Deepstate.
Kwa mtazamo wa Yasin , alijua Hamza angenywea kutokana na ukubwa wake , lakini matokeo yake ilikuwa ni tofauti. Hamza alionekana kutokumjali kabisa wala kuwa na hofu.
Yulia kusikia kauli ya Hamza aliganda kwa sekunde kadhaa , lakini palepale alijikuta akicheka chini chini , katika moyo wake alionekana kuridhishwa na Hamza.
“Babe huna haja ya kuwa na haraka , tuna muda wa kutosha wa kuwa pamoja kwenye ulimwengu huu , ni kwamba tu mdogo wangu Yasin amekuja kunipa zawadi ya farasi na wewe ndio umetokea, unaonaje nikiijaribu kwanza?”
“Unajua kupanda Farasi?”
“Ndio najua , nisingejua kungekuwa na haja ya mimi kujenga banda la farasi nyuma ya hoteli kubwa kama hii , si ingekuwa ni upotevu tu wa pesa?”
Muda huo Bertha aliekuwa bize kuongea na mwanaume , huku akionekana kumvalisha scarf shingoni alisikika;
“Bosi , nimesikia ukisema naweza kupanda mimi au nimesikia vibaya?”
“Wewe mpenzi wangu amekuja , kaa mbali?”Aliongea Yulia.
“Hata mimi kaa mbali , unadhani mpenzi wako tu ndio mwanaume , mpenzi wangu Ayubu pia yupo hapa na ni handsome kuliko huyo Hamza wako”Aliongea Bertha huku akijipiga kifua.
“Unaongea nini mpenzi , acha ukorofi basi”Yule mwanaume mtanashati aliekuwa na Bertha alimtuliza na kisha palepale akasimama na kumsogelea Hamza kwa kujiamini na kumpatia mkono.
“Hello Bro , jina langu naitwa Afande Ayubu Masana , kutoka Kambi ya moto. Mara nyingi nakuwa safarini na bosi Yasin na ndio mara yangu ya kwanza kukuona. Mpenzi wangu ana tabia ya ukorofi naomba radhi kwa ajili yake na ni furaha kwangu kukutana na wewe”
“Hakuna shaka , hakika kweli ni mtanashati kunizidi mimi” Aliongea Hamza kwa dhati kabisa na kumfanya Ayubu kucheka kidogo na kisha akamsogelea bosi wake.
“Bosi Yasin , ngoja nikailete ile farasi , sidhani kama Kocha ataiweza kuiongoza”
“Sawa Ayubu”
“Ayubu unaondokaje bila kuniiaga wakati nimekupa zawadi?”Aliongea Bertha huku akimkonyeza.
Ayubu ambae alikuwa akitembea alisimama na kumkonyeza Bertha na kisha mrembo huyo alisogea na walipeana light kiss na kuachiana. Hamza aliekuwa akiangalia wenza hao, mwili wake ulimsisimka na kujiambia kweli mapenzi ni upofu.
“Darling , uletewe kinywaji?”Aliongea Yulia akipokea glasi ya mvinyo kutoka kwa mhudumu.
“Sipendi kunywa chochote leo”
“Kwanini?”
“Basi tu sijisikii”
“Sister huyu farasi ninaekupatia kama zawadi , ni wa kipekee sana , kwa kumwangalia tu lazima umpende”Aliingilia Yasin.
“Nina farasi wengi wazuri hapa , yupo Holly , Bari na Thera. Nadhani haujapanga kunipatia farasi chotara. Banda langu halina nafasi kwa machotara?”Aliongea Yulia.
“Haha! Farasi ninaekupatia kama zawadi ni wa damu safi kabisa , labda nielezee hivi , kama nisingeweka oda kwa muda mrefu tokea mwaka jana huko Asia nisingeweza kuinunua hata kwa msaada wa marafiki zangu”Aliongea Yasini.
Yulia mara baada ya kusikia hivyo , alijikuta macho yake yakichanua kwa mshangao huku usiriasi ukiongezeka.
“Kama umeagiza kwa muda mrefu hivyo , bado tu unataka kunipatia mimi?”
“Una kila thamani ya kuwa dada yangu , ndio maana nataka kukupatia kitu ambacho hela haiwezi kununua kwa wepesi , kama ulishawahi kusikia Ferghana Horse , ndio zawadi yangu kwako”Aliongea Yasini huku akipiga makofi mengi, wakati huo Yulia akiwa katika hali ya mshangao.
Moja ya hobi ya Yulia tofauti na watu wengi , ilikuwa ni farasi , alikuwa akipenda farasi kuliko magari ya kifahari na hio ilimfanya kufuatilia aina nyingi ya farasi duniani na uwezo wao. Hivyo jina la Farasi aina ya Ferghana halikuwa geni kwake.
“Umelipia shilingi ngapi mpaka kuipata! Nasikia farasi wa aina hio hawazidi elfu tatu duniani?”Aliongea Yulia.
“Hela ni suala dogo sana kwangu . Ijapokuwa mdogo wako sio tajiri kama wewe , lakini sikosi ya kukununulia zawadi ya Christmas”Aliongea Yasin kwa majivuno.
“Umekuja na bahati leo. Mimi ni mpenzi sana wa farasi na ni kwa muda mrefu sana nimekuwa nikizifuga , lakini sijawahi kupata damu ya farasi aina ya Ferghana kabisa. Kwanza unajua kupanda farasi?”Aliongea Yulia akimwangalia Hamza.
“Ndio”
“Haha safi sana , unaweza kuendesha utakavyo baadae”Akiongea Yasin
Wakati wakiongea sauti kali ya farasi iliweza kusikika kutoka mbali.Dakika mbili hazikuwa nyingi ilionekana gari ikisogelea eneo hilo ndani yake ikiwa imebeba Farasi aliekuwa akizunguka zunguka kwa kurudi nyuma na kwenda mbele.
Yulia mara baada ya kuona farasi ile , macho yake yalichanua akiwa na muonekano kama vile haamini.
“Kama nilivyozisikia sifa za Ferghana , umbo lake , rangi yake , kila kitu ni kizuri”
Hamza aliishia kumwangalia mwanamke huyo na hakika aliweza kuona Yulia alikuwa ni mpenzi mkubwa wa farasi.
Ukisikia pure breed or pure blooded horse maana yake ni farasi ambae damu yake ni safi , hana mchananganyiko wowote wa damu kutoka kwenye asili ya chimbuko la uzao wake. Sasa aina ya farasi hao ni ghali mno , kuna hadi farasi waliokuwa wakiuzwa kwa mabilioni ya hela na ni kwa watu matajiri pekee kama Yulia wanaweza kumiliki aina ya farasi hao , farasi wa damu safi ni ghali kuliko magari mengi ya kifahari.
Mara baada ya gari ile kusimama , walitoka wachina wawili kutoka mbele ya gari wakiambatana na Ayubu na kusogea upande wa nyuma na kufungua mlango , sekunde ambayo mlango ulifunguliwa farasi ile iliruka na kutoka na kwa ustadi wa hali ya juu kabisa kijeshi , Afande Ayubu aliirukia na kuishika hatamu zake. Lakini sasa ile farasi ilionekana kukataa kumtii na kuanza kuzunguka ikionekana inataka kumrusha chini Ayubu.
Ayubu pia alikuwa na nishati za mbingu na ardhi , alikuwa akikaribiana na Bertha , lakini licha ya hivyo aliogopa kuituliza ile fatasi na nishati za mbingu na ardhi kwa kuogopa kuidhuru, hivyo alishuka tu chini na kisha akaishikilia kamba na kuisogeza mbele ya Yulia.
Muda ambao Ayubu alisogeza farasi hio mbele ya kundi hilo la watu , alikuwa amejaa jasho la kutosha usoni na Bertha haraka haraka alimpatia kitambaa kujifuta , huku wale wachina wakisalimiana na Yasin.
“Hii farasi bado tu haijatiishwa?”Aliongea Yulia huku akikunja sura.
“Haha.. hio ni farasi poli , nimeipata kwa tabu sana ndio maana nimeamua kukupatia makusudi. Sister , Hamza , mnaonaje mkiijaribisha kuipanda?”Aliongea Yasin huku akiangaliana na wale wachina na kucheka , ilikuwa ni wazi kulikuwa na nia mbaya kwenye macho yake.
“Yasin , unataka kuniua , yaani Ayubu ambae ana mafunzo ya nishati za mbingu na ardhi imemshusha chini kwa nguvu bila hata kuiongoza , ni ngumu kuiitiisha farasi kwa muda mfupi, halafu unataka nijaribu?.”
“Sister kama ujasiri huna basi potezea , sitaki ujidhalilishe kwa kudondoshwa chini kama kifusi. Hamza vipi wewe , unaogopa pia kujaribu?”Aliongea
“Hapana , naweza kuipanda”Aliongea Hamza na kumfanya Yasin kuzubaa kidogo na kisha akacheka.
“Oh! Nimekumbuka sasa hivi nimeambiwa wewe ni mpiganaji hatari sana, lakini huwezi kutumia nguvu kuilazimisha ikutii , maana unaweza kuijeruhi na itakuwa usumbufu tena”
“Siwezi kutumia nguvu na hii farasi haiwezi kuumia”Aliongea
Yasin aliishia kuongea na wale wachina kwa namna ya kuwatafsiria na walionekana kuwa na mashaka na Hamza na upande wa Yulia alionekana kushangaa.
“Babe , kuna haja ya kujaribu sasa hivi , hii farasi ndio kali kuliko zote duniani , inachukua muda mrefu sana mpaka kumtii mtu ..”Aliongea Yulia akiwa na shauku.
Hamza alimshika Yulia kiuno kwa kumvutia kwake na kisha alimwangalia kwa tabasamu la ujasiri.
“Unataka kuipanda na mimi?”
Mkao wao ulikuwa sio wa kawaida , kwa namna sura zilivyokaribiana , Yulia aliweza kuona ni kwa namna gani Hamza alikuwa akijiamini.Mara baada ya kusita kidogo , Yulia aliona ngoja amuamini ili kuona kama kweli anao uwezo wa kutiisha farasi hatari duniani kama Ferghana.
“Nitakusikiliza , unapaswa tu kunilinda nisiumie”Aliongea Yulia huku akiweka mwonekano wa msichana mdogo.
Mara baada ya Yasin kusikia wawili hao wanakwenda kupanda hio farasi , alijikuta akisota ndani kwa ndani , lakini kwa nje aliwapigia makofi.
“Safi sana , Hamza hakika una ujasiri. Ndio maana mwanamke kama dada yangu ameweza kukupenda. Ayubu mpatie hatamu Hamza”
Ayubu bila kusita alifanya kama bosi wake alivyosema na kumpatia Hamza kamba za farasi ile. Lakini Hamza hakujisumbua hata kupokea kamba zile na badala yake alimbeba Yulia.
“Naendesha farasi haina haja ya hizo kamba”Aliongea na kauli yake ilimshangaza Yulia na wengine.
“Una uhakika , hii farasi ni kali kama simba!?”Aliongea Ayubu.
Hamza alicheka kidogo na kisha akiwa ameshikilia Yulia , hatua moja tu alikuwa asharuka na kwenda kutua kwenye mgongo wa farasi ile nyekundu.
Ayubu haraka haraka aliachia zile kamba na kuiachia huru , huku akirudi nyuma na kukaa mkao wa kumlinda bosi wake.
Farasi ile mara baada ya kuhisi kuna mtu katua kwenye mgongo wake , ilionyesha makeke yake kwa mara nyingine kutaka kumshusha Hamza na Yulia chini. Hata hivyo Hamza hakukasirika , aliendelea kukaa juu yake huku akiiangalia kwa macho makali yenye nguvu ya mkandamizo.
Msisimko wa kimkandamizo ambao Hamza alikuwa akiupeleka kwa farasi ile ni mambo aliokuwa ameyafanya kwa kipindi chote cha kuzaliwa kwake , alikuwa akivuta kumbukumbu za matukio ya hatari alioyafanya , iwe kwenye vita au kwenye misheni na kadri alivyokuwa akiikodolea ile farasi macho ni kama alikuwa akionyesha nini maana ya kuwa mtu hatari na ile farasi ilionekana kuona kitu katika macho ya Hamza na kushikwa na hofu.
Wanyama wako sensitive zaidi kuliko binadamu , hususani mbele ya watu waliofunikwa na vivuli vya dhambi. Wanyama wanakuwa sensitive kwasababu ulinzi wao binafsi upo katika hisia zao na sio kwenye macho.
Hamza mara baada ya kuvua helmeti la upole alilokuwa amevaa na kuuvika ule uhalisia wake aliokuwa nao miaka kadhaa iliopita , farasi hio yenye kiburi hatimae ilimchukulia kama kiumbe hatari zaidi.
“Chii.. chii!!”
Ile farasi iliishia kukoroma kidogo tu na kisha ilishusha kwato zake chini bila ya kusogea.
Yasin , Ayubu , Bertha na wale wachina walionekana kutoa macho , huku wakihisi ubaridi kwenye migongo yao wakati Hamza akirukia farasi ile , ila kilichowaacha na butwaa ni mara baada ya kuona ile farasi ikitulia .
Hamza aliipiga tumboni ile farasi na miguu yake kwa pamoja na palepale ilianza kutembea kwenda mbele kwa adabu kabisa. Hamza aligeuka kulia na ile farasi pia ilifanya hivyo hivyo.
Yulia mwanzoni alihisi ni ajabu , lakini mara baada ya kuhisi mabadiliko ya muonekano wa Hamza , alionekana kuelewa kilichotokea na alijikuta akishindwa kujizuia na kumwangalia Hamza.
“Wewe ni hatari mno , ni watu wangapi umeua?”Aliongea Yulia na muda ule Hamza alirudi katika hali ya kawaida na kisha alimuweka Yulia vizuri mbele yake.
“Mswali gani hayo , unaweza kweli kuwa na mtu kama mimi?”Aliongea Hamza.
“Ngumu kusema sasa hivi , unajuaje , pengine naweza kukupenda na kuanza kukufauta kama mbwa au kifaranga”
“Unayajua hata mapenzi yalivyo?”Aliongea na Yulia alisogeza mdomo wake karibu na sikio la Hamza na kumnong’oneza.
“Wewe ndio unapaswa kujiuliza , je katika moyo wako ulishawahi kujali kuhusu hisia zangu mpenzi? Najua tokea mwanzo ulivyochukua hatua ya kunisogelea , hukutegemea mapenzi ya dhati kutoka kwangu , bali ni kwasababu nina kitu unachotaka. Nakuona kama kaa nyamizi anaetafuta gamba , baada ya kupata na kuona halimtoshi au muda wowote anapoona zuri zaidi anaachana na la mwanzo na kuchukua jipya. Kama mimi ni gamba ambalo unahitaji kwa muda , kuna haja ya kujali hisia zangu kwako?”
Hamza aliishia kuangalia macho ya mwanamke huyo mrembo na kupepesa kwa sekunde , hakujua ni namna gani anapaswa kujibu. Hio ni kwasababu ni kweli kabisa mahusiano yao yalianzia kisiwani Chole , lakini licha ya siku ile hakuwahi kufikiria mahusiano yao kwa uzito kabisa . Kama isingekuwa Yulia kumtega na Herbert na kisha kumkasirisha na kupelekea kupatwa na majanga na kisha kulipa kwa kufanya nae mapenzi hakufikiria sana , lakini mara baada ya Bertha kuumia na kuona Yulia akiwa na wasiwasi , Hamza aliona pengine ipo nafasi ya kumponyesha mwanamke huyo na kumfanya awe na hisia kama watu wengine.
Muda huo sasa Hamza hakujua hisia zake kwa Yulia ni za namna gani , ni za mapenzi au za kutaka kujaribu kumfanya mwanamke huyo kuwa na hisia.
Yulia mara baada ya kuona Hamza amenyamaza pasipo kujibu , aliishia tu kucheka na kisha aligeuza uso wake na kumwangalia mdogo wake Yasin.
“Shukrani kwako mdogo wangu , hii farasi inaleta hisia tofauti sana. Mimi dada yako nimepokea zawadi hii”
Yasin aliishia kulazimisha tabasamu huku akioneysha ishara kwamba sio kitu.
Hamza aliendesha farasi na kwenda mbali zaidi na kundi hilo la watu na muda ule ndio Yulia alipata uhuru wa kuongea.
“Ulisema utanisaidia kuimiliki familia ya Wanyika na nguvu yake yote , ni kweli?”
Hamza alikuwa akifikiria kuhusu maneno mengine ambayo Yulia aliongea na mara baada ya kusikia kauli hio alijikuta akishindwa kujizuia na kutoa pumzi nyingi.
“Unataka kuongea nini?”
“Yasin ndio mshindani wangu mkuu , ingawa nimefanya vitu vichache vizuri kwa nchi , ndani ya ukoo wangu , nilichofanya ni kwa ajili ya nafsi yangu mwenyewe na sio kwa manufaa ya familia nzima. Upande wa Yasin amekuwa kidete kwenye kupanua biashara za familia katika masoko ya kimataifa. Na ndugu wengi waliopo kwenye bodi wanampa sapoti kubwa”
“Nataka unisaidie kumuua Yasini , hakikisha unafanya kisiri siri na hakuna mtu atakaejua kama nahusika , ukifanikisha , utakuwa umenisaidia jambo kubwa sana”Aliongea Yulia akiwa siriasi.
“Hata kama ni mtoto wa mjomba , lakini bado ni binamu yako kwa damu kabisa si ndio, hajakufanyia hila yoyote kwanini unataka kumuua?”Aliongea Hamza.
“Katika kupambania madaraka ndani ya familia , hakuna undugu. Mimi wazazi wangu wote wamekwisha fariki na ndani ya familia nipo mimi kama mimi , kama bado nataka kusimama lazima niwe kiongozi”
“Kwanini unataka kuwa kiongozi wa familia ya Wanyika , kwa akili zako hata kama sio kiongozi wa ukoo bado unaweza kuwa na nafasi kubwa katika idara ya sayansi na teknolojia ndani ya nchi ya Tanzania na hio inaweza kuwa nguvu yako tosha na nchi ndio ingekulinda na hakuna mtu yoyote angekugusa hata awe mwanafamilia”
“Kichwa kikubwa ila ubongo mdogo”Aliongea Yulia akisonya.
“Hey ! Usidhani kwasababu ni mpenzi wangu siwezi kukushikisha adabu, ukiendelea kuongea mbovu nitakupiga makofi ya makalioni “
“Nimesema hivyo sio kukutusi , bali kwasababu hufikirii mbali katika mtazamo wangu , hivi ushawahi kujua nipo katika hatari kubwa kiasi gani?”
“Unamaanisha nini?”
“Unadhani mimi kujihusisha na Earth Axis ndio tiketi yangu ya kujikinga na hatari?. Ngoja nikuambie tu tunaweza tukawa nyuma katika maendeleo ya sayansi na teknolojia , lakini haiwezi kuwa ngumu kwa nchi kutafuta mtu mwingine kuifanyia utafiti na kutafsiri taarifa zake , tupo nyuma kimaendeleo tu ila hatupo nyuma kiakili , kama mimi nimepatikana basi wengine wanaweza kupatikana pia. Sio kwamba hawawezi ni kwasababu tu ni kwamba mimi tayari washanipa kazi na wanataka kulinda taarifa ndio maana hawawezi kuruhusu kila mtu kujaribu. Hata kama nikifa leo au kesho watatafuta mtu kama mimi mwingine tu , wanaweza wasimpate mrithi wangu kesho , kesho kutwa au miaka mitano ijayo lakini mwisho wa siku lazima atapatikana tu. Nchi yetu sasa hivi tumetoka katika kuiendesha kwa manufaa yetu binafsi na tumeimarika kifikra kuangalia ni kipi ambacho nchi inafaidika na viongozi kupitia Malibu wamejengewa mtazamo huo , hivyo mtu yoyote kwasasa mbele ya maslahi ya taifa ni nyenzo tu ambayo inaweza kuachwa ikipoteza faida au nyenzo nzuri zaidi ikitokea. Mimi natumika tu hapa kwasababu ya akili yangu na kadri ninavyoendelea kutumika ndio thamani yangu inavyozidi kupungua. Unadhani watanifanya nini kama wakishaona hawanihitaji tena huku uwepo wangu ni tishio kwa usalama wa nchi?”
Hamza mara baada ya kusikia maelezo hayo moyo wake ulitetemeka .
“Unamaanisha wewe ni kama bomu?”
“Inaweza isiwe hivyo lakini sio mbali na unachomaanisha. Kwangu mimi kuna njia mbili tu naweza kuzichagua. Ya kwanza ni kuwa kiongozi wa familia , nikiwa kiongozi maana yake nakuwa mkuu wa Deepstate ambae naiongoza nchi nyuma ya pazia , pili kukubali kuendelea kufanya kazi kwa ajili ya serikali na kukosa uhuru wangu na kuishi maisha yangu yote kama mfungwa licha ya mfannikio makubwa nitakayofanya”
Hamza alijikuta akivuta pumzi nyingi iliochanganyika na harufu ya bahari, kwa namna Yulia alivyoongea ni kama sasa ameweza kugundua mambo sio mepesi kama alivyokuwa akichukulia.
Ilikuwa kweli kabisa , kipaji ni kama upanga ukatao kuwili, kipaji na nguvu ya kimadaraka ndio huonekana. Kama Yulia hatoweza kuwa kiongozi wa familia , basi kampuni ya Prima itachukuliwa na mtu mwingine. Isitoshe Prima haikuwa kampuni ya Yulia bali ni kampuni ya Familia na alipewa uongozi kwa ajili ya kulinda kile anachokifanya nyuma ya pazia katika kufasiri siri za Earth Axis.
Sasa kama Yulia atapoteza nafasi yake kama mwenyekiti wa kampuni maana yake atabakiwa kuwa na cheo tu cha mkuu wa idara ya utafiti na mwanajeshi. Kwa maana hio Yulia hatoonekana uraiani tena na maisha yake yote yatakuwa katika taasisi akitii maagizo ya nchi kwa utiifu kama sheria za kijeshi zinavyomtaka na akikengeuka anazimwa haraka.
“Kama siwezi kuwa kiongozi wa ukoo , basi sitokuwa na natasi tena ya kusimama ndani ya nchi hii na kujilinda , mimi mwenyewe na uhuru wangu. Yasin anajua nguvu yangu na akishapata nafasi hawezi kunivumilia na ikifikia muda huo kitu pekee nitakachoweza fanya ni kuuza uhuru wangu na kuacha nchi ndio inilinde. Naweza kusema nitoroke na hela nilizokuwa nazo nikaishi mbali , lakini hakuna ambae ataniacha niwe salama watanitafuta na kuniua popote pale”Aliongea Yulia .
Hamza aliishia kumwangalia mwanamke huyo kwa macho yasioelezeka akionekana kuwaza pia na kisha alitingisha kichwa kwa ishara ya kukataa.
“Sitokusaidia kumuua mdogo wako”
“Kwanini , si ulisema unakwenda kunifanya kiongozi?”
“Kwasababu nikifanya hivyo , hautokuja kuelewa hisia za ubinadamu zilivyo”Aliongea Hamza.
“Naona bado unaniamini sana , kwahio unadhani nitatoa chozi nikishapatwa na hisia za kibinadamu, inasikitisha kwasababu pengine muda huo nikiwa na hisia nitakuwa nishapoteza uhuru wangu tayari”
“Haiwezekani , siwezi kuruhusu itokee”Aliongea Hamza.
“Kivipi! Utaweza kupigana na nchi kwa ajili yangu ? Haha..acha hizo bwana , usiniambie unao uwezo huo au upo tayari? Mbele yako unachopendelea zaidi ni mwonekno wangu , pengine miaka kumi au ishirini ijayo nitakuwa nimepoteza mvuto na ukaniacha halafu nitafanya nini?”Aliongea kwa kejeli.
“Yulia kwanzia sasa unapaswa kuzingatia jambo moja tu”Aliongea Hamza kwa usiriasi.
“Jambo gani?”
“Nifanye nikupende”Aliongea Hamza akishikilia moyo wake na kauli ile ilimgandisha Yulia maana ni kama hakutegemea angeongea hivyo.
“Ili mradi utakuwa mwanamke ambae nakupenda kweli , hata kama itanipasa kuwa adui wa dunia kwa ajili yako , siwezi kusita na hakuna wa kunizuia”
Yulia aliishia kumwangalia Hamza uso wake wa kimashambulizi na alijikuta akimeza mate mengi , alishikwa na hali ya ukimya na kutokujua aongee nini. Walikuja kushitukia farasi imegeuka na kuwarudisha walipotoka.
“Inashangaza sana!”Aliongea Yasin huku akipiga makofi.
“Hii ndio mara yangu ya kwanza kuona mbinu ya namna hii ya kutiisha farasi”Aliendelea kuongea huku wale wachina pia wakitingisha kichwa.
“Sijawahi kufundisha farasi , ila nilichokifanya ni kuipa woga. Farasi ni moja ya wanyama wenye akili sana na wanajua ni wakati gani wa kuhisi woga. Ukweli ipo hivyo hivyo hata kwa binadamu. Muda mwingine binadamu anaweza kujihisi sio muoga , ila ukweli ni muoga ila ujinga tu umemjaa”Aliongea Hamza na kauli yake ilimfanya Yasin kucheka.
“Kweli kabisa, watu wanapaswa kuheshimu moyo unachowaambia. Ni kama nilivyotarajia kwa Bro Hamza mtu jasiri aliefanikisha hata kumuua mtoto wa Mzee Kijazi” Kauli hio ilimkumbusha Hamza alivyomuua Herbert Kijazi na kumuacha Himidu kushughulikia kutuliza familia ya marehemu.Ila hata hivyo hakutaka kufikiria sana na alimgeukia Yulia.
“Twende sehemu iliotulia na nitakutambulisha kwa huyu Bro niliekuja nae”
Yulia alikuwa ashamuona Zade kwa muda mrefu akiingia katika eneo hilo na Hamza. Ila kwasababu Hamza hakuongea chochote hakutaka kuuliza.
“Sawa , Yasin mdogo wangu sitokupa kampuni kwasasa , unaweza kumchukua Bertha tu muondoke nae kwasasa”Aliongea Yulia na kisha aligeuka na kuwapa ishara Hamza na Zade kumfuata.
Bertha kusikia kauli hio , alipatwa na furaha kwa kuona ndio muda sahihi wa kutoka out na mpenzi wake.
Kuhusu Yasin , alimwangalia Hamza na Yulia wakiondoka na uso wake ulizidi kujawa na ukauzu na muda ule simu yake ilianza kuita na aliitoa na kuangalia jina la mpigaji na kutoa tabasamu mara moja.
“Kanali Dastani, wakati sahihi kabisa!!”Aliongea huku akiwa na tabasamu la kejeli akiendelea kuwaangalia Hamza na Yulia wakitokomea huku simu ikiwa sikioni.
Hamza alifuatishana na Yulia mpaka ndani ya ofisi lakini kabla hajaongea chochote , Yulia alimgeukia Hamza.
“Nielezee kwanza , ni taarifa gani za kitafiti za Saidi ulizonipatia?” Hamza mara baada ya kusikia swali hilo alishangaa.
“Nini kimetokea kwenye hizo taarifa kwani?”
Comments