamza mnaendeleaje huko, sijadhania utapiga?”Aliongea Shangazi na haraka  Hamza aliweka simu ile loudspeaker , ili na Regina aweze kusikia.

“Shangazi  hivi cheti chetu cha ndoa  na mke wangu kipo wapi?”

“Cheti chenu cha ndoa! Mimi najuaje , labda kitakuwa ndani ya chumba cha Regina, kwanini unauliza?” Aliongea na Regina alionekana kushangaa.

“Shangazi , nimeolewa?!”

“Regina unaongea nini?  Kuna tatizo huko kwani , si umeolewa zaidi ya nunsu mwaka sasa..” Shangazi upande wa pili alionekana kuchanganyikiwa.

"Mhmh, inakuwaje niolewe…" Aliongea Regina chini chini. Hamza, ili kumzuia Shangazi kutokuwa na wasiwasi, alimtuliza na kumwambia wanarudi nyumbani siku sio nyingi.

Mara baada ya kukata simu, Hamza alimwangalia Regina usoni kwa upole.

"Wife, unaonaje sasa? Umeamini ni kweli mimi ni mume wako kabisa. Ni kwamba tu ulipata majeraha ndiyo yanayokufanya usikumbuke, ila ni kwa muda tu."

Regina, mara baada ya kusikia hivyo, alionekana kuwa na wasiwasi. Aliinua mkono wake na kumnyooshea Nyakasura.

"Huyo mwanamke ni nani?"

"Huyu anaitwa Nyakasura," alijibu Hamza. "Kwanini anaonekana kama anakupenda?" Aliongea Regina.

"Nini! Mimi kumpenda? Wewe Regina, hebu acha kuongea ujinga wako unavyojisikia kwa sababu umepoteza kumbukumbu. Sipendelei wanaume wahuni mimi," aliongea Nyakasura.

"Wife, hebu acha kuongea ujinga. Sina mahusiano yoyote na Nyakasura. Ni kwamba tu ulivyokuwa

umeumia, alikuja na kutusaidia." "Ila kasema wewe ni muhuni, ni kweli?"

"Hapa…" Hamza alijikuta akikosa maneno, hakujua hata ajibu ndio au hapana.

"Ni muhuni ndio, ana wanawake zaidi ya watatu

Dar. Nakuambia haya kwa sababu huna kumbukumbu," aliongea Nyakasura akimsagia Hamza kunguni.

"Imekuwaje nikaolewa na mwanaume wa hivi mimi? Wewe umetumia uchawi kunipata?"

Hamza chozi lilitaka kumtoka, lakini machozi yalikuwa mbali. Hakutaka kujitetea na aliishia kujilaumu kuja na Nyakasura hapo.

"Mke wangu, naweza kukuelezea hivi vitu taratibu tukisharudi nyumbani. Unaonaje ukifanyiwa vipimo kwanza na tusubiri mpaka kumbukumbu zako zikirudi?" Hamza alibembeleza.

"Kama unataka kuelezea, elezea sasa hivi. Hili halina uhusiano wa mimi kwenda kufanya vipimo. Kipi kingine unanificha?" Aliongea Regina huku ukauzu ukizidi kuonekana kwenye uso wake.

Hamza kichwa kilimuuma, na mara baada ya kufikiria kwa sekunde kadhaa, aliishia kusaga meno yake kwa nguvu na kisha akatingisha kichwa. "Ndio, ni kweli nina wanawake wengine, lakini mke wangu nakupenda sana. Ni wewe pia uliejaribu kuniokoa ndio maana ukaumia," aliongea Hamza huku akimwangalia Rhoda ambaye pia alitingisha kichwa.

"Sister Regina, mimi naitwa Rhoda. Kila anachosema Bro ni kweli."

"Mh, mbona siamini? Yaani mwanaume kama wewe nilitaka kufa kwa ajili yako?"

"Lakini ndio kweli mke wangu."

"Haiwezekani. Lazima sikuwa na akili nzuri na sasa hivi nimeamka. Sikujui na usiniambie nakupenda. Siku nyingine usije kunisogelea tena." Aliongea Regina akiwa na ukauzu.

Hamza alijikuta akibung’aa, hakuamini hali ingefikia katika hatua hiyo.

"Wife…"

"Usiniite wife mimi, niko single," aliongea Regina akiwa amekaza macho kuonyesha usiriasi.

Hamza macho yake yaliishia kukumbwa na majonzi na maumivu. Aliishia kuvuta pumzi nyingi na kuzishusha kisha akaweka muonekano wa kizembe. Pengine muonekano huo ndio uleule aliokuwa nao mara ya kwanza anakutana na Regina. "Basi sawa Bosi, hunijui, ndio nakubali. Unapaswa kupumzika, ngoja niwasindikize hawa," Hamza aligeuka na kuwapa Rhoda na Nyakasura ishara ya kuondoka.

"Nataka simu yangu, nahitaji kuwasiliana na watu wangu," aliongea Regina.

"Hakuna shida, ila simu yako haipo hapa. Ngoja niwasiliane na Josh kutoka kwenye kampuni akuletee."

Mara baada ya Regina kusikia hivyo, hatimaye muonekano wake ulirudi katika hali ya ahueni na kutingisha kichwa kukubali.

Mara baada ya kundi hilo la watu kutoka nje ya korido, Nyakasura alimwangalia Hamza na tabasamu lisilokuwa tabasamu.

"Mr Hamza! Unapanga kufanya nini kuanzia sasa? Naona amekusahau," aliongea Nyakasura kwa kejeli.

Hamza aliishia kukunja sura tu huku akiona wazi kuwa Nyakasura alikuwa akiyafurahia matatizo yake waziwazi.

"Ndio kanisahau, ila wewe inakuhusu nini?" aliongea Hamza.

"Mh! Ni kweli hainihusu, ila sitaki tu kuona ukilia," aliongea Nyakasura huku akimpandisha.

"Mr Hamza, tuandae vipimo?" aliuliza Dokta.

"Haina haja," aliongea Hamza akitingisha kichwa,

na kufanya wafanyakazi wa hospitali waliokuwa wakimfuata nyuma kushangaa.

"Kwanini?"

"Nishasema haina haja, hakuna haja ya kuwa na sababu." Mara baada ya kuongea hivyo, aliwaambia waondoke.

"Nyie pia mnapaswa kuondoka. Rhoda, unaweza kupumzika kwanza kwa siku kadhaa au kama upo vizuri, tangulia kuelekea Dar utusubiri mpaka tutakaporudi," aliongea Hamza.

"Huna haja ya kunifukuza, maana ndio naondoka," aliongea Nyakasura.

"Bro, take care of yourself," aliongea Rhoda, akijua hata kama abakie asingekuwa na msaada.

Mara baada ya wanawake hao wawili kuondoka, Hamza aligeuza na kurudi wodini.

“Kuna kitu kingine unataka. Nishasema siitambui hio ndoa , unaweza kuondoka , mwanasheria wangu atakupigia simu”Aliongea Regina.

Hamza aliishia kumwangalia msichana huyo ambaye ukauzu wake ni kama wa malkia wa

kuzimu. Kwanini ni kama anavyoongea nishawahi

kukutana naye kabla ya kumjua? Hamza alijiwazia. Lakini licha ya kuingiwa na wazo na hisia za namna hiyo, alijikuta tu akipotezea na kujiambia aliyekuwa mbele yake ni mke wake Regina na si mwingine.

"Najua haunikumbuki. Kama unataka talaka, nitakubali, ila siwezi kukuacha," aliongea Hamza. "Kwanini? Si una wanawake wengine, kwanini usiwachukue wao?" aliuliza Regina.

Hamza alitoa tabasamu na kisha alitembea kwenda kukaa pembeni ya kitanda na kumwangalia Regina na urembo wake.

"Kuna wanawake wengi sana kwenye huu ulimwengu, lakini kuna mwanamke mmoja tu ambaye ni mke wangu, na ndiye huyu aliyeko mbele yangu. Nawezaje kukuacha?"

"Wewe ni kichaa. Kwanini huelewi? Sikupendi tena. Haijalishi ni uhusiano gani tulikuwa nao, sasa hivi hatujuani."

"Hata watu ambao hawafahamiani wanaweza kuwa marafiki," aliongea Hamza.

"Unamaanisha nini?"

"Hamna tu. Ninachotaka kusema ni kwamba siwezi kukuacha. Ilimradi naishi, nitaendelea kukupenda. Kama umenisahau, nitakufukuzia mpaka unipende tena. Ukipoteza kumbukumbu zako tena, nitakufukuzia tena. Hata upoteze kumbukumbu mara elfu moja, kazi yangu itakuwa ni kukufanya unipende tena na tena na tena, na kuendelea kukufanya kuwa mwanamke wangu," aliongea Hamza kwa msisitizo.

"Kwani mimi ni bora sana au ni kwa sababu ni mrembo kuliko wao?"

"Kabisa, mke wangu, wewe ni mrembo sana, lakini suala la msingi ni kwamba nikishafanya maamuzi ya kukufanya mke, hilo ni suala ambalo haliwezi kubadilika."

"Kwa hiyo unanipenda sana?"

"Si kukupenda sana, nakupenda mno."

Regina, mara baada ya kusikia hivyo, alionyesha hali ya uchokozi kwenye macho yake.

"Kama unanipenda sana, nikikuambia uachane na hao wanawake wengine, upo tayari?"

"Hapana. Pia nawapenda."

"Mhmhh! Wewe ni muongo. Huwezi halafu unasema unanipenda sana?" aliongea Regina kwa hasira.

"Mimi si muongo. Kama ningekuwa muongo nisingekubali. Sina aibu na vilevile mimi ni mtu mwenye tamaa. Hivi ndivyo nilivyo."

"Sasa nikuambie labda uwe tayari kuachana na hao wanawake wengine, la sivyo siwezi kukubali." "Haina shida. Nitafanya kila liwezekanalo kukufukuzia mpaka unikubali mimi na wanawake wangu. Nitakufanya uone kwamba mimi ndiye mtu sahihi zaidi kuwa mume wako kwenye ulimwengu huu."

"Wewe ni mshenzi!!" Regina alikosa neno. "Vyovyote vile, kwa sababu nina uvumilivu na muda wa kutosha, nitahakikisha unalipenda taratibu hili lishenzi na kuolewa nalo tena."

"Sitaki kuongea na wewe tena."

Regina aliishia kulala chini na kujifunika na blanketi gubigubi huku akigeukia upande mwingine akitaka kulala.

Hamza aliishia kuangalia mgongo wa Regina na kisha alitoa tabasamu.

"Wife, naitwa Hamza. Kwa leo kariri jina langu."

"Silikumbuki hilo jina."

"Haina shida. Utalikumbuka taratibu taratibu. Ukisahau, kila siku nitakutajia tena."

"Nina njaa na usingizi, halafu unalazimisha nikumbuke jina lako? Hivi kuna mtu anataka kufukuziwa na mwanaume kama wewe?"

Hamza, mara baada ya kusikia sauti ya Regina ndani ya shuka, alihisi kuna kitu hakipo sawa. "Wife, kuna kitu unataka kula nikakuletee?" "Bila ya kula donati zenye ladha ya strawberry, siwezi kukumbuka jina lako baya milele," aliongea Regina.

Hamza kusikia hivyo alitetemeka, palepale alijirusha kitandani na kumgeuza Regina. Aliishia kumwangalia usoni na mara baada ya kuona mwonekano wa kichokozi wa Regina, hatimaye alijua.

“Wife! Ina maana hukupoteza kumbukumbu?” Hamza alipiga makelele.

“Hebu punguza makelele, unadhani mimi kiziwi? Hizo donati unaenda kuleta au huendi?”

“Haha... naenda bwana. Ila mke wangu, kwa hiyo

hukupoteza kumbukumbu? Kwanini sasa uliniigizia?”

“Nani kakuambia unikatili? Yaani nilipona chupuchupu kufa, lakini bado ukawa unacheza cheza na Nyakasura, huku unajua kabisa simpendi.”

Hamza hatimaye alijua kuwa ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu ulikuwa umesababishwa na Nyakasura. Hakuamini kwamba alikuwa akichezewa akili na Regina. Alijihisi kama sekunde iliyopita alikuwa kuzimu na nyingine peponi. “Dah! Mke wangu, kwa kujua tu kuigiza, upewe tuzo. Ila mke wangu, naomba usifanye hivi siku nyingine?”

“Nani kakuambia unikasirishe?”

“Lakini umenikatili. Yaani ghafla tu unaniambia niachane na kila mwanamke? Wife, uko siriasi au ulikuwa ukifanya tu utani kuniona nitakuwaje?” “Yaani wewe aibu huna. Licha ya kupoteza kumbukumbu kwa ajili yako, hutaki kujali. Nilijaribu kuona kama nitakuwa na uwezo wa kuwaondoa hao vimchepuko vyako, lakini usivyo na aibu sasa...”

Hamza jasho lilimtoka. Namna alivyochezewa na Regina, kama asingekuwa jasiri na kutovuka mstari aliojiwekea, angeingia mzima mzima. “Mke wangu, usije kukasirika. Najua nimekuangusha, ila nitakuwa mwema kwako maisha yangu yote,” aliongea Hamza huku akicheka.

“Unaongea sana, nina njaa mimi.” “Okey! Sawa mke wangu, ngoja nikakuletee unachopenda.”

Ukweli ni kwamba Hamza alijua muda mrefu tu Regina hakuwa amepoteza kumbukumbu. Mara baada ya kuona Regina kaanzisha kamchezo, aliamua kushirikiana naye. Ndio maana aliwaambia madaktari haina haja ya vipimo.

Regina aliishia kumuangalia Hamza aliyekuwa akitokomea nje. Macho yake yalionyesha hali ya furaha lakini pia masikitiko kwa wakati mmoja.

Ndani ya nusu saa, Hamza aliweza kurudi na boksi la donati na kumpatia Regina. Kama kawaida, mwanamke huyo alipoziona donati, mwili wake ulimchangamka—ndio kilichomtokea mara zote. Hamza, upande wake, alitaka kujua maendeleo ya Regina mara baada ya pete ile kumfanyia miujiza. “Wife, mwili wako unajihisi vipi? Unajua ile pete ilichofanya?”

“Mimi najuaje ilichofanya kama haujaniokoa wewe?”

“Usiniambie haikushangazi. Hakuna hata jeraha kwenye mwili wako. Unadhani naweza kukufanyia upasuaji halafu jeraha litoweke?”

Muda ule Regina alishika kifua chake.

“Ah! Halafu ni kweli. Kwanini sina kidonda? Nilikuwa na wasiwasi nitapata kovu baya.”

Hamza aliishia kusungua paji la uso wake huku akijiuliza, Inamaanisha kweli huyu mwanamke

hakugundua kuwa hana kidonda?

Hakuwa na jinsi ila kumwambia stori nzima namna alivyopona. Regina, mara baada ya kusikia, uso wake ulijawa na mshangao na shauku kwa wakati mmoja.

“Hakuna ninachohisi kutoka kwenye hii pete. Ni kweli ndio ilioniokoa?”

“Hata mimi sina uhakika. Nashindwa kuelewa ni mwili wako wenyewe ambao una koneksheni na hii pete au vipi. Ukweli nimewaza na kuhisi labda damu yenu, hii pete, na kuhusu stori ya kitabu kisicho na maandishi, kuna uhusiano.”

“Kivipi?”

“Hata mimi sina uhakika pia, lakini Huge wa Binamu anaonekana kuithamini sana hii pete. Ila kwa sababu ya uhusiano wetu ndio maana halazimishi kunipokonya kwa nguvu. Pili, anaonekana kuwa na hasira tunaimiliki na haonyeshi tu. Lakini kama tunaendelea kuwa nayo, tunapaswa kujua siri iliyopo nyuma ya hii pete, la sivyo itakuwa hatari kwetu.”

“Ni mambo magumu kweli. Kwa sasa tuachane na haya. Tutaongea vizuri tukirudi.”

Regina hakutaka kuumiza kichwa chake kuhusu pete hiyo, hivyo aliendelea kula donati zake.

Waliendelea kudumu ndani ya wodi hiyo kwa muda, huku Hamza akiendelea kuchokozana na Regina mpaka pale simu yake ilipoanza kuita. Alipoangalia, aliyepiga alikuwa Sally, na alipokea haraka.

“Sally, washafika hao?” aliuliza Hamza. “Vipi kwanza wewe? Hali yako? Hujapata majeraha?” sauti ya mwanamke ilisikika kwa Kiingereza.

“Kwa hiyo unajua?”

“Taarifa ilishatumwa kwangu, na nimetoka kuongea na Black Fog na kanithibitishia. Prince, nadhani sikupaswa kuendelea kubakia huku kisiwani. Nilipaswa kuwa karibu yako kukupa ulinzi,” aliongea Sally kwa wasiwasi, kiasi cha kutaka kulia.

“Sally, nipo sawa. Huna haja ya kuwa na wasiwasi. Mwili wangu upo sawa pia. Sijapoteza uhai kutokana na janga lililonipata, ila nimepiga hatua kutoka kwenye changamoto iliyokuwa inaninyemelea. Ni jambo zuri kwangu.”

“Kama upo sawa, tumefarijika. Ndege ya Azzle imewasili na wote wana wasiwasi. Nitaongeza umakini kufuatilia watu wa Baraza la Set na Od ones. Ukipata muda, njoo ututembelee...” Kulikuwa na hali ya uchungu kwenye sauti ya Sally. “Sawa, nitatafuta muda wa kuja huko baada ya mwaka mpya.”

Hamza mara baada ya kukata simu, aligundua Regina alikuwa akimwangalia huku akimkodolea macho.

“Nini tatizo, mke wangu?”

“Huyo Sally, anakupenda sana?”

“Namchukulia kama mdogo wangu, kama ilivyo kwa Rhoda.”

“Hata nikiongea, nitakuwa tu najipotezea muda,” Regina alijibu kwa kutikisa kichwa, kisha hakutaka kujisumbua zaidi. Aliishia kuweka boksi pembeni na kujilaza kitandani.

 

Mchana huo, Regina alifanyiwa vipimo vya mwisho na alionekana kuwa sawa kabisa. Hamza, akiwa na moyo wa furaha, alimwambia Mzee Pino kutoa mchango wa Euro milioni kumi kwa hospitali hiyo kama shukrani.

Baada ya kuondoka hospitalini, wawili hao walipanga kukaa Paris kwa siku mbili zaidi. Kwanza, Regina alipanga kwenda kazini kuweka mambo sawa na Josh na wengine. Pili, alitaka kumnunulia Shangazi zawadi pamoja na baadhi ya marafiki zake waliokuwa na uhusiano mzuri naye.

Siku ya kwenda kuchagua zawadi, Regina alionekana kusita kidogo lakini mwishowe aliamua na alinunua vipodozi vya kila aina, akipanga kumpelekea Lamla. Hamza, mara baada ya kuona jambo hilo, aliishia kumkubali Regina kwa roho yake nzuri. Alijiambia moyoni, Kama ingekuwa

mtu mwingine, asingeweza kumsamehe kabisa mtu kama Lamla.

Hatimaye siku iliyofuata, safari ya kurejea Tanzania ilianza. Hamza hakusahau kununua zawadi kwa ajili ya “warembo wake” wengine, lakini hakuthubutu kumfanya Regina kugundua jambo hilo. Zawadi hizo zilitangulizwa kwa ujanja kwa anuani ya Morogoro.

Kwa bahati nzuri, hata baada ya kufika nchini, Regina alikuwa bize sana na masuala ya kampuni. Kulikuwa na matukio mengi yaliyokuwa yakifanyika kila mwisho wa mwaka, hivyo hakuwa na muda wa kumfuatilia Hamza kuhusu alichokuwa akifanya.

Hamza alipata nafasi ya kusafiri kwenda Morogoro, ambako alikutana na maboksi mengi ya mizigo kutoka Paris na kuyapakia kwenye gari. Hakusahau kumwachia mke wa Mzee Hizza baadhi ya vipodozi kama zawadi.

Ile tu Hamza alipofika Dar es Salaam na alikuwa akielekea kwa Dina, simu yake ilianza kuita. Alipoangalia, aliona mpigaji ni Black Fog, na akapokea haraka.

“Bro, kikosi cha Baffodil nimekwisha kukikusanya. Ni wapi napaswa kuwapeleka?”

Hamza alifikiria kidogo, kisha akasema, “Sio mbaya, tuende kwa Dina kwanza. Nitajua cha kufanya kuanzia hapo.”

Previoua Next