Worldless Book
“Nini kilichompata huyo msichana?”Lilikuwa swali la Hamza kwenda kwa Rhoda.
Mapigo yake ya moyo yalikuwa yakienda spidi mno kwa kuhisi jambo kubwa limempata Irene.
“Amechomwa mwilini na tawi la mti. Sasa hivi Bazo amemchukua kumuwahisha Muhasi , hospitali ya taifa”Aliongea Rhoda.
“Tawi la mti kwenye mwili wake!?” Hamza aliongea huku akihisi utosi wa kichwa chake ukianza kumuwasha.
“Ndio , kulikuwa na mtu aliekuwa amejificha kwenye bustani ya nyumbani kwao , wakati anataka kuingia ndani ya geti alimshambulia Irene kabla Bazo hajashituka”Aliongea Rhoda huku akionekana ni kama anataka kulia.
“Samahani sana Bro ..nimeshindwa kutimiza wajibu wangu”Aliongea.
“Haina haja ya kujilaumu , kama ni mtu mwenye uwezo ambae Bazo ameshindwa kumtambua , basi hakuna kitu ambacho angeweza kufanya. Naelekea huko hospitalini sasa hivi”
Hamza hakuongea neno lingine zaidi na palepale alikata simu na haraka sana alikimbilia nje.
Regina pia aliweza kusikia mazunguzo ya kwenye simu na alisita kidogo na kisha aliweka vitu alivyokuwa ameshikilia mkiononi na kumkimbilia Hamza nje.
Hamza alikuwa ndio anajiandaa kuendesha na ile anamuona Regina akiingia pia alijikuta akimwangalia.
“Na wewe unaenda?”
“Kama isingekuwa sababu yangu ungemsindikiza Irene kwenda nyumbani na asingepatwa na tatizo. Siwezi kukaa na kusubiri taarifa nyumbani kwa amani”Aliongea Regina wakati akifunga mkanda.
Muda huo akili ya Hamza ilikuwa katika hali ya kuchanganyikiwa na hakuwa na muda wa kujali ni kipi mwanamke huyo anafikiria. Hivyo aliwasha gari na kulitoa kwa haraka nje ya geti.
Muhasi ni moja ya hospitali kubwa ya taifa ndani ya jiji la Dar es salaam. Ingawa ilikuwa ni usiku lakini kulikuwa na madaktari bingwa wabobezi waliokuwa zamu.
Lakini hata kwa wale madaktari waliokuwa na uzoefu , walijikuta katika hali ya kiwewe mara baada ya kuona hali aliokuwa nayo Irene mara baada ya kuingizwa katika wodi ya dharula.
Ndani ya chumba hicho cha dharula , taa zilikuwa zikiwaka lakini hali ilikuwa kinzani.
Msichana aliekuwa amelazwa kwenye kitanda cha wagonjwa, madaktari mbalimbali walikuwa wameitwa kuja kumwangalia , lakini karibia wote walikuwa katika hali ya kutafakari namna ya kumuokoa.
Tawi la mti wa maua lilikuwa limemchoma Irene kuanzia tumboni na kusababisha damu nyingi kuonekana kupitia mgongoni.
Irene alikuwa amepoteza fahamu na sura yake ilikuwa imetapakaa damu.
“Mbona wote mmesimama tu bila ya kufanya chochote , harakisheni mumuokoe binti yangu”
Alikuwa ni Patrin Baba yake Irene alievalia suti nyeusi , akiwa anaingia ndani ya eneo hilo kama vile amepandwa na ukichaa , ilionekana bado alikuwa katika majukumu yake ya kazi wakati anapokea taarifa ya kujeruhiwa kwa binti yake.
Manesi kadhaa walionekana kushindana nae nguvu wakimwambia asiingie ndani na kuwapa madaktari muda wa kufikiria.
Nyuma yake alikuwepo bibi yake Irene aliekuwa amekaa kwenye viti , akiwa amefunika uso wake na mikono huku akionekana kulia chinichini.
Bazo alikuwa amesimama kando ya mlango akiwa katika hali ya majuto makubwa , kucha ya mkono wake ilikuwa imetoboa ngozi ya mwili wake na kufanya damu kumtoka.
Muda mfupi alifika mwanaume mwingine kwa spidi kubwa na kuzama ndani na kumwangalia msichana aliekuwa juu ya kitanda.
“Mnaota nini sasa?”Aliongea
“Prince!”
Bazo aliishia kuita na kumwangalia Hamza kwa sekunde kadhaa kisha akashusha kichwa chake chini kwa aibu.
Regina na Rhoda walifuatia na kumfuata Hamza ndani na mara baada ya kuona hali aliokuwa nayo Irene walijikuta wakikumbwa na hali ya wasiwasi.
“Hamza!” Aliita kwa jazba Baba Irene na kumsogelea Hamza kwa kasi.
“Wewe ndio umesababisha haya?! Umejingiza kwenye matatizo na kumsababishia binti yangu matatizo , si ndio?”
Hamza mara baada ya kuangalia uso wa Baba Irene uliokuwa katika majonzi , alijikuta akihisi machungu katika moyo wake. Hata hivyo haukuwa muda mzuri wa kulaumiana na kuelezana sababu ya kilichomtokea Irene, hivyo palepale alimkwida tai na kumwangalia usoni kwa macho ya usiriasi.
“Kama unataka binti yako kuendelea kuwa hai, unapaswa kunyamaza. Nataka kujua sababu na kwanini juu ya kilichomtokea kama ilivyo kwako pia”Aliongea.
Baba Irene alijikuta akihofia muonekano wa Hamza , aliishia tu kumeza mate na kisha akapiga hatua mbili nyuma.
“Kama binti yangu akipoteza uhai, nitakufanya ulipe na uhai wako “
Katika macho ya baba aliechanganyikiwa , ilikuwa ni wazi kabisa Hamza ndio aliemsambabishia Irene matatizo. Vinginevyo kwanini Hamza atume bodigadi wa kumlinda Irene kwa siri?.
Bibi yake Irene aliekuwa amekaa kwenye benchi , mara baada ya kumuona Regina alionekana kuonyesha hali isiokuwa ya kawaida katika uso wake , kama vile alikuwa katika hali ya maumivu.
Hamza alipiga hatua na kusogelea karibu na kitanda cha mgonjwa na mara baada ya kuchunguza hali yake , alionekana kushusha presha na kuanza kufikiria cha kufanya.
“Anazidi kupoteza damu , ondoeni kwanza huo mti”Hamza alionekana kufikia katika maamuzi.
“Wewe ni nani? Unajua ni hatari kiasi gani tukiuondoa huo mti sasa hivi? Tunaweza kumsababishia matatizo zaidi”
“Kwahio kama hamna mpango wa kuuondoa, mnasubiria afe kwanza. Kama hamna njia ya kumsaidia mgonjwa mnapaswa kunisikiliza mimi kwanzia sasa”Aliongea Hamza na kisha kwa hasira aliwaangalia madaktari hao mmoja baada ya mwingine.
“Nisikilizeni , tutachomoa hilo tawi na kisha tutafanya Diagnostic peritoneal Lavage”
Madaktari wale walijikuta wakiangaliana kwa maswali na kisha wakamwangalia wote Hamza.
“Wewe ni daktari?”Aliuliza mmoja wao. “Mkiendelea kunichelewesha na maswali yenu , msije kunilaumu nikiwa muuaji. Nitawaua wote kujiondolea vikwazo”
Kundi hilo la madaktari walijikuta wakitetemeka mara baada ya kusikia maneno ya Hamza na usiriasi uliokuwa katika macho yake. Na haraka walionekana kumwangalia aliekuwa ni kiongozi na alitoa ishara ya kutingisha kichwa na kisha kukubali kunyofoa tawi kutoka katika mwili wa Irene.
“Tutaanza hatua za kuondoa tawi kwenye mwili wa ngonjwa, andaeni damu kwa ajili ya kumuwekea , leta NS, sindano , na Scalpel”Aliongea Hamza.
“Damu ipo kwenye hifadhi , lakini vipi kuhusu kundi lake la damu?”Aliuliza Daktari kiongozi.
“Hatuna taarifa zake”Alijibu moja ya mhudumu wa afya wa masuala ya kumbukumbu za wagonjwa.
“Binti yako ana kundi la damu lipi?”Aliuliza Hamza akimlenga Baba Irene.
Baba Irene alionekana kushangazwa na hali ya kitaaluma aliokuwa nayo Hamza , hakutegemea alikuwa akijua maswala ya kitabibu , ila kwa haraka haraka alijibu .
“Sijui”
“Yaani wewe ni baba ila hujui mtoto wako ana kundi gani la damu?”Aliongea Hamza na Baba Irene aliishia tu kuinamisha kichwa chake chini kwa aibu. Ilikuwa ni moja ya ujinga uliokuwa kwa watanzania wengi kutojua makundi ya damu ya watoto wao na wao wenyewe, hali ambayo inapelekea ucheleweshwaji wa matibabu nyakati za dharula kama hizo.
“Haraka sana fanya utaratibu wa kumpima”Aliongea dokta mkuu wa zamu.
“Haikuchukua muda mtaalamu wa maabara alifika na kufanya vipimo na ndani ya dakika moja tu vilitoa majibu , maana kila kitu kilienda kidigitali.
“Ana damu group P na hatuna hifadhi ya damu hio kwenye benki yetu”Aliongea mtaalamu yule wa maabara akiwa pia katika hali ya mshangao kama vile kipimo kilikuwa kimekosea.
“Nini !”
Madokta wote waliokuwepo hapo , walijikuta wakiwa katika hali ya mshangao. Wengine walionekana hata hawakuwahi kusikia aina hio ya group la damu na kujikuta wakiwa katika hali ya maswali mengi.
Hamza aliishia kukunja ndita mara baada ya kusikia majibu hayo. Kundi la damu la aina ya P lilikuwa adimu sana kuonekana , ilikuwa ni sawa na kusema kati ya watu milioni kumi ni mmoja tu anaeweza kubahatika kuwa na kundi hilo la damu.
“Kama hatuna aina hio ya damu basi hatuwezi kumuongezea.Tunapaswa kufanya nini?”
“Haraka! Hebu ulizia kama katika mtandao wa taarifa shirikishi kuna hospitali ndani ya Dar es salaam , hata nje ya hapa kuna hifadhi ya damu ya kundi hilo”Aliongea dokta mkuu. Huku katika moyo wake alikuwa akiamini mgonjwa matumaini ya kupona yalikuwa madogo sana. Hata kama hospitali nyingine ingekuwa na damu hio mpaka utaratibu wa kuipata na kufikishwa hapo wangeshachelewa.
Baba Irene aliekuwa akisikia maelezo yote , nagoti ya miguu yalimlegea na alijikuta akipiga magoti chini bila ya kupenda.
“Naombeni mumuokoe mwanangu. Msaidieni binti yangu apone”
Muda huo Baba Irene hakuwa na ule mwonekano wake wa kijasiri kama mwanausalama , alikuwa ni baba halisia aliekuwa katika matatizo ya kuhofia uhai wa binti yake .
Hamza alijikuta pia akishindwa kuzikabili hisia zake, aliweza kuona kila sekunde iliokuwa ikipotea inapotea na uhai wa Irene. Alijikuta akishindwa kuamini kama hana uwezo wa kumsaidia Irene. Hamza alitamani kujipiga vibao vingi sana ili kupata muujiza wa kubadilisha kundi hilo la damu na kuwa la kawaida.
“Group langu la damu ni P”
Sauti kavu iliojaa ukauzu ilisikika kutoka nyuma ya migongo ya madaktari na kufanya mwili wa Hamza kuingiwa na ubaridi. Alijikuta akigeuka na kuangalia upande sauti ilikosikika.
Muonekano wa Regina ulikuwa sio wa kusomeka kirahisi , alionekana ni kama vile alikuwa katika mshangao lakini haukuwa mshangao.
Ukweli ni kwamba mara baada ya kumuona Irene akiwa juu ya kitanda na sura yake ilivyokuwa katika hali ya kutia huruma mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kwa nguvu mno.
“Wife! Una damu Group P?!”Aliuliza Hamza akitaka kuthibitisha kwa mara nyingine.
Lakini muda huo kabla ya Regina kujibu sauti nyingine ya mhudumu wa afya ilisikika.
“Kuna mtu mwenye kundi hilo la damu hapa nchini, ni taarifa kutokea hospitali ya Mayaya. Ni mwanamke anaefahamika kwa jina la Regina Samweli Dosam. Mkazi wa Dar es salaam”
Kwa kauli hio kila alichoongea kilitibitisha kauli ya Regina.
Kila mmoja alishikwa na butwaa , walijihisi ni kama vile Malaika alikuwa katika eneo hilo .
Yaani wanawake wawili wenye damu
zinazofanana kimakundi kuwepo kimiujiza katika eneo moja?.
“Inaonekana Mungu yupo upande wa mgonjwa”
“Imenishangaza mno!”Madaktari baadhi walioonekana kuwa wanafunzi walishangaa.
“Nilishapima damu yangu muda mrefu tu na ipo kwenye kanzidata,ni safi, mnaweza kutoa na kumsaidia mgonjwa”Aliongea Regina.
“Bosi Regina! Asante sana , asante sana , sitokuja kusahau hili maisha yangu yote”
“Baba Irene huna haja ya kunishukuru hivyo natoa mchango wa damu kama mtu mwingine tu. Kuokoa uhai wa mtu ni muhimu zaidi kwa mtu yoyote”Aliongea Regina.
Haraka sana watoa huduma walimchukua Regina na kumwandaa kwa ajili ya damu kutolewa na kuwekewa Mgonjwa.
Bibi yake Irene aliekwua ameketi kwenye kiti alionekana kuwa na hali isioelezeka katika uso wake na alijikuta akitokwa na machozi mengi zaidi.
Hamza mara baada ya kuona Regina kwa hiari yake kaamua kuchangia damu , alijikuta akikumbwa na wimbi la joto katika moyo wake.
Aliinua uso wake na kumwangalia Bibi yake Irene na alijikuta akiingiwa na hali ya ufumbuzi katika akili yake.
Hatimae mara baada ya mchakato wa kuchangia damu kukamilika na kuwekewa Irene . Hamza alianza mchakato wa kuondoa tawi katika mwili wa Irene.
Sekunde mti ule ulivyochomolewa , damu nyingi ilifyatuka kutoka kwenye jeraha.
“Anaonekana kwenda kufa , amepoteza damu nyingi sana , hata kama huyu dada amchangie damu haitotosha”Aliuongea Daktari.
“Niko sawa , mnaweza kutoa damu ya kutosha”Aliongea Regina aliekuwa amelala kitandani.
“Msije kufanya ujinga, Siwezi kumuona mke wangu anakufa kwa ajili ya kumuokoa Irene”Alionya Hamza.
Regina alijikuta akimwangalia mwanaume huyo kwa sekunde kadhaa na kisha akaongea.
“Vipi utafanyaje sasa?”
Hamza aligeuka na kuwaangalia madaktari na kisha akatoa maelekezo mengine.
“Tutatumia damu yake kupitia Renal Artery na kisha tutaipitisha kupitia Vein “
Mara baada ya kusikia maelekezo ya Hamza , madaktari wale walishindwa kumuelewa na kumfanya Hamza kutokuwa na jinsi na kuanza kuwalezea.
“Njamaanisha tutaitoa damu yake na kuirudisha kwa wakati mmoja ili kumfanya apumue”Aliongea.
“Inawezekana! Umejifunzia wapi hii mbinu? Sijawahi kusikia inafundishwa katika chuo chochote “Aliongea Dokta mkuu ambae pia ni profesa.
“Sitaki kusikia ujinga unaongolewa darasani hapa , kama unataka kujifunza jifunze , tupo kwenye dharula”Aliongea Hamza na wakati huo alikuwa akifanya kile alichokusudia.
Dakika chache mbele Hamza aliweza kufanikiwa kutatua tatizo la mzunguko wa damu na upungufu wake na kufanikiwa hatua za kumuokoa kwa wakati mmoja kwa kuzuia damu isiendelee kutoka.
Dakika chache mbele mara baada ya vipimo
(Physical sign’s) kurudi kawaida , haraka
alitolewa na kupelekwa ICU na Hamza hatimae alipumua.
Madaktari walioshuhudia kila alichokifanya Hamza , walijikuta wakimkubali mno kwa ubingwa wake , Hata Dokta mkuu alitamani kumuona Hamza akifanya kazi ndani ya hospitali hio na pengine kuwa profesa katika chuo chao.
Hata hivyo Dokta huyo mara baada ya kuweka pendekezo hilo , Hamza alimgomea.
Hamza alitoka mpaka kwenye Korido na kuwasogelea , bibi yake Irene, baba yake ,Roda Bazo na Regina ambae alikuwa amepumzika kwenye kiti kutokana na kutoa damu nyingi.
Mara baada ya hali ya Irene kutoka kuwa ya hatari , mambo mengi ambayo hayakuwa na umuhimu kuliko uhai , yalianza kupita katika vichwa vya kila mmoja kwa mara nyingine.
Hamza alimwangalia bibi yake Irene ambae alikuwa katika hali ya mawazo na kisha aliuliza ;
“Madam kwanini usituelezee ni kipi kinachoendelea hapa?”Aliongea Hamza na kumfanya bibi yake Irene mwili wake kumtingishika.
“Wewe ! Unamaanisha nini?”
“Naweza kuelewa kwanini watu wa Bondeni kutaka kumuua mke wangu , lakini kwanini Dosal na mwanae wametuma watu kumuua Irene huku Mathias Huge mkuu wa kitengo cha Binamu akitaka kumteka. Unataka kusema hujui sababu ya haya yote?”
“Unamaanisha nini!Kwamba kilichompata Irene ni kwasababu ya watu wa Bondeni”Aliuliza Regina aliekwua katika hali ya msahngao mara baada ya kusikia kauli ya Hamza.
“Wife nilitaka kukuambia , lakini sikupata nafasi.. Ni kama ulivyosikia watu waliomshambulia Irene wametumwa na Mzee Dosal na mwanae Suwi. Nadhani sasa unaelewa kwanini muda ule nilikwambia ni suala linalohusiana na wewe?”
Regina uso wake ulikumbwa na hali ya kutokuamini na kuchanganyikiwa kwa wakati mmoja.
“Kwanini? Si walipaswa kudili na mimi”Aliuliza Regina.
Muda ule ndio Regina alianza kukumbuka mazungumzo yake na Hamza , pia kuhusu yeye kuwa na group la damu sawa na Irene.
“Madam ni kipi ambacho hatujui , ni kheri ukaongea ukweli la sivyo familia yako itakuwa hatarini”Aliongea Regina akimwangalia Bibi yake Irene.
“Unapaswa kujua nguvu ya watu wa Binamu , wakipanga kuua mtu ni rahisi sana, kama jaribio lao la kwanza limefeli ni hakika wakijaribu tena lazima wafanikiwe maana watajipanga zaidi”aliongea.
“Hapana! Sio kama najaribu kuficha, nimemuahidi Madam , siwezi kuongea chochote”
“Kila kitu kinakaribia kuwa wazi , unadhani utaweza kuficha ?”Aliongea Hamza.
“Mama wanaongea nini. Nini kinaendelea”Aliongea Baba yake Irene akionekana kuwa katika hali ya kuchanganyikiwa.
“Mwanangu! Baba yako sio baba yako wa damu. Kabla sijakutana na baba yako nilikuwa tayari mjamzito na baba yako ni babu yake Regina, Mzee Dosam”
Mara baada ya kauli hio kumtoka , mwili wa Baba yake Irene ni kama umefunikwa na ubaridi mkali na kupelekea viungo vyake kufa ganzi.
Regina pia mara baada ya kusikia ukweli huo , alijikuta akishikwa na mshangao mkubwa kiasi cha kutoweza kuongea neno.
Hamza upande wake hakuonyesha mshangao zaidi ya kuvuta pumzi na kuzishusha.
“Kipindi cha nyuma mimi na Mariposa tulikuwa vijakazi tuliotoka Bondeni pamoja na Mzee Dosam na Madam lakini ndio yakutokea yakatuokea....” Alisita akionekana kushindwa kuongea.
“Baada ya kugundua ni mjamzito Madam alishindwa kunivumilia na Mzee Dosam alinikingia kifua lakini mwisho wa siku akaniambia niondoke. Nilikuwa mwanamke ambae sijazoea mazingira ya ulimwengu wa kawaida yalivyo kutokana na kukulia Bondeni na sikuwa na elimu yoyote wala ujuzi wa kunifanya niajiriwe , mwisho wa siku katika kujihangaikia ndipo nilipokuja kukutana na Shedrack , mwanzoni alikuwa akionyesha kunipenda na ujauzito wangu , lakini mara baada ya kumzaa Patrin, alitaka nimzalie mtoto mwingine lakini sikuwa tayari bado.Mwisho wa siku alikasirika na kunipa talaka, baada ya muda mfupi baadae akapoteza maisha. Ndio nilipoamua kumpatia Patrin jina la mwisho la ukoo wangu na maisha yakaendelea. Baada ya kumuona Patrin mwanangu akikua mpaka kuanzisha familia yake , nilidhani nitafurahia maisha ya amani na wajukuu, lakini bado watu wa Bondeni inaonekana hawakutaka kuniacha huru..”
Baba Irene mara baada ya kusikia hayo yote alijikuta mshituko wake ukigeuka na kuwa huzuni na mawazo.
“Mama! Kwanini hukuniambia hayo yote?Ulionekana kuteseka mno , lakini mimi mwanao mpaka umri huu sijui chochote” Alijikuta akimshika mama yake mkono na kuanza kutoa machozi ya kiume.
Regina machozi pia yalikuwa karibu , ijapokuwa alikuwa bibi yake aliemfukuza , lakini alishindwa kujizuia na kuhisi haikuwa rahisi kwake.
Kumfukuza mfanyakazi wa ndani na kufanya kila liwezekanalo kutojulikana yeye na historia yake na kuwaacha wajitegemee wenyewe...
Regina hakuwahi kuwaza mambo hayo yalifanywa na bibi yake.
Hamza alijikuta akivuta pumzi na kujiambia ndio maana bibi huyo alionekana kuwa na chuki siku aliomuona na Irene , kumbe chanzo ni hayo yote.
Comments