Yulia aliishia kumwangalia Hamza na mwonekano wa macho yasiokuwa na furaha.
“Una uhakika ulikopi hizo taarifa kwenye tarakishi yake?”
“Ndio”
Hamza alikuwa na uhakika , ingawa hakuwa mtaalamu wa masuala ya kompyuta, lakini kukopi taarifa halikuwa tatizo kwake.
“Kama ni hivyo basi Saidi hakuwahi kuweka taarifa za tafiti zake kwenye tarakishi”
“Unataka kusema kwamba taarifa nilizokopi kwenye tarakishi hazikuwa teknolojia ya kutengeneza maroboti ya kibailojia?”
Hamza alionekana kushangaa , mwanzoni alijua Yulia atakuwa amezifanyia kazi taarifa hizo na kuja kwake hapo angepata majibu kumbe zilikuwa sio sahihi.
Kusikia taarifa hio , Hamza hakujua awe na furaha au awe na wasiwasi , alihisi furaha kwasababu Yulia kukosa taarifa hio ingemzuia kufanya mambo ya hatari, lakini kilichompa wasiwasi ni kwamba kama Saidi atarudi na hakuna taarifa zozote juu ya tafiti hizo ingekuwa ngumu zaidi kudili na Saidi.
“Huyu Saidi niseme tu , anao uwezo. Hii inamaanisha taarifa zote amezikariri , ili ziwe salama zaidi”
“Usimuwazie sana , una Earth Axis tayari , huna haja ya kuwazia teknolojia za Saidi . ngoja kwanza nikutambulishe. Huyu ni Braza wangu , jina lake anaitwa Zade Maduli. Tafuta namna ya kumpa nafasi ili aweze kukupa ulinzi masaa ishirini na nne , itakuwa vizuri zaidi akiwa undercover”Aliongea Hamza na kumfanya Yulia kumwangalia Zade.
“Kwanini ghafla tu ukaamua kuniandalia bodigadi, tayari yupo Bertha , ijapokuwa simpendi , lakini huyu mtu wako ana nguvu kumzidi Bertha kweli?”
“Sio mtu wangu , jina lake anaitwa Zade na anayo kila sifa”
“Mh! Kwahio unawaswasi na usalama wangu sana ndio maana ukaniandalia mtu wa kunilinda?”
“Wewe ni mpenzi wangu , hivyo ni jukumu langu kuhakikisha usalama wako. Nimeingia katika mgogoro na waumini wa Sinagogu na nguvu yao imegeuka kuwa kubwa kuliko nilivyofikiria. Ili kujilinda mwenyewe napaswa pia kulinda watu wanaonizunguka”
Yulia mara baada ya kusikia maelezo mafupi ya Hamza alionekana kuelewa.
“Kama ni hivyo basi ngoja nitamuona , kwanzia sasa utakuwa unanifuata pamoja na Bertha , lakini hakikisha usiigize anachokifanya Bertha”
“Madam , jina langu naitwa Zade”Aliongea Yule ninja kwa ukauzu mara baada ya kuhisi dharau kutoka kwa Yulia.
Hamza mara baada ya kumpa maelezo machache Zade alipanga kuondoka , alipanga kuonana na Eliza pamoja na Prisila ili kuwapatia zawadi zao.
“Hamza kuna harambee na mnada kesho kutwa , vipi na wewe unaenda?”
“Harambee na mnada , ni wa nini?”
“Kwani Regina hajakuambia?”
“Mke wangu hajaongea chochote , kwani vipi?” Yulia mara baada ya kusikia hivyo alionekana kupatwa na hali flani hivi kama mtu alielewa jambo na kisha akaongea.
“Nadhani alifanya makusudi kutokukuambia..”Aliongea na kuanza kumwambia kuhusu Mnada huo pamoja na Harambee.Na Hamza mara baada ya kusikiliza maelezo ya Yulia hatimae alionekana kuelewa.
Kumbe kila mwisho wa mwaka wafanyabiashara wakubwa ndani ya jiji la Dar es salaam , hukusanyika pamoja kuchangishana hela pamoja na kufanya mnada ambao ungesaidia katika misaada ya watu wasiojiweza. Mnada huo pamoja na Harambee hufanyika kila mwisho wa mwaka mara moja tu.
Kushiriki katika mnada huo ni moja ya sehemu ya kujijengea taswira na heshima kwa jamii. Ni mnada ambao mara nyingi huhusisha kupiga mnada wa vitu vya watu wa kawaida, iwe ni wasanii au wabunifu , huleta bidhaa na kisha hupigwa mnada kununuliwa na matajiri.
Vitu hivyo havina thamani sana kwa matajiri hao , mara nyingi ni kama utaratibu tu au namna ya kutoa msaada , lakini malengo makubwa pia ni kuhimiza wabunifu na wasanii kuongeza juhudi pia , kuliko ile kutoa hela moja kwa moja bila ya kufanya kazi. Hivyo ni mnada ambao ni maarufu mno.
“Regina anashiriki pia kila mwaka , tena kawaida kwasababu nyie ni wanandoa unapaswa kushiriki nae , lakini kwasababu hajakuambia labda hataki kuongozana na wewe au hataki nikuone”Aliongea Yulia huku akicheka.
“Sio lazima iwe kweli , pengine hajapata tu muda wa kuniambia”
“Basi kama hatokuambia , unaonaje tukishiriki pamoja?”Aliongea huku akiwa na mwonekano wa kichokozi.
“Huna haja ya kunichokoza , siwezi kuthubutu”
“Mhmh , nilijua huwezi kuthubutu”Aliongea Yulia huku akimwangalia Hamza na macho yaliojaa masikitiko
“Unaweza kwenda, tutawasiliana kukiwa na lolote , nataka kwanza nidili na huyu Yasin”
Hamza hata yeye pia alitamani kumfurahisha Yulia , lakini ingekuwa ngumu kwenda nae yeye na kisha akamuacha Regina , ingekuwa ni ushenzi wa hali ya juu sana.
Hamza muda wote wa mchana aliutumia kugawa zawadi , alianza kumpelekea Prisila ambae alifurahi kumuona na pia kupewa zawadi , isitoshe ilikuwa zawadi ya pili kutoka kwa Hamza. Ya kwanza ilikuwa ni gauni ambalo hakuwahi kuwazia kulinunua.
Hamza mara baada ya kufika kwa Eliza na kumpelekea zawadi , mrembo huyo alifurahi , sio kwasababu ya thamani kubwa ya zawadi hizo bali Hamza aliwakumbuka ndugu wazazi na ndugu zake kuwanunulia zawadi.
Eliza alimwabia Hamza ndugu zake wangekuja Dar kwa ajili ya sherehe ya Christmas na kama atakuwa na muda anakaribishwa.
“Nitaangalia itakavyokuwa , ijapokuwa naweza kuwa bize sana siku hio , ila nitaangalia namna ya kupata chakula pamoja”
Ukweli ni kwamba ndugu wa Eliza walitamani sana kumuona Hamza , hio yote ni kutokana na msaada mkubwa alio wapatia , walikuwa wakijua Hamza ana mke hivyo waliona isingekuwa sahihi kumwambia Eliza ampeleke Iringa na badala yake waliona wao ndio waje wapate nafasi ya kumuona.
Kati ya wanawake wote Hamza hakupanga kupelekea zawadi ni Irene, kwasababu hisia zake kwa mwanamke huyo bado hazikuwa zimeeleweka bayana. Mara baada ya kufika nyumbani alimpigia simu na kuongea nae na simu na kisha kukubaliana kuonana siku inayofuata. Mara baada ya kukata simu alijua Regina alisharudi kazini hivyo alitoka chumbani na kushuka chini.
Wakati anashuka , aliweza kumsikia Regina akiongea na Shangazi kwa furaha jikoni.
Regina alikuwa hata hajafika chumbani kwake na kubadilisha na alionekana akiongea mfululizo.
“Shangazi , nishaanza kupatwa na msisimko kabisa , kumbe kuvuna nishati kunamfanya mtu kujisikia vizuri hivi , yaani nahisi mwili wangu wote ni kama umeshikwa na hali ya ubaridii na naweza kusikia pumzi zangu”
Shangazi aliekuwa bize kuandaa chakula aliendelea kumsikiliza Regina na tabasamu tu.
“Ni hatua nzuri , hapo unachukuliwa umeingia rasmi katika hatua ya nusu mzunguko. Nadhani nafsi ya bibi yako inakuangalia na kukuongoza”Aliongea Shangazi akiwa na furaha kubwa.
Shangazi pia ni mtu wa Bondeni , kama Regina akiweza kuvuna nishati na kupanda levo , ingekuwa rahisi kwao kurudi kwenye asili yao na kupokelewa.
“Wife ndio kwanza upo kwenye daraja la nusu mzunguko . Safari iliopo mbele yako ni ndefu mno, huna haja ya kufurahi namna hio”Aliongea Hamza alieegamia mlango wa jikoni.
“Unadhani kila mtu ana kipaji kama wewe! Sijawahi kuwazia katika maisha yangu nitakuja kuhisi hivi , watu wenye nishati za mbingu na ardhi niliwaona kama watu waliopatwa na bahati . Sasa na mimi nimepanda levo kwanini nisifurahi ?”
“Haha , Regina , umejaaliwa akili nyingi , nina uhakika ukiendeleza juhudi utakuwa mtaalamu hapo baadae. Kuhusu mwisho utakaofikia ni ngumu kutabiria kwasasa”Aliongea Shangazi.
Hamza alisogea na kumshika Regina mkono na kupima msukumo wa damu na macho yake yalionyesha mshangao , ilionekana ni kweli , nguvu ya msukumo wa damu ilionekana kuwa mara mbili na mwanzo.
“Hili andiko linaonekana kuwa na nguvu kubwa kweli , yaani ndio kwanza upo levo ya nusu mzunguko lakini mzunguko wako wa damu umeimarika kiasi hiki?”
“Ni urithi wa babu na bibi walioniachia , halafu sasa hivi baada ya kujihisi hivi nimegundua naweza kufanya kitu cha kimaajabu”
“Kitu cha kimaajabu , unamaanisha nini?”Aliongea Hamza kwa mshangao na haikuwa kwake tu hata kwa Shangazi pia.
Regina alichukua glasi na kisha alimimina maji ya moto kwenye ile glasi na kisha akaishikilia kwa nguvu , ndani ya sekunde chache tu yale maji yalianza kupoa kwa kasi ya ajabu sana na kuwa ya baridi kiasi cha kuelekea kushikwa na ukungu wa ubaridi.
“Mnaonaje haya maajabu , kipindi cha jua kali naweza tu nunua Strawberry popote pale na kuzipa baridi na kula na pia naweza kushikilia Ice cream kwa muda mrefu bila ya kuyeyuka. Ni rahisi sana mnajua hadi nashangaa”Aliongea Regina kama vile anataka kuruka ruka.
Hamza na Shangazi walijikuta wakiangaliana na kuonekana wakiwa kama wamechanganyikiwa.
‘Wife , umewezaje?’
Hamza alishindwa kuelewa kabisa na kujikuta akimwangalia Regina kwa shauku. Regina mara baada ya kuona walivyochanganyikiwa alionekana kujivunia zaidi.
“Mimi sielewi , nilikuwa nikiwaza jambo flani hivi ila ghafla tu yale maandishi ni kama yamejitafsiri katika kichwa changu na kuna sauti inaniambia nihisi hivi kwenye moyo wangu na mikono yangu itaonyesha matokeo na ndio kilichotokea”
“Lakini ndio kwanza upo levo ya nusu mzunguko , kuweza kutoa nishati ya mbingu na ardhi inaweza fanywa na mtu aliefikia levo ya nafsi na kupata ufunuo. Wapo hata baadhi ya watu wamefikia levo ya nafsi lakini hawajawahi pata ufunuo wa namna ya kutoa nishati zao nje zaidi ya kuzitawala ndani ya miili yao tu”
Hamza hakuelewa , hajawahi kusikia mahali popote pale katika mafunzo ya nishati , mtu akiwa katika levo ya nusu mzunguko kupata ufunuo.
Ikumbukwe kwamba mafunzo ya nishati ni kama mtu anavyofanya maombi , kadri uvyosali ndio unavyozidi kunyonya nguvu ya kiroho na kukuwa kimadaraja , ukifikia daraja flani ndio sasa unafunuliwa vitu ambavyo hukuwahi kufikiria. Sasa Regina ambae ndio kwanza tu ameanza kuingia katika daraja la nusu mzunguko inawezekana vipi akapata ufunuo haraka hivyo. Hata Shangazi alionekana kushangaa.
“Regina mbinu unayojifunza ndio bibi yako alijifunza pia , lakini ulichofanya ni tofauti kabisa na bibi yako , alikuwa akitoa nishati lakini haikuwa ya ubaridi mkali kama wewe”Aliongea shangazi.
Hamza hata yeye aliweza kuthibitisha wasiwasi wake , alichotoa Regina kilionekana kukosa uhusiano na ufunuo kabisa wa kinishati. Kwasababu siku zote nishati ina nguvu mno kiasi kwamba ili mtu ahimili kutoa lazima afikie daraja la ukamilisho wa mwili au ukaidi wa asili , kitu ambacho Regina alikuwa mbali sana. Lakini hata hivyo Hamza alifikiria tofauti , aliona pengine ni kama Nyakasura tu, watu waliozaliwa tayari na uwezo, ambao unahitaji kitu kama switch tu kuamsha.
Hamza aliona kama ni kweli basi anachofikiria Regina ni ujinga kutaka kutumia uwezo huo kuzipa baridi Strawberry , kwasababu kama uwezo upo ndani yake mara nyingi ni hatari kama mtu hawezi kuudhibiti na anaweza kuua mtu bila kukusudia.
“Mbona mna hali ya mashaka usoni , kuna kitu nimekosea?”
“Regina kuna hali mbaya unajisikia mwilini?”Aliongea Shangazi akimwangalia Regina kwa wasiwasi.
“Hapana najisikia vizuri tu , mwili wangu ni mwepesi sana”
“Wife kwasasa kuna uwezekano wa aina mbili , kwanza labda ile pete ndio inaonyesha athari zake kwako au mwili wako wenyewe ulikuwa na uwezo ambao umeanza kujionyesha wenyewe baada ya kuanza mafunzo. Kwasasa hakuna uwezekano wa kujua nini kinakutokea , kama utaendelea kuhisi hakuna tofauti katika mwili wako , basi unaweza kuendelea kujifunza”
Hamza alifikiria mambo mawili kwa wakati mmoja , nishati ile iliotoka katika pete kumponya Regina ilikuwa pia na nguvu ya ubaridi , lakini hakutaka kuamini moja kwa moja kama ndio imemfanya Regina kuwa na uwezo huo , pengine Regina mwenyewe ndio alikuwa na uwezo ambao labda alizaliwa nao.
Regina mara baada ya kusikia maelezo ya Hamza alionekana kufarijika , isitoshe alimwamini Hamza kwasababu alikuwa ni Gwiji.
“Vyovyote vile inaweza kuwa na faida kwa Regina na kwa familia kwa ujumla , leo naenda kupika chakula kizuri kwa ajili ya kusherehekea”Aliongea Shangazi.
“Shangazi wewe unapika chakula kingi , huna haja ya kuongezea sana”Aliongea na kumfanya Shangazi kucheka na Hamza pia.
Wakati wa chakula cha usiku Hamza alimwambia Regina atatoka kesho kwenda kuonana na Irene. Hakutaka tu kuondoka kimya kimya , Regina kusikia hivyo uso wake palepale ulionyesha hali ya kutokufurahi.
“Niko bize na kazi, lakini wewe una hadi muda wa kusindikiza watu matembezini , hata hivyo sitaki kujali unachofanya , unaweza kwenda tu” Aliongea Regina kwa sauti hafifu.
Hamza mara baada ya kuona amemfanya mwanamke huyo kutokuwa na furaha , alijikuta akitoa tabasamu la haya.
“Mke wangu , unaonaje baada ya chakula twende tukatembee , tunaweza kwenda kuangalia movie na miwani za teknolojia mpya ya Meta?”
Hamza alikumbuka hajatoka out sana na Regina , lakini alishawahi kwenda na Dina na Eliza kuangalia filamu , lakini muda huo alikumbuka kulikuwa na uzinduzi wa teknolojia mpya ya miwani ya kampuni ya Meta ambazo zilikuwa zikitumiwa kwa mara ya kwanza katika moja ya ukumbi wa sinema Mlimani nchini Tanzania.
“Itakuwa vizuri Regina. Mnaweza kwenda kuangalia movie , isitoshe muda bado mapema na ukikaa nyumbani hupumziki zaidi ya kufanya kazi”Aliongea Shangazi haraka kumpigia pasi Hamza.
Regina kusikia hivyo aliguswa moyoni , ijapokuwa kuangalia filamu kwa Tanzania ilikuwa sio maarufu sana kama date , lakini Regina ambae alikuwa na exposure alitamani kujaribu pia.
Mara yake ya mwisho kwenda kuangalia sinema , ilikuwa nchini Marekani na alienda na marafiki zake waliokuwa na wapenzi wao huko Las Vegas , ila tokea hapo hakuwahi tena baada ya kuchukua hatamu ya uongozi wa kampuni.
“Ni wapi tunaenda kuangalia na filamu gani kama sio nzuri siendi?”
“Tunaenda Century Cinemax Mlimani City ndio pazuri , filamu inaitwa the Descent”Aliongea Hamza na Regina alitingisha kichwa.
Hamza mara baada ya Regina kukubali alitamani kutoa kicheko cha furaha , lakini alijifanyisha tu kushangaa.
“Wife mbona hata huulizi ni filamu inayohusiana na nini? Si umesema kama ni mbaya huendi?”
Regina alijikuta akishangaa na kukumbuka alikubali haraka haraka bila ya kufikiria.
“Jina ndio nimelipenda nimeona ni nzuri , kwani ni mbaya au? Basi tusiende”
“Ni nzuri , halafu napenda nikaiangalie na wewe mke wangu”Aliongea Hamza na tabasamu.
Baada ya chakula , Regina alibadilisha na kuvaa vazi la rangi ya gray na mkoba wa Prada mdogo. Kwa staili aliovaa hakuwa kama bosi wa kampuni kubwa kama ya Dosam , alionekana kama mrembo ambae amemaliza chuo na ndio anatoka date na mpenzi wake.
Uzuri wake haukuwa ule wa vipodozi , ulikuwa ule wa asili na ngozi laini iliotunzwa vizuri. Moja ya sababu ambazo zinamfanya Regina kuvutia ni silika yake ya ukauzu ni kama ilimwongezea hadhi ya mwanamke wa matawi.
Mara baada ya kuelekea gereji na Hamza kumuona Regina alikuwa akielekea moja kwa moja katika gari yake , almzuia haraka.
“Wife tunaenda date , haina haja ya kutumia gari la kuteka attention ya watu , tutumie ya mwonekano wa kawaida”
Regina aliishia kuitikia ‘ oh!’ na kisha alimfuata Hamza na kuingia kwenye Mercedenz S65. Haikuwa gari ya kawaida kithamani , ilikuwa gari ya kawaida kimwonekano pekee , ila ilikuwa ikigharimu zaidi ya milioni mianne za kitanzania mpaka mia sita kuingiza Tanzania.
Hamza aliendesha gari mpaka Mlimani City , mara baada ya kuingia na kuegesha gari , alitumia simu kununua tiketi haraka haraka.
Regina ilikuwa mara yake ya kwanza kuja Ml;imani kwa ajili ya kuangalia filamu , na pia alikuwa mgeni kwenye kutumia simu kama hivyo kununua tiketi.
‘Wife kuna siti maalumu za wapenzi , tuchukue hizi au za kawaida?”Aliongea Hamza.
“Ndio zikoje hizo za wapenzi?”
“Tunatenganishwa na watu wengine tunakuwa sisi tu yaani” Aliongea Hamza huku akimkonyeza.
“Wewe, unapanga kufanya vitu vichafu sio?”
“Wife vitu gani vichafu , wapenzi wakiwa wanaangalia filamu , ni kawaida kufanya vitu kama kukiss , kushikana na mengineyo , kwanini useme ni vichafu?”
“Ah! Kama ni hivyo basi siendi”
“Basi, basi mke wangu , hatutokaa pamoja , sitokukiss wala kukugusa , sawa?”
“Basi twende tu na hizo za wapenzi , nataka kujaribu kama wtu wengine”Aliongea Regina kwa sauti ndogo.
Hamza mara baada ya kusikia kauli hio alishangaa na kujiambia wanawake wapo kinyume nyume wanavyoongea.
Mara baada ya kupata tiketi zao walishuka na moja kwa moja walielekea mlangoni , wakati wakielekea ndani Regina aliona vinywaji flani hivi vilivyohifadhiwa kwenye shelf na vilikuwa na picha za mtu kama Zombie huku umbo lake likiwa sio la kawaida.
“Hivyo vinywaji ni shilingi ngapi?”
“Elfu kumi na tano tu dada”
“Kuna vyenye radha ya strawberry?”
Wakati Hamza akitaka kuuliza kwanini wameweka nembo za picha ya mazombie, alisogea mteja mwingine na kuongea kauli ambayo ilimshangaza Hamza kidogo.
“Dada chungu changu kimeachwa?”Aliongea yule mteja na Hamza palepale ni kama kuna suala lilichipua kwenye akili yake.
Comments