Hamza, mara baada ya kufika nje ya mgahawa wa Dina, aligundua kuwa sehemu hiyo ilikuwa imepambwa kwa miti ya Christmasi. “Bro, karibu sana. Marafiki zako wapo ndani wanakusubiria,” aliongea Lau, ambaye alimsaidia Hamza kushusha mizigo.
Muda huo ndipo Hamza alijua kuwa Black Fog na wenzake walikuwa tayari wamefika. Alimshika bega Lau kwa kugonga kidogo huku akisema:
“Nilisikia uliumia, vipi? Umeshapona sasa?” “Ni majeraha madogo sana, bro. Niko sawa kabisa sasa hivi,” alijibu Lau huku Hamza akitingisha kichwa na kuingia ndani ya mgahawa huo.
“Umesema marafiki zangu wapo hapa. Mbona siwaoni? Wako wapi?” aliuliza Hamza. “Ndiyo bro, wamefika. Madam kawachukua na kuwapeleka kwenye nyumba ya wageni, nyuma ya tanki,” Lau alieleza.
Hamza, baada ya kusikia hivyo, alijua mahali nyumba hiyo ilipokuwa. Ilikuwa moja ya nyumba zinazomilikiwa na Dina ndani ya eneo hilo la Kijichi. Mara baada ya kutembea kuelekea huko, alipofika karibu na geti jeusi, alilisukuma na kuingia ndani. Palepale alimwona Dina akiwa anazungumza na kundi la wanaume na wanawake kama kumi hivi.
Watu hao walikuwa wamevalia kawaida sana. Ilikuwa vigumu kujua kama walitokea nje ya nchi, kwani hata Dina alikuwa akizungumza nao kwa Kiswahili. Mbali na Black Fog, ambaye alikuwa na mwonekano wa “ushombe shombe,” wengine wote walionekana Waafrika kabisa. Moja ya sifa za maninja waliokuwa wakifundishwa na Asmuntis ni uwezo mkubwa wa kuishi katika kila aina ya mazingira na kuendana na wenyeji. Hicho ndicho kilichomfurahisha Hamza.
Hamza alionekana kuridhika kuwaangalia tu. Kitu cha msingi kwake kilikuwa ni kupata maninja ambao wanaweza kuishi Tanzania bila kushitukiwa. Vinginevyo, kama angeleta wazungu wenye nywele nyeupe na macho ya bluu, ingekuwa vigumu kuwaficha hata kwa kutumia mbinu za kisasa.
Mara baada ya kumuona Hamza, kundi lile la watu lilisimama haraka, nyuso zao zikionyesha hali ya msisimko. Hamza aliishia kukohoa kidogo na kuwapa ishara ya kukaa. Hakutaka kuabudiwa Tanzania, kwani kwanza, haikuwa na haja, na pili, hakupenda kabisa. Kundi lile la wauaji lilielewa haraka kuwa Hamza hapendi makuu, lakini bado walimwangalia kwa macho ya heshima na kumkubali sana.
“Hamza, kwa nini hukuniambia una marafiki kibao wanakuja? Sikuandaa chochote kabisa. Nimefanya maandalizi haraka haraka,” aliongea Dina, ambaye alikuwa amependeza mno na kuvutia.
“Usijali, Sister. Tumezoea kulala hata nje. Popote pale tunakaa, hayahitajiki maandalizi makubwa,” alijibu Rhoda.
Kundi lile lilitingisha kichwa kuunga mkono bosi wao, Rhoda. Kwao, kuchaguliwa kuja Tanzania kutimiza maagizo ya mtu mzito kama Hamza ilikuwa bahati kubwa. Hawakujali wanakula nini au watalala vipi.
“Rhoda, unaweza usijali, lakini kwangu ni tofauti. Ninajali sana. Ni mara chache sana Hamza kunitambulisha kwa marafiki zake wengi namna hii.
Ijapokuwa siwajui, lakini nataka kuwakirimia vizuri kwa niaba ya Hamza,” aliongea Dina.
Hamza alimshika mkono Dina na kumpa ishara ya kukaa.
“Hawa, kuanzia sasa, ni wenzetu. Haina haja ya kufikiria sana. Wachukulie tu kawaida. Nadhani bado hamjajitambulisha. Mnaonaje tukianza kujuana kwanza?” aliuliza Hamza.
“Nini! Ina maana hata huwafahamu? Siyo marafiki zako?” Dina alishangaa.
“Ni stori ndefu. Wao wananijua mimi, ila sijawahi kuwaona. Kuna sura kama mbili tu hivi nahisi kuzitambua,” alijibu Hamza, kisha akanyoosha mkono kumwelekezea mwanamke mmoja wa maji ya kunde.
“Wewe ni Amina, kama sikosei, si ndiyo?”
Mwanamke huyo, baada ya kuona Hamza
alilifahamu jina lake, alishikwa na furaha kubwa.
“Ndiyo!”
“Unaonekana kuwa na muda mrefu sana ndani ya Baffodil. Nakumbuka nilikuona mara ya kwanza kwenye Bahari ya Caribbean. Wewe ndiye uliowaua wanajeshi nane wa Baraza Takatifu na kuzamisha meli yao, si ndiyo?”
Amina, macho yake yalichanua kwa furaha aliposikia maneno hayo.
“Ndiyo mimi! Sikudhani unakumbuka vizuri.”
Dina, mara baada ya kusikia maneno hayo, macho yake yalijawa na mshangao.
“Nini? Baffodil? Baraza Takatifu? Mnaongea kuhusu nini?”
Hamza hakuwa na haraka ya kumjibu. Palepale aligeukia wanaume wawili waliokuwa kushoto kwake. Wa kwanza alifahamika kwa jina la Bazo, wa pili aliitwa Hemani, na wa tatu alikuwa Zade. Wote walikuwa na umri wa miaka thelathini kuendelea.
Katika kundi lile la watu kumi, kulikuwa na wanne ambao Hamza aliwafahamu. Hii ni kwa sababu wengi walidumu muda mrefu kama wanachama wa Odd Ones na kuondoka pamoja naye. Alijikuta akifurahi kwani alikumbuka vyema uwezo wao.
Baada ya utambulisho kumalizika, Dina alizidi kuchanganyikiwa. Wakati anataka kuuliza zaidi, geti liligongwa.
“Madam, viongozi wamefika,” aliongea Lau.
“Okey! Wapeleke mpaka kule kwenye ukumbi. Nakuja muda si mrefu,” alijibu Dina, na Lau aliitikia kisha akaondoka.
“Una wageni?” aliuliza Hamza.
“Ndio, ni ndugu wa babu.”
“Ndugu wa babu yako wanafanya nini Dar? Si walikuwa Congo?”
“Babu licha ya kuniachia uongozi, hakutelekeza ndugu zake. Asilimia ya faida inayopatikana ina mgao kwao. Kisinda anaamini yeye alipaswa kuwa kiongozi, si mimi. Ndiyo maana wapo hapa,” alieleza Dina.
“Kuna lolote naweza kukusaidia katika hili?” aliuliza Hamza kwa kujali.
“Kwa leo ni kikao cha kawaida tu. Naweza kumudu mwenyewe. Isitoshe, wanajaribu kunizunguka, lakini michezo yao naijua,” aliongea Dina huku Hamza akitingisha kichwa.
“Kama una wageni, basi ngoja nikutambulishe hawa watu haraka haraka,” aliongea Hamza. Kisha alimweleza Dina kwa ufupi kuhusu wageni hao na kazi yao nchini.
Dina alishangaa kusikia kuwa wageni hao wote ni maninja, tena wakiwa katika mia moja bora ya wauaji waliobobea. Ilimshangaza pia Hamza kuleta kundi hilo Tanzania. Hata hivyo, alielewa baada ya Hamza kumweleza kuwa lengo ni kutoa ulinzi kutokana na hofu ya usalama iliyopo.
Jambo lililomshangaza zaidi ni kujua kuwa Black Fog ni ninja anayeshika nafasi ya tisa kati ya wauaji hatari zaidi duniani. Alikuwa kama haamini, lakini huo ndio ulikuwa ukweli.
“Dina, kuanzia leo, mpatie Amina kazi ya kukusaidia kuhudumia wateja ndani ya eneo hili,” aliongea Hamza.
“Kuhudumia wateja!?” Dina alishtuka.
“Ndio, atakuwa anakulinda, ikitokea upo hatarini ni rahisi yeye kunifikia na kuchukua hatua,” aliongea Hamza. Licha ya kwamba maninja hao walikuwa na uwezo wa hali ya juu, lakini Hamza alijua hawawezi kulinda watu wake kwa asilimia mia moja endapo adui akawa mkubwa zaidi kwa nguvu.
Kuwaweka karibu maana yake alitaka iwe rahisi kupata taarifa pale ambapo adui atatokea kuwa na nguvu, na yeye kuchukua hatua.
“Kama shida ni kuwa na kazi, naweza kumpatia kazi nyingine tofauti na ya uhudumu,” aliongea Black.
“Madam Dina! Naweza kufanya kazi ya kuhudumia wateja, usiwe na wasiwasi kabisa,” aliongea Amina.
“Najua! Ila nitakupatia kazi itakayokuweka zaidi karibu na mimi,” aliongea Dina huku akitabasamu, kauli yake ilimfanya Hamza kutingisha kichwa.
“Amina, unaweza kufanya kuanzia sasa atakachokuambia Dina,” aliongea Hamza, na Amina alitingisha kichwa kukubali.
Kwa sababu ilikuwa tayari ni mchana, Hamza aliona si vibaya akichukua marafiki zake hao kwenda kupata chakula cha mchana. Isitoshe, mgahawa wa Dina haukuwa ukipika vyakula zaidi ya chai.
Mara baada ya kuachana na Dina ambaye alienda moja kwa moja kwenye kikao na viongozi wa kifamilia, Hamza alichukuana na Black Fog na wengine na kuelekea mgahawa mwingine, karibu sana na eneo la mgahawa wa Dina.
Hamza na kundi hilo la maninja walifanikiwa kupata chakula ndani ya mgahawa huo, na muda wa chakula, Hamza aligawa majukumu kwa kila mmoja. Kazi ambayo walipatiwa ni kuwalinda warembo wake kwa namna ya siri sana, huku wakiwa na ukaribu wa kimawasiliano baina yao. Timu hiyo ya usalama kama kawaida ilipaswa kuongozwa na Rhoda.
Ile Hamza anapanga kutoka katika mgahawa huo kwa ajili ya kwenda kumtafuta Yulia, simu yake ilianza kuita. Alipoangalia, aliyekuwa anapiga ni Regina, na alipokea mara moja.
“Wewe Hamza uko wapi? Njoo haraka!” Regina aliongea huku akionekana kuwa na wasiwasi kama vile kuna kitu kikubwa kimetokea.
Hamza alishituka mara baada ya kuhisi pengine Regina yupo hatarini.
“Wife, upo wapi?”
“Nitakuwa wapi kama si kazini? Nataka uje ofisini kwangu. Kwani upo wapi? Hata kama hutaki kufanya kazi, angalau igiza basi unafanya kazi,” aliongea Regina.
“Ofisini? Nini kimetokea huko ofisini kukufanya ukose subira namna hiyo?”
“Mwenzio nilikuwa navuna nishati hapa, na nimeshtuka nahisi kabisa mwili wangu ukinisisimka. Yaani inashangaza kweli, nahisi ni kama vile kila seli ya mwili wangu inapumua. Nataka uje uangalie kama ni nishati ya mbingu na ardhi au ni tofauti.”
Hamza mara baada ya kusikia kauli hiyo, kidogo ajigonge na kudondoka chini. Alijua mwanamke huyo alikuwa hatarini kumbe kapatwa na msisimko.
“Wife, naona unataka kuniogopesha kufa. Umeanza kujifunza muda mrefu mpaka sasa, si kawaida tu kupatwa na hali tofauti ya kimwili. Kama umeanza kuhisi msisimko, basi jua unaendelea vizuri.”
“Nimefurahi sana. Tatizo ni kwamba nilikuwa nikijifunza kila siku ila sikuwa nikihisi chochote. Lakini leo ghafla tu napatwa na msisimko. Yaani ninavyojisikia hapa haielezeki, kumbe hili andiko la kimalaika lina nguvu hivi kwa kurudia rudia tu maneno yake?”
Hamza aliona Regina alikuwa na furaha kiasi hicho, hata yeye pia alifurahi kwa ajili yake.
“Wife, kwa sasa nipo mbali na makao makuu ya kampuni, hivyo nadhani tutaonana usiku nikirudi.”
“Mh! Si useme tu upo na mwanamke hapo na nakusumbua. Unajing'ata-ng'ata ya nini sasa?”
“Wife, unaongea ujinga gani sasa. Nipo na Rhoda na wenzake kutoka Bafodi, najaribu kuwapangia majukumu na mahali pa kukaa…” aliongea Hamza.
Regina mara baada ya kusikia hivyo alikumbuka ujio wa jambo hilo.
“Kwa hiyo unapanga kufanya nini? Kuna kitu unataka nikusaidie?”
“Kwa sababu unafahamiana na Rhoda, unaonaje ukikaa naye karibu?” aliongea Hamza.
“Unamaanisha kama kumpa kazi au?”
“Ndio, unaweza kumtafutia nafasi kwenye kampuni na kumfanya awe karibu yako muda wote.”
“Kwanini wewe usiwe msaidizi wangu moja kwa moja? Hata hivyo unafahamika kama msaidizi wangu tayari na una ofisi kabisa.”
“Niwe msaidizi wako kabisa? Usiniambie bado tu unataka niendelee na aina ileile ya kazi. Kama ni hivyo, sina shida. Kazi yenyewe nyepesi!”
“Unaonaje ukiongoza idara ya usalama wa kampuni? Isitoshe Yonesi hayupo na nafasi yake ipo wazi. Isitoshe pia wale wanaume ni marafiki zako.”
Regina alijua kama nafasi ya Hamza itachukuliwa na Rhoda, maana yake yeye hatakuwa na kazi yoyote ndani ya kampuni. Regina hakutaka kumuona Hamza hana kazi na kuishia kudhurura tu.
Hamza mara baada ya kusikia hivyo hakuona tatizo. Isitoshe, ilikuwa ni kweli alipenda kupiga stori na Aroni na wenzake, lakini pia kulikuwa na motisha ya walinzi wengine kama vile Anna na wenzake.
“Hehe… Kama wife wewe ndio umesema, mimi ni nani hata nipinge?” aliongea Hamza.
“Mhmh, usidhani sijui ni kipi unafikiria.
Ukithubutu kumgusa tena Anna na wenzake, nitawafukuza kazi,” Regina alionya.
“Sithubutu,” aliongea Hamza huku kwenye moyo wake akijiambia kama kuna la kufanyika, linapaswa kufanyika katika hali ya usiri mkubwa.
Mara baada ya kumaliza kuongea na Regina, Hamza alishusha pumzi, akaweka simu yake mfukoni, na kisha alimwangalia mwanaume mrefu mwenye nyusi nyingi usoni.
“Zade, mwanamke unaopaswa kumlinda kidogo si wa kawaida. Nitakupeleka,” aliongea Hamza.
Mwanamke ambaye si wa kawaida anayemzungumzia Hamza ni Yulia. Kuhusu wengine kama vile Eliza, Prisila, na Irene, ili mradi maninja hao watakuwa karibu yao kisiri, wangekuwa salama bila ya kuhisi chochote. Lakini Hamza alijua kama angempanga Zade kwenda kumlinda Yulia kisirisiri, halafu mwanamke huyo alikuwa akizungukwa na watalamu wa juu kama Bertha, lazima angegundulika. Pengine mpaka maelezo yanapatikana, Zade anaweza kusababisha maafa au kusababishiwa maafa.
Hivyo, Hamza aliona akutane kwanza na Yulia ili amkabidhi Zade.
Hamza mara baada ya kuendesha gari mpaka katika hoteli ya Prima, meneja wa hoteli hiyo mara baada ya kumuona Hamza alionekana kumtambua mara moja na kumsogelea kumsalimia.
“Mr. Hamza, mdogo wake wa kiume mkurugenzi, Mr. Yasin, yupo hapa pia. Yupo kwenye banda la farasi nyuma. Mkurugenzi katoa maelekezo niwapeleke huko nyuma,” aliongea meneja.
Hamza alionekana kushangaa kidogo, hakujua nyuma ya jengo hilo kulikuwa na banda la farasi. Ilionekana matajiri walikuwa wamejitengea eneo kwa ajili ya kujifunza kupanda farasi. Kuhusu pia Yulia kuwa na mdogo wake anayefahamika kwa jina la Yasin, hakujua pia. Hii ilikuwa mara yake ya kwanza kusikia.
Hamza mara baada ya kupelekwa upande wa nyuma, aliweza kumuona Yulia aliyekuwa amevalia mavazi ya kuendeshea farasi. Alikuwa akiongea kwa furaha na kijana mmoja mrefu huku wakicheka.
Hata hivyo, licha ya wawili hao kuongea kwa furaha, macho yao yalikuwa na hali ya ukauzu na utofauti, ni kama vile tabasamu yao yalikuwa ya kinafiki.
Ukiachana na wawili hao, chini ya mwanvuli katika kiti cha kupungia upepo wa bahari, kulikuwa na mtu mwenye mwili uliotuna—Bertha, mlinzi wa Yulia. Pembeni yake kulikuwa na kijana mdogo ambaye alikuwa akizungumza naye, na kwa namna walivyokuwa wakizungumza, ni kama vile kijana huyo ni mtu muhimu sana kwake. Hamza alijikuta akikunja sura kidogo, akihisi kuna kitu kinaendelea, akajiuliza kama huyu kijana ndiye mpenzi wa Bertha aliyekuwa akiongea naye mara kwa mara kwenye simu.
Hata hivyo, Hamza hakujali sana, kwani macho yake na ya Yulia yalikutana.
Yulia, mara baada ya kumuona Hamza, macho yake yalichanua, akamkimbilia na kumshika mikono.
“Darling, hatimaye umerudi kutoka Ulaya?” aliongea Yulia kwa kujibebisha. Ila kwa Hamza, mara baada ya kumwangalia usoni, alijua kabisa mwanamke huyo alikuwa akimwigizia. Ingawa hakujua mpango wake ni nini kuonyesha maigizo hayo, aliamua kutoa tu ushirikiano.
Alinyoosha mkono wake, akamshika kidevu na kisha kuinama na kumkisi kwenye lipsi zake nyekundu.
“Nilikumisi sana. Nimerudi ndiyo,” aliongea Hamza, na kumfanya Yulia kutoa tabasamu.
“Ngoja nikutambulishe. Huyu hapa anaitwa Yasin, ni mtoto wa mjomba Ali. Ndio amerudi kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kusherehekea sikukuu za Krismasi na mwaka mpya,” aliongea Yulia. Yasin, kwa kujiamini, alitembea na kumsogelea Hamza huku akiwa na tabasamu usoni.
“Nimesikia kutoka kwa sister amejipatia shujaa mwenye kila sifa. Ni mara yangu ya kwanza kukuona. Naitwa Yasin Ali. Unaonekana kuwa na umri sawa na mimi, hivyo nitakuita tu Hamza,” aliongea huku akimpatia Hamza mkono, na Hamza aliupokea bila shida.
Ijapokuwa walikuwa ndugu, Hamza alipomsikiliza tu huyo bwana, alijua kabisa wawili hao hawana maelewano mazuri. Kitendo cha kusema wao wana umri unaolingana kilionekana kama ishara ya kumkejeli Yulia.
Kwa sababu uhusiano wao haukuwa mzuri, Hamza hakujali sana kufahamiana na huyo bwana zaidi ya kuitikia salamu pekee.
“Yulia, nina jambo nataka kuongea na wewe.
Unaonaje tukitafuta sehemu iliyotulia?” aliongea Hamza kwa haraka, akimzuia Yasin kuendelea kuongea naye.
Comments